Dar es Salaam. Kila ninapofika sehemu mpya kwenye dunia huwa nina tabia ya kulinganisha hali nionayo na hali tuliyonayo nyumbani Tanzania. Sio kwa lengo la kubeza bali kwa kutafuta yale mazuri ambayo tunaweza kuyaiga na kujifunza ili kuyatumia kuimarisha maisha yetu na uchumi wetu.
Safari yangu ya hivi karibuni nchini China imenipa masomo kadhaa ya kibiashara ambayo naamini yanaweza kutusaidia sana. Wiki moja iliyopita nilikuwa Beijing, mji mkuu wa China, taifa lenye nguvu ya pili kubwa zaidi kiuchumi duniani baada ya Marekani, namba mbili kwa idadi ya watu baada ya India na kinara wa dunia katika uzalishaji wa viwandani.
Safari yangu haikuishia Beijing pekee, bali nimezunguka pia katika majimbo na miji mbalimbali ikiwamo Guangzhou, Shandong, Fujian, Shanghai na Shaanxi. Katika kila mahali ninapopita, napata darasa jipya kuhusu namna Wachina wanavyopanga shughuli zao za biashara na uzalishaji.
Nisije kueleweka vibaya siandiki makala hii kwa mtindo wa hotuba za hamasa kwamba “tunaweza kuwa kama China kesho.” La hasha. Najua mazingira yetu ni tofauti. Ninachojaribu kuonesha hapa ni mambo machache ambayo, tukiyazingatia, yanaweza kutupatia mwanga wa namna ya kuboresha biashara na masoko yetu nyumbani.
Serikali ya Tanzania kwa muda imeweka msukumo mkubwa wa kukuza biashara kama njia ya kuongeza mapato ya wananchi na taifa. Tumeshuhudia uwekezaji katika miundombinu ya masoko, barabara, bandari na sera za kusaidia sekta binafsi. Hata hivyo, matokeo hayajawa makubwa kama yalivyotarajiwa. Masoko mengi hayafanyi kazi kwa ufanisi, baadhi yanadoda baada ya muda mfupi. Swali ni kwa nini?
Utaratibu wa Wachina Sokoni
Moja ya mambo yaliyovutia macho yangu ni namna masoko na maduka makubwa ya China yanavyopangwa. Kila ghorofa au eneo linauza bidhaa maalumu pekee. Ukienda ghorofa ya kwanza utakuta bidhaa za aina fulani tu, ya pili bidhaa tofauti, na kuendelea. Ukianza kusaka viatu, unaweza kutembea maduka zaidi ya 200 yenye bidhaa sawa lakini zenye ubora, chapa na bei zinazoshindana.
Ni nadra sana kukutana na mchanganyiko holela wa bidhaa yaani duka la vipodozi liko karibu na duka la mchele, au duka la simu liko jirani na fundi spana. Kwao, kila kitu kina nafasi yake. Matokeo yake ni kwamba mteja ana uhakika wa kukuta wingi wa bidhaa na kufanya uamuzi sahihi kwa kulinganisha.
Sasa tazama mfano wetu wa Machinga Complex au Soko la Ndugai Dodoma. Utakuta duka la vipodozi liko karibu na la vifaa vya magari, pembeni yake kuna nafaka. Hali hii inamnyima mteja sababu ya kurudi mara kwa mara kwa sababu hana uhakika wa kukuta anachokitafuta katika wingi na tofauti. Ndiyo maana masoko yetu mengi huishia kudorora.
Tunachoweza kujifunza ni kuweka msisitizo katika “umaalumu wa biashara.” Tukiamua eneo fulani ni la kuuza bidhaa za elektroniki, basi tuwekeze huko, tuamue kila mteja akifika pale atapata kila kitu kuanzia redio, simu, televisheni hadi friji. Ukisema eneo jingine ni la mavazi, basi liwe la mavazi pekee. Mfumo huu si tu unaleta urahisi kwa wateja bali pia unachochea ushindani wa kibiashara, hivyo kushusha bei na kuongeza ubora.
China haikusimama tu katika upangaji wa masoko. Wamepiga hatua zaidi kwa kugawa majimbo yao kulingana na umaalumu wa uzalishaji. Kila jimbo au mji unajulikana kwa kitu fulani. Yapo maeneo mashuhuri kwa nguo na viatu, mengine kwa vifaa vya ujenzi, vingine kwa teknolojia ya kisasa, mitambo au kilimo cha aina fulani. Matokeo yake ni kuibuka kwa chapa kubwa za kimataifa na ushindani wa kitaifa.
Hii ni dhana ambayo Tanzania inaweza kuanza kuitekeleza taratibu. Hebu tujiulize: kwa nini Mkoa wa Pwani usibadilishwe kuwa kitovu cha viwanda vidogo na vya kati? Kwa nini Mwanza isiwe kitovu cha teknolojia ya kielektroniki, Tanga ikajikita katika uchumi wa buluu na vifaa vya majini, huku Kilimanjaro ikizingatia kilimo cha bustani na bidhaa za chakula?
Mfumo huu si marufuku kwa shughuli nyingine, bali ni msisitizo wa maalumu. Umaalumu huzaa utaalamu, kuongeza tija na kuimarisha ufanisi.
Somo jingine kubwa kutoka China ni namna walivyowekeza katika teknolojia na ubunifu. Hata masoko ya kawaida ya mitaani yanatumia mifumo ya kidijitali ya malipo. Hii si tu inarahisisha biashara bali pia inapunguza wizi na kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi.
Kwa Tanzania, bado tupo nyuma. Wakati tunazungumzia uchumi wa kidijitali, bado wafanyabiashara wengi wadogo wanatumia daftari na hesabu za kichwa. Tukiamua kwa dhati, tunaweza kuwekeza katika teknolojia rahisi za malipo na usimamizi wa biashara, tukaanzia maeneo maalumu kisha tukasambaza kote nchini.
Bila shaka, Tanzania tuna changamoto zetu. Soko letu bado dogo, mtaji ni mdogo, teknolojia ni finyu na mara nyingine urasimu ni kikwazo. Lakini mifumo kama hii ya umaalumu inaweza kuanza kidogo kidogo. Tunachohitaji ni sera thabiti, uwekezaji wa kimkakati na kushirikisha sekta binafsi.
Mfano rahisi ni sekta ya kilimo. Tumezoea kila mkoa kulima kila kitu. Matokeo yake ni ushindani usio na tija na bei kushuka bila faida kwa mkulima. Tukiamua mazao fulani yalimwe zaidi katika mikoa maalumu, tunaweza kuongeza ubora na uzalishaji, na kuvutia masoko ya ndani na nje.
Somo kuu kutoka China ni kwamba biashara inahitaji upangaji, umaalumu na nidhamu. Hawawezi kuwa kinara kwa bahati mbaya; wamepanga kila kitu kwa makini kuanzia masoko, viwanda hadi majimbo.
Tanzania tuna fursa kubwa ya kujifunza na kuboresha. Tukiamua kupanga masoko yetu vizuri, kuamua kila eneo lijulikane kwa kitu fulani, kuwekeza katika teknolojia na kuhamasisha umaalumu wa uzalishaji, basi tunaweza kupiga hatua kubwa.
China walipoanza miaka ya 1970 hawakuwa tofauti sana na sisi. Leo hii ni taifa namba mbili kiuchumi duniani. Tunapaswa kujifunza na kuchukua yale yanayowezekana kwa mazingira yetu. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumejipanga si tu kwa ajili ya leo bali kwa vizazi vijavyo.