Dar es Salaam. Viatu vyenye soli nyembamba mara nyingi huvaliwa na wasichana na wanawake waliochoshwa na uvaaji wa vile virefu, ambavyo huwa na madhara kwa wanaovitumia kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, uvaaji wa viatu virefu mara kwa mara husababisha madhara yanayoweza kutokea kwa muda mfupi au mrefu kulingana na namna ya matumizi.
Kwa mujibu wa tovuti ya Ranka Hospital, madhara yanayoweza kujitokeza haraka ni maumivu ya miguu kutokana na mgandamizo unaowekwa kwenye vidole na sehemu ya mbele ya mguu.
Vilevile, mvaaji hupata malengelenge na michubuko hasa sehemu za kufungia mguu, pia mguu na vifundo vinaweza kuvimba kutokana na mzunguko wa damu kutofanyika vizuri.
Kwa mujibu wa wataalamu, madhara ya muda mrefu ni pamoja na maumivu ya mgongo eneo la chini kutokana na aina hiyo ya viatu kubadilisha mkao wa mwili na kusababisha mgandamizo kwenye uti wa mgongo.
Mvaaji pia anaweza kupata maumivu ya goti, kupinda kwa vidole kutokana na kubanwa muda mrefu, pamoja na kukaza au kudhoofika kwa misuli ya mguu.
Inashauriwa na wataalamu wa afya, viatu virefu visivaliwe kwa muda mfupi na si kila siku, ikipendekezwa badala yake,uvaaji wa vile vyenye soli nyembamba (flat shoes) ambavyo wengi huviita ‘simple’ kutokana na wepesi wake wa kuvaa na kutembea.
Lakini la kujiuliza ni je, uvaaji wa aina hii ya viatu ni kweli hulinda afya ya miguu au huchangia matatizo mengine yasiyoonekana mara moja?
Vilevile, la kujiuliza ni je, viatu hivyo ni kwa ajili ya kutembea navyo mwendo mrefu?
Wataalamu wa afya wanasema ‘simple’ zisizo na soli ya ndani (mara nyingi huwa za mfano wa sponchi laini, mpira au jeli) zinaweza kuongeza hatari ya maumivu chini ya kisigino, mguu mzima na mhusika kuchoka haraka zinapovaliwa kwa muda mrefu.
Vilevile, inaelezwa zinaweza kuathiri mkao wa mgongo kwa kuongeza msongo eneo la chini, kwani mgawanyo usio sawa wa uzito mwilini unaweza kusababisha maumivu ya kiuno na misuli ya miguu.
Frank Arabi, daktari kutoka kitengo cha mifupa katika Hospitali ya CCBRT, akizungumza na Mwananchi Oktoba 2, 2025 amesema mtu anapotaka kuvaa kiatu kitaalamu anatakiwa kuchagua kile chenye soli nene na laini.
Anasema anapovaa kiatu cha aina hiyo kinamsaidia kufanya uvungu (upinde) wa mguu usipoteza umbo lake kwa kiwango kikubwa.
Dk Arabi anasema uvungu wa miguu ni muhimu katika kusaidia kupunguza mgandamizo na kuweka msawazo wa uzito mwili na kutoa msaada kwa miguu.
“Kuna viatu wanapenda kuvaa wanaviita ‘simple’, huwa vina soli nyembamba sana chini, ni hatari. Vinachangia kupata maumivu ya miguu na mgongo,” anasema.
Anasema watu walio katika hatari zaidi ni wanaovaa aina hiyo ya viatu, huku wakifanya kazi za kusimama au kutembea kwa muda mrefu.
“Pia wale wenye uzito mkubwa ni vyema kuwa makini kwani hawa hupata maumivu sana. Ni muhimu mtu anapoamua kuvaa viatu kuzingatia viwe na soli nene na laini,” anasema.
Mtaalamu wa fiziotherapia, Dk Andrew Charles, anasema athari za kutozingatia uvaaji sahihi wa viatu, unaweza usizione mara moja.
“Mtu anaweza asione athari zake kwa mara moja, lakini kwa kutozingatia hilo anajitengenezea changamoto ya maumivu ya miguu kwa baadaye,” anasema.
Utafiti kuhusu uvaaji viatu na madhara kiafya uliofanywa na PubMed Central (PMC) pamoja na machapisho katika mitandao ya Sanders Podiatry na Dovetail Orthopedics, vinaeleza kuwa miguu ya binadamu ina uvungu unaosaidia kusambaza uzito, hivyo simple zisizo na soli ya ndani au zilizotengenezwa pasipo kufuata umbile la uvungu wa mguu, husababisha mguu ubanwe au kulazimika kubeba mzigo wote, hivyo kusababisha uchovu na maumivu ya nyayo na vifundo.
Soli ya ndani (insole) ama iwe ya sponchi, mpira au jeli inaelezwa hupunguza mshtuko na presha mguu unapokanyaga chini wakati wa kutembea au kukimbia, hivyo isipokuwapo husababisha uzito wote wa mwili kusambazwa moja kwa moja kwenye nyayo.
Hali hiyo inaelezwa huongeza presha kwenye visigino na kwenye sehemu ya mbele ya mguu.
Watu wenye miguu isiyo na uvungu au upinde huathirika, hivyo wanahitaji zaidi viatu vyenye kuwapatia msaada, kinyume cha hilo huongeza maumivu na uchovu.
Pia, watu wanaokaa muda mrefu, kusimama au kutembea kazini kama vile watumishi dukani, walimu na wauguzi hupata athari wanapovaa viatu vyenye soli nyembamba visivyosaidia uvungu wa mguu.
Wamo pia watu wanene au wenye uzito mkubwa; wazee ambao misuli na viungo vyao huwa dhaifu na wenye historia ya matatizo ya miguu au viungo.
Mguu wa mwanadamu umegawanyika sehemu kuu tatu ambazo zinashirikiana ili uwe na nguvu, usawa na urahisi wa kusogea, ambazo ni mbele inayojumuisha vidole, ikisaidia kusukuma mwili mbele wakati wa kutembea au kukimbia, pia huchukua sehemu kubwa ya uzito wakati wa kusimama kwa muda mfupi.
Sehemu ya katikati inajumuisha uvungu au upinde wa mguu ambayo ni muhimu kwa kusambaza uzito wa mwili, kupunguza mshtuko na kutoa msaada kwa mguu.
Vilevile, sehemu ya nyuma ya mguu inayojumisha kisigino na mfupa wa nyuma ambayo hubeba uzito mkubwa wa mwili wakati wa kusimama na kuanza kutembea. Pia husaidia katika mwelekeo wa mguu na kuweka uwiano sawa wa mwili.
Kila sehemu ya mguu hutegemea misuli, mishipa na viungo vya ndani ili kuruhusu harakati na ustahimilivu.
Watu wanavaa viatu vyenye soli iliyochakaa nao wanakuwa katika hatari ya kupata changamoto ya maumivu ya miguu na mgongo kutokana na kushindwa kusaidia uvungu wa mguu kupunguza mgandamizo.
Pia kwa viatu ambavyo vimeisha upande mmoja husababisha mgongo kutokuwa katika msawazo pale mtu anapokaa, kusimama au kutembea.
Vilevile, unapotakiwa kuchagua viatu vya kuvaa ni vyema kuhakikisha vinakutosha vizuri, havibani wala kumpwaya.
Soli ya kiatu inapaswa kuwa yenye upana wa wastani na laini ili kusaidia kutoharibu umbo la uvungu wa mguu.
Inasisitizwa kuzingatia aina ya shughuli au kazi anayofanya mvaaji, hali ya hewa na afya ya miguu.