Mradi wa kidijitali uchunguzi saratani ya matiti waanza

Dar es Salaam. Serikali imeanza utekelezaji wa mradi mpya wa huduma za saratani ya matiti kuanzia tathmini hadi matibabu kwa kutumia teknolojia ya kidijitali, katika ngazi ya msingi ili kuimarisha utambuzi wa mapema, hususan waishio maeneo ambayo huduma ni ngumu kufikika.

Mradi huo unahusisha upigaji wa picha za matiti kwa kutumia ultrasound, uchunguzi wa chembe kwa kutumia sindano nyembamba (Fine-needle aspiration cytology) na Biopsy kwa sindano kubwa (Core-needle biopsy).

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Oktoba 3, 2025 na Mkurugenzi huduma za afya ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Rashid Mfaume wakati akifungua mdahalo maalumu kando ya Mkutano Mkuu wa 12 wa afya ‘Tanzania Health Summit’, uliojadili mbinu shirikishi za utambuzi wa haraka kwa ajili ya kuboreshwa utambuzi wa mapema wa saratani ya matiti.


Nchini Tanzania, takwimu zinaonesha saratani ya matiti ni ya pili kwa ukubwa ikiwa na asilimia 14.4 ya wagonjwa wapya wa saratani na ni chanzo cha pili cha vifo vya saratani miongoni mwa wanawake.

Saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti kwa pamoja zinachangia zaidi ya nusu ya asilimia 50 wagonjwa wapya wa saratani kwa wanawake nchini kwa mujibu wa takwimu za (Globocan 2022).

Dk Mfaume amesema mradi huo unahusisha  huduma za afya ya kinga uchunguzi na kuwapa rufaa kwenda katika hospitali zenye uwezo wa kugundua saratani, ili kupambana na walio wengi kufika vituoni katika hatua za juu za ugonjwa.

Amesema ikigundulika katika zile hatua za awali, itasaidia matibabu atakayoyapata atapona kabisa.

“Wizara ya Afya, Tamisemi na wadau  tuna ile huduma jumuishi kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii,  jukumu lao mojawapo wanalolifanya ni uchunguzi wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, kundi hili limepewa mafunzo ili kubaini.

“Wakibaini mhusika ana dalili wanampeleka katika vituo vya ngazi ya msingi kama zahanati na vituo vya afya na kupitia sapoti hii na fedha wanazozikusanya kwenye hivi vituo wananunua vifaa vile vidogo vidogo kwa ajili ya uchunguzi wa awali na baadaye kutoa rufaa, badala ya kubaini tayari kuna uvimbe unatoa damu hali ya saratani inakuwa imeshafikia mbali zaidi,” amesema.

Amesema lengo kuu ni kupanua huduma za uelewa, uchunguzi wa mapema, matibabu na huduma za tiba msaada ili kupunguza idadi ya watu wanaougua saratani na kupunguza vifo vinavyotokana nayo.

Amesema hiyo ni sambamba na malengo ya Shirika la Afya Duniani, WHO Global Breast Cancer Initiative inayotaka asilimia 60 ya wagonjwa kugunduliwa katika hatua ya kwanza au ya pili utambuzi wa saratani ya matiti ndani ya siku 60 na asilimia 80 au zaidi ya wagonjwa kupata huduma kamili za matibabu,” amesema Dk Mfaume.

Mkurugenzi Mkazi, Shirika la Jhpiego Alice

Christensen amesema wanashirikiana na Taasisi ya Pfizer Foundation pamoja na Wizara ya Afya, Tamisemi katika kuharakisha mapambano dhidi ya saratani ya matiti nchini.


“Tulifanya mradi wa majaribio kwa kipindi cha mwaka mmoja mwaka 2024, na Pfizer waliridhishwa sana na mradi huo, hivyo tumeuendeleza. Hivi sasa, tumeupanua kuwa mradi wa miaka mitatu. Kama mnavyojua, nchini Tanzania saratani ya matiti ni sababu ya pili ya vifo miongoni mwa wanawake, na bahati mbaya wengi hufika hospitalini wakiwa wamechelewa, saratani imeshasambaa na inakuwa vigumu zaidi kutibu,” amesema.

Amefafanua kuwa Jhpiego inasaidia wanawake kugundua saratani mapema kwa kuwafikia kupitia uchunguzi wa awali. Hii inajumuisha kuongeza uelewa wa jamii, kufanya kampeni kwa kushirikiana na wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili kuwahamasisha wanawake kwenda kupima saratani ya matiti.

Mkurugenzi wa Mradi huo unaofadhiliwa na Pfizer Foundation chini ya usimamizi wa JHPIEGO, Dk Maryrose Giattas Kahwa amesema mradi huo unatekelezwa Tanzania Bara na visiwani katika mikoa 9, halmashauri 45 na wanategemea kuwezesha vituo 137.

Amesema kazi yao kubwa ni kutekeleza programu hiyo ya Serikali kwa kwenda  sambamba na mikakati iliyowekwa na Serikali kwenye kuokoa Watanzania.

“Hivyo tumejikita kwenye uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti na kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha kinamama wanaopata saratani ya matiti wanapata tiba inavyostahili.

“Katika utekelezaji lengo mojawapo ni kuhakikisha tunaongeza uelewa kwenye jamii na kuwajengea uwezo watoa huduma za afya wanaofanya kazi katika vituo vya kutolea huduma ngazi za kituo cha afya, halmashauri, ngazi ya mkoa waweze kufanya uchunguzi wa kina kwa kutumia njia za teknolojia ya kisasa lakini pia kuwajengea uwezo watoa huduma ngazi ya jamii waweze kuwa na ufahamu mkubwa katika masuala ya kuhusu saratani ya matiti,” amesema.

Amesema pia wanawapa elimu kuwa na data za kutosha kulingana na viashiria  vilivyoonekana.

“Pia tunatoa vifaa vya kusaidia kufanya uchunguzi wa kina zikiwemo Ultrasound, tumeenda katika mikoa yote tumekabidhi ultrasound 31 ambazo zitatumika bara, pamoja na visiwani ambazo zimegharimu takribali zaidi ya Sh590 milioni pamoja na vifaa vingine 1000.

“Zaidi ya vifaa tunaboresha rufaa za  wagonjwa wetu wengi tunawapoteza wanapotoka eneo moja kwenda jingine kwa sababu hawana pesa na wengine utakuta hawana bima ya afya, kwahiyo tunashirikiana na wadau wengine kuhakikisha wanapata huduma na tiba ya saratani ya matiti inavyostahili,” amesema.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mama na Mtoto Wizara ya Afya, Dk Nassoro Mzee amesema  saratani ya matiti inaweza kumpata yeyote lakini asilimia 99 wanapata wanawake, lakini asilimia 0.5 huwapata wanaume.

Amesema Jhpiego imekuja na afua tatu katika kupunguza saratani ya matiti ya kwanza kupapasa titi, mama anaweza kufanya mwenyewe na kugundua kama kuna uvimbe na pili anaweza kukamua chuchu kuona kama inatoa damu na majimaji yasiyoeleweka akafanya vipimo zaidi.

“Elimu hii watoa huduma ngazi ya jamii watawapa kinamama wakibaini hatua ya tatu ni kupiga picha kwa kufanya ultrasound na kuona ule uvimbe ni saratani au siyo na nne ni kuchukua kinyama kwa ajili ya vipimo.

“Zamani vituo vyote vya huduma walikuwa wanapapasa na kabla walikuwa wanachukua kinyama kwa kisu ilikuwa inafanya mgonjwa anasubiri muda mrefu na huenda akabadilishiwa vituo kwa ajili ya uangalizi kituo cha kwanza kupapasa, rufaa upasuaji na akaambiwa apeleke kinyama Muhimbili au hospital ya kanda kwa ajili ya vipimo,” amesema.

Amesema wanachokifanya Jhpiego afua zote zinafanyika kwa pamoja katika ngazi ya halmashauri ambako karibu asilimia 80 ya wananchi wanapata huduma za afya katika vituo vya msingi, hivyo huduma hiyo itawafikia wengi na kuondoa usumbufu wa kwenda mijini kupata huduma.

“Huduma hii inatumia teknolojia ya kidijitali unaweza kifanya vipimo,  akaletewa majibu bila kufuata na yatakapoletwa kwenye kituo chako mgonjwa ataendelea kupata matibabu palepale, mradi huu Jhpiego wanaotoa huduma mkoba ambapo pia wanaweza kuchukua kinyama,” amesema Dk Mzee.

Mradi huu wa saratani ya matiti (Beat Breast Cancer Project) unafadhiliwa na Pfizer Foundation chini ya umamizi wa JHPIEGO wakishirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-Tamisemi kwa ufadhili wa miaka mitatu Januari 2025 mpaka Desemba 2027.