TCU kuongeza siku 4 za udahili

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kuongeza muda wa udahili kwa mwaka wa masomo 2025/2026 kwa kuweka awamu ya tatu na yamwisho anayotarajiwa kufunguliwa Oktoba 6, na kufungwa Oktoba 10, mwaka huu.

Hayo yamaelezwa leo Oktoba 3, 2025 na Katibu Mtendaji wa TCU Profesa Charles Kihampa kupitia taarifa yake iliyowekwa kwenye tovuti hiyo imeeleza kuwa majina ya waombaji waliopata nafasi katika awamu ya pili yatatangazwa na vyuo husika kuanzia Oktoba 6, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ongezeko la muda linalenga kutoa nafasi kwa wanafunzi walioomba katika vyuo zaidi ya kimoja na ambao hawakuthibitisha nafasi zao katika awamu ya kwanza.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa waombaji waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja katika awamu ya pili, pamoja na wale ambao hawakuthibitisha nafasi zao awali, wanapaswa kuthibitisha chuo wanachokusudia kusoma kati ya Oktoba 6 hadi 19, 2025.

“Uthibitisho huo utafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu au barua pepe wakati wa maombi. Kwa wale watakaoshindwa kupokea ujumbe huo kwa wakati, TCU imewaelekeza kuwasiliana na mifumo ya udahili ya vyuo husika ili kupata msaada,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha TCU imeeleza kuwa orodha kamili ya majina ya waombaji waliodahiliwa katika zaidi ya chuo kimoja itapatikana kwenye tovuti ya Tume (www.tcu.go.tz) kuanzia Oktoba 6.

Pamoja na kukamilika kwa awamu mbili, TCU imesema imepokea maombi kutoka Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso) na vyuo vikuu mbalimbali ya kuongezwa muda wa udahili kwa waombaji waliokosa nafasi.

Kutokana na maombi hayo, tume imekubali kufungua awamu ya tatu na ya mwisho ya udahili kuanzia Oktoba 6 hadi 10, 2025, ili kutoa nafasi kwa wanafunzi waliokosa nafasi katika awamu zilizopita na kwa programu ambazo bado zina nafasi wazi.

Taarifa inasema ifikapo Oktoba 20, 2025 Vyuo vitatangaza majina ya waliodahiliwa katika awamu ya tatu na Oktoba 20, hadi Novemba 3, 2025 itakuwa ni kuthibitisha udahili kwa waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja katika awamu ya tatu na wale walioshindwa kuthibitisha udahili wao katika awamu za udahili zilizopita.

Katika taarufa hiyo TCU imewataka waombaji wote ambao bado hawajapata nafasi au hawakuweza kuomba kwa sababu mbalimbali kutumia ipasavyo fursa ya awamu ya tatu. Aidha, imeelekeza vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kuendelea kutangaza programu ambazo bado zina nafasi ili kuhakikisha waombaji wapya wanazifahamu.

Tume pia imekumbusha kuwa masuala yote yahusuyo udahili na uthibitisho wa nafasi yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vyuo vyote vimeagizwa kushughulikia changamoto za wanafunzi kwa haraka na kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa.

Kwa mujibu wa TCU, hatua hii inalenga kuhakikisha kila mwombaji anayestahili na mwenye sifa anapata nafasi ya kujiunga na elimu ya juu, huku vyuo vikuu vikihimizwa kutumia nafasi zilizopo ipasavyo kabla ya kufungwa rasmi kwa udahili wa mwaka wa masomo 2025/2026.