Shauri la Chadema dhidi ya Msajili lasimama kwa muda usiojulikana

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Manyara, imesimamisha kwa muda usiojulikana usikilizaji wa shauri la mapitio ya mahakama, lililofunguliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kutowatambua viongozi wake wa sekretarieti.

Uamuzi huo umetolewa jana Alhamisi, Oktoba 2, 2025 na Jaji Nenelwa Mwihambi, kutokana na kuwapo taarifa ya kusudio la wajibu maombi kukata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama wa kuwaruhusu waombaji kufungua shauri hilo.

Jaji Mwihambi katika uamuzi wake amekubali hoja za wajibu maombi kupitia Wakili wa Serikali, Erigh Rumisha kuwa kutokana na kuwapo taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani, mahakama hiyo (Mahakama Kuu) inaondolewa mamlaka ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo.

Mbali na hilo, baada ya kujadili hoja za pande zote na kurejea sheria na uamuzi wa kesi mbalimbali zilizokwisha kuamuliwa na mahakama hiyo na Mahakama ya Rufani, Jaji amekataa ombi la Wakili Rumisha aliyeomba shauri hilo litupwe.

Badala yake, Jaji Mwihambi amekubali hoja za mawakili wa Chadema wakiongozwa na Mpale Mpoki, hivyo ametoa uamuzi wa kusimamisha usikilizwaji wa shauri hilo kusubiri hatima ya taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

“Mahakama hii inatambua kwamba mamlaka yake yameondolewa na uwepo wa taarifa ya rufaa katika Mahakama ya Rufani. Hata hivyo, sishawishiki na hoja ya wakili wa Serikali kwamba nifute shauri hili,” amesema Jaji Mwihambi na kuhitimisha:

“Badala yake, kwa kuzingatia mazingira ya shauri hili, ninaona ni muhimu kuahirisha mchakato wa shauri hili hadi pale rufaa itakapopitiwa na kuamuliwa, au taarifa ya rufaa itakapoondolewa. Imeamuriwa hivyo.”

Shauri hilo linatokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kutowatambua viongozi wa sekretarieti ya Chadema walioteuliwa na kupitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho Januari 22, 2025.

Msajili alitoa uamuzi huo baada ya kukubali pingamizi lililowasilishwa kwake na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Mwanga, Lembruce Mchome.

Katika pingamizi hilo, Mchome alidai viongozi hao si halali kwa kuwa akidi ya wajumbe wa Baraza Kuu lililowapitisha viongozi hao haikuwa imetimia.

Viongozi hao ni katibu mkuu, naibu katibu mkuu (Bara na Zanzibar) na wajumbe watano wa kamati kuu walioteuliwa na mwenyekiti wa chama hicho.

Kutokana na uamuzi huo, msajili alikitaka chama hicho kurekebisha kasoro hiyo kwa maana ya kuitisha upya baraza kuu lenye akidi sahihi na kuwapitisha tena viongozi hao, huku akitoa uamuzi wa kusitisha ruzuku ya chama hicho mpaka kitakapotekeleza maelekezo hayo.

Chadema haikuridhishwa na uamuzi wa Msajili ikafungua shauri la maombi mchanganyiko namba 19054/2025 mahakamani hapo, pamoja na mambo mengine ikiomba kibali cha kufungua shauri la mapitio ya mahakama kuupinga uamuzi wa Msajili.

Mahakama katika uamuzi uliotolewa Agosti 28, 2025 ilikubali maombi hayo ikaridhia chama hicho kufungua shauri ndani ya siku 14.

Waombaji walitekeleza uamuzi huo kwa kufungua shauri la maombi ya mapitio namba 23268/2025 lililofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa Chadema dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika shauri hilo, Bodi hiyo inaiomba mahakama itengue uamuzi wa Msajili na itoe amri ya zuio dhidi yake ya kutokukiingilia chama hicho.

Wajibu maombi hawakuridhika na uamuzi wa mahakama, wakaanza mchakato wa kukata rufaa Mahakama ya Rufani kwa kuwasilisha kusudio la kukata rufaa kabla ya kuwasilisha sababu za rufaa.

Katika majibu yao kupitia kiapo kinzani, pia wajibu maombi waliambatanisha taarifa ya pingamizi la awali wakidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa kuna rufaa inayoendelea mbele ya Mahakama ya Rufani dhidi ya uamuzi huo.

Siku ya usikilizwaji wa pingamizi hilo hapakuwapo ubishi kutoka pande zote, kwamba taarifa ya kukata rufaa iliwasilishwa Mahakama ya Rufani Septemba mosi, 2025 na kwamba, jambo hilo linaathiri mamlaka ya mahakama hiyo kuendelea na shauri hilo.

Hata hivyo, mawakili walitofautiana juu ya hatua sahihi ya kuchukua.

Wakili Rumisha aliomba shauri hilo litupiliwe mbali akiirejesha mahakama katika uamuzi wake kwenye shauri la Legal and Human Rights Center dhidi Waziri wa Fedha na Mipango na wenzake, (Shauri la Maombi Mchanganyiko namba 28/2022).

Alisisitiza kuwa Mahakama ya Rufani katika kesi ya Exaud Gabriel Mmari dhidi ya Yona Seti Akyo na wenzake, rufaa ya madai namba 91/2019, iliyoamuliwa mwaka 2021, Mahakama ya Rufani limlaumu jaji wa mahakama ya chini kwa kuendelea na shauri wakati alikuwa anafahamu kwamba kulikuwa na taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Aliiomba mahakama ijiepushe kutoa uamuzi unaopingana, kama ilivyoelekezwa katika shauri la ULC (Tanzania) Ltd dhidi ya National Insurance Corporation na mwenzake (2003) kwamba majaji wa mahakama moja wasitoe uamuzi unaokinzana kuhusu hoja zinazofanana.

Wakili Mpoki aliomba shauri hilo lisifutwe bali lisogezwe mbele kwa muda usiojulikana kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani.

Aliirejesha mahakama katika uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika kesi ya Arcado Ntagazwa dhidi ya Buyogera Bunyambo (1997) kama ilivyorejelewa katika kesi ya Exaud Gabriel Mmari.

Alidai kulifuta shauri hilo, kutakuwa ni kuingilia mamlaka ya Mahakama ya Rufani. Alisisitiza kikanuni Mahakama Kuu haifungwi na uamuzi wake wa awali.

Hivyo, aliiomba mahakama isitishe usikilizaji wa shauri akidai hiyo ndiyo hatua sahihi.

Jaji Mwihambi katika uamuzi amesema kila shauri linaamuliwa kulingana na mazingira yake binafsi.

Amesema Mahakama ya Rufani katika kesi ya Arcado Ntagazwa dhidi ya Buyogera Bunyambo ilirejelea uamuzi wake katika kesi ya Milcah Kalondu Mrema dhidi ya Felix Christopher Mrema (rufaa ya madai namba 64/2011).

Amesema Mahamama ya Rufani ilisema mara tu taarifa rasmi ya kusudio la kukata rufaa inapowasilishwa kwenye Ofisi ya Msajili, jaji wa mahakama ya awali alikuwa na wajibu wa kusitisha mchakato mara moja na kuruhusu mchakato wa rufaa kuchukua nafasi au hadi taarifa hiyo iondolewe.

“Kwa hiyo, mwongozo uliotolewa na Mahakama ya Rufani katika mazingira yanayofanana na shauri la sasa ni kwamba mchakato unapaswa kusitishwa,” amesema.

Jaji Mwihambi amesema kwa sasa ana machaguo mawili kama walivyoeleza mawakili; ama kufuta shauri au kuahirisha usikilizaji wake kwa muda usiojulikana.

Amesema iwapo shauri litafutwa na Mahakama ya Rufani ikaamua rufaa kwa manufaa ya mwombaji, basi atalazimika kuwasilisha tena maombi upya.

Lakini iwapo shauri litaahirishwa kwa muda usiojulikana na Mahakama ya Rufani ikaamua rufaa kwa manufaa ya mwombaji, basi shauri litaendelea pale lilipoishia.

Amesema anakubaliana na hoja ya Wakili Rumisha, kwamba majaji wa mahakama moja hawapaswi kutoa uamuzi unaopingana kuhusu hoja zinazofanana, akisisizitiza isipokuwa pale inapolazimu kufanya hivyo.

Hata hivyo, amesema anaona ni muhimu kutofautiana na uamuzi katika kesi ya Legal and Human Rights Center (supra) na kwamba, badala yake anafuata msimamo wa Mahakama ya Rufani katika kesi ya Arcado Ntagazwa dhidi ya Buyogera Bunyambo kwamba, hatua inayopaswa kuchukuliwa katika mazingira kama haya ni kusitisha mchakato.