Mbeya. Taharuki imetanda kiwanda cha Wakulima wa Chai kilichopo Katumba wilayani Rungwe mkoani Mbeya kufuatia wafanyakazi 216 kuandamana kwa mabango kupinga kufukuzwa kazi wakidai stahiki zao, huku wakiiomba serikali kuingilia kati.
Imeelezwa kuwa tangu kufungwa kwa kiwanda hicho Mei 9 mwaka huu, zaidi ya wakulima 15,000 wameathirika na baadhi wameanza kutelekeza mashamba yao na wengine kuhamia kilimo cha mazao mengine na kuathiri uchumi wa Wilaya hiyo.
Wakizungumza leo Alhamisi Oktoba 2 wakati wa maandamano hayo, wafanyakazi hao wamesema msimamo wao ni kuendelea na kazi hadi waajiri wao Tatepa na Maris Afrika (wawekezaji kiwandani hapo) watakapowalipa stahiki zao zaidi ya Sh2.17 bilioni.

Mwenyekiti wa kamati ya madai ya wafanyakazi kiwandani hapo, Robert Shayo amesema barua waliyopokea kutoka kwa waajiri kufukuzwa kazi imeibua mshtuko na sintofahamu.
Amesema jumla ya wafanyakazi 216 ndio walipokea barua ya kufukuzwa kazi, wakidaiwa hadi Septemba 30 wawe wameondoka ofisini, kinyume na makubaliano ya mkataba.
“Msimamo ni kubaki hapa kazini, tunadai mafao NSSSF, madai ya likizo na malipo mengine ya kisheria kwa mujibu wa mkataba kazini, wametushtukiza sana,” amesema Shayo.
Kuhusu kuendelea kubaki kazini ilhali barua inawataka kuondoka, Shayo amesema gharama zitaongezeka kisheria kwakuwa kumekuwapo kukiuka utaratibu wa kuwaondoa kazini.

Meneja wa kiwanda hicho, Stanslaus Benela amesema hawapo tayari kuondoka kazini, akieleza kuwa tangu kufungwa kiwanda hicho imeathiri uchumi wa wananchi wa Rungwe na wakulima wenyewe na kushusha pato la Taifa.
Amesema hadi sasa wapo wakulima walioanza kutelekeza mashamba yao, wengine wakihamia kilimo cha mazao mengine kwa kung’oa zao la chai akiomba serikali kuingilia kati suala hilo ili kupata mwekezaji mpya.
“Wakulima zaidi ya 15,000 wameathirika, lakini uchumi wa wananchi na Wilaya hii kwa ujumla umeshuka na kuigusa Taifa kwakuwa huduma ya maji na umeme bili hazilipwi, jamii iliyozunguka kiwanda nao wameguswa,” amesema.
“Taasisi za kifedha ambazo zilikuwa hapa Rungwe zikipokea mishahara ya wafanyakazi na wakulima kupitishia malipo yao hakuna tena, mifuko ya hifadhi ya jamii nayo haipokei kitu,” amesema meneja huyo.

Naye Katibu wa Umoja wa Wafanyakazi wa Kilimo mashambani Mkoa wa Mbeya (TPAWU), Jacline Novat amesema wamependekeza muajiri kutoa mshahara wa msingi kwa mfanyakazi, malipo ya likizo, cheti cha utumishi, tuzo ya muda ya mrefu.
Amesema muajiri pia ameombwa kulipa Sh500,000 kwa kila mfanyakazi kwa kutambua mchango wake, kodi ya nyumba ya miezi mitatu, na waajiriwa nje ya Tukuyu walipwe nauli zao.
“Kwa maana hiyo tunasubiri mrejesho kutoka kwa muajiri Jumatatu ya wiki ijayo ili tujue hatma yetu, kimsingi tuwe na uvumilivu kwakuwa yupo mwakilishi wake ambaye atatupa taarifa” amesema Jacline.

Mwakilishi wa Bodi ya Wakurugenzi ya kiwanda hicho (WATCO), Essau Sengo amesema ameona maandamano hayo na kikao walichokaa atawasilisha kwa muajiri na Jumatatu atatoa mrejesho.
Amesema msimamo wa wafanyakazi hao kubaki eneo la kazi, amewaomba kuwa watulivu akieleza kuwa lengo ni kuona sheria na taratibu zifuatwe ili kila mmoja apate haki yake.
“Kwa niaba ya bodi ya wakurugenzi niwahakikishie nimepokea ujumbe wenu nitaufanyia kazi na Jumatatu wiki ijayo mtapata majibu yenu, kwa maana hiyo mko tayari kusimamia haki zenu kisheria,” amesema Sengo.