Wazee wetu walisema, “Kawaida ni kama sheria.” Ni kweli. Sasa imekuwa kama sheria ile ya kawaida ya mstaafu anapofikisha miaka 60, akiwa na miaka 40 ya kuwa mwajiriwa, maradhi huanza kugeuza mwili wake kuwa eneo la kujidai la maradhi nyemelezi.
Huyu mstaafu alifanya kazi njema akiwa mwajiriwa kwa miaka 40 na hakusumbuliwa na maradhi makubwa zaidi ya yale ya kawaida, kuumwa kichwa, tumbo, mafua, na kuharisha kulikofuata siku za vilaji na vinywaji, kulipiza mchango wake aliochangia harusi ya jamaa au rafiki!
Haya yalikuwa ni maradhi madogo tu, ambayo dokta Mbotoni wa iliyokuwa zahanati ya shirika alilokuwa akifanyia kazi mstaafu wetu, alitumia vidonge na sindano mbili au tatu tu kuyafanya yachape lapa na kuondoka kwenye mwili wa mstaafu fasta!
Haya magonjwa nyemelezi ya ukubwani hayakupata hata kujua jina la mstaafu, achilia mbali kumuingia, maana dawa zilikuwa tele za kuhakikisha kila saa yu mzima na ‘fit’ ili kulijenga taifa. Ole wake mstaafu! “Barabara murefu haikosi kona,” aliimba Dk Remmy.
Haya, mstaafu wetu akafikisha miaka 60 yake, na sheria tuliyojiwekea wenyewe ikamtaka, “Aachie ngazi, babu mchuma, uondoke.” Akastaafu na ‘kipinda mgongo’ cha vimilioni vyake 39 baada ya ajira ya miaka 40 ya kulijenga taifa! Halafu leo kuna watu wanapata ‘kiinua mgongo’ kweli cha shilingi milioni 400 kwa ajira ya miaka mitano ya kuunga mkono hoja!
Ghafla, yale magonjwa yaliyokuwa yamekaa pembeni, yakisubiri mstaafu astaafu, sasa yakajitokeza kwa mbwembwe, na ghafla mstaafu akawa makazi rasmi ya magonjwa nyemelezi ya shinikizo la juu na la chini la damu, matatizo ya moyo, na kisukari, ambacho mstaafu wetu mpaka leo bado anajiuliza, likuwaje kuitwa ugonjwa huo kisukari wakati hauna utamu wowote, bali shubiri!
Naam, maradhi nyemelezi yakafanya mwili wa mstaafu wetu kuwa makazi yake rasmi ya kujidai, na yakajidai kweli, yakijua kuwa mstaafu ameishastaafu. Matibabu ya dezo aliyokuwa akiyapata ya shirika alilofanyia kazi kwa miaka 40 sasa ni historia. Ili kuyathibiti ilihitaji pesa yake ya mfukoni, ambayo baada ya kustaafu sasa imekuwa ‘bidhaa adimu!’
Pensheni ya shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi, matibabu ya bure kwa wazee kuanzia miaka 60 sasa yamekuwa maneno ya kanga tu, na kubaki kutegemea bima ya afya ya watoto wetu ambao wengi bado wanasaka ajira kwa tochi!
Tabu kubwa inayompata mstaafu ni gharama kubwa za vifaa vinavyohitajika kutibu maradhi nyemelezi ya wazee, ambayo sasa ni kama yamepata eneo la kujidai kwenye mwili wake. Ametakiwa amiliki kipima joto kwa ajili ya kupima joto lake asubuhi na jioni. Bei ya kipima joto cha chini kabisa ni shilingi laki moja na elfu kumi!
Anatakiwa kuwa na mashine ya kupima sukari yake asubuhi na jioni. Kimashine cha kupimia sukari cha chini kabisa ni elfu sabini. Kitobolea cha kutoa damu yake kwenye kidole ili ipimwe, kifuko chenye vitoboleo 50 ni shilingi elfu 40, na ‘slide’ za kuweka kwenye kimashine ili kupima sukari ni shilingi elfu 20 kwa vi-slide 20, kwa kifuko kimoja kitakachokuwezesha kupima sukari kwa siku 10 tu!
Ukijumlisha, kila siku anatakiwa kumeza vidonge vitatu tofauti ambavyo bei yake ni ‘mama wee!’. Kwa pensheni ya shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi, mstaafu anaishia kuiona Kinondoni ile, ikimkonyeza fasta awe mkazi wa kudumu huko!
Ndio maana mstaafu anajikuta akilazimika kujifanya mganga wa kienyeji, na anashukuru, angalau maradhi yake yamemfanya awe na PhD ya tiba mbadala ya vitunguu, saumu, tangawizi, mdalasini, magome ya mzamarau, na kadhalika, pale pensheni yake bidhaa adimu, ambayo ni mara nyingi tu!
Matibabu ya bure yamekuwa ni maneno ya kanga, pensheni ndio hiyo laki moja na nusu kwa mwezi, basi angalau Siri- Kali isaidie kupunguza gharama za vifaa vya kutibu magonjwa nyemelezi ya wazee. Inawezekana.