Fursa za kiuchumi katika kipato halali

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na hamasa kubwa ya watu kujaribu fursa za biashara, uzalishaji na ajira binafsi, hasa kutokana na uwepo wa mitandao ya kijamii. Wito wa kutafuta “mkwanja” umekuwa kama wimbo unaorudiwa na vijana wengi.

Mtandaoni tunashuhudia kila aina ya mbinu za upatikanaji wa fedha kwa haraka. Hata hivyo, katikati ya shauku hii kuna ulazima wa kujiwekea mipaka; tuzoeshe nafsi zetu kutafuta kipato kinachotokana na shughuli halali, kinachokubalika na sheria, maadili na imani zetu.

Kwa maana rahisi, “halali” ni kile kinachokubalika. Dhana hii haina tafsiri moja tu, inaweza kutofautiana kulingana na mfumo wa sheria wa nchi, misingi ya dini au mazoea ya jamii. Kwa mfano, shughuli inayoruhusiwa kisheria inaweza kuonekana isiwe na heshima katika mila zetu, au ikawa dhambi katika dini fulani.

Aidha, baadhi ya nchi zinaruhusu biashara ya ukahaba kwa mujibu wa sheria zao, lakini jamii nyingi huiona kama fedheha, na katika imani nyingi za kidini ni kosa. Hivyo, wakati tunapotathmini uhalali wa chanzo cha kipato, tuangalie zaidi ya tu kile kinachoandikwa kwenye vitabu vya sheria.

Kujishughulisha na shughuli zisizo halali siyo tu ni uvunjaji wa sheria, bali ni kukiuka kanuni za maadili na utu. Shughuli nyingi haramu zinatoa faida kubwa kwa haraka, lakini pia zinaacha maumivu yasiyoponyeka na athari mbaya kwa wahanga wake. Hazijengi hadhi yetu wala kuheshimu utu wa wengine. Badala yake, zinapanda mbegu ya uovu na kuzidisha mateso.

Mfano mmoja wa shughuli hizi ni biashara haramu ya usafirishaji watu, ajira za kulazimishwa na uuzaji wa viungo vya binadamu. Uhalifu wa kimtandao ni mfano mwingine. Katika zama hizi za dijitali, baadhi ya watu wanasumbuliwa na tamaa ya kupata pesa kupitia mbinu za wizi wa kimtandao.

Inaweza kuonekana njia ya mkato ya kuingiza mamilioni, lakini ni wizi unaovunja maisha ya wengine. Watu wanaporwa fedha zao na kuachwa na maumivu makubwa. Hakuna haki katika kuendesha magari ya kifahari au kuishi maisha ya starehe kwa kutumia jasho la watu wengine. Faida unayopata kwa kumuibia mwenzako haiwezi kukuletea amani.

Aidha, kuna biashara ya dawa za kulevya. Huonekana kama sekta yenye faida kubwa kwa wanaohusika nayo, lakini athari zake mbaya ni kubwa zaidi. Inaharibu kizazi cha vijana, inachochea uhalifu na haina msingi wa ujenzi wa jamii yenye afya. Unapokuwa bilionea kwa sababu ya kusambaza uharibifu na uraibu, unawezaje kujisifu? Faida ya haraka inayoharibu maisha ya wengine haijengi jamii bali inaiangamiza.

Kwa upande mwingine, michezo ya kamari na bahati nasibu imekuwa ikitangazwa sana kama njia ya mkato ya kujipatia kipato. Licha ya kuwapo watu wachache wanaoshinda, wengi hupoteza muda na rasilimali zao wakitegemea “bahati.” Vijana wengi wanakuza uvivu na kuacha kufanya kazi au kujishughulisha na shughuli za maana.

Bila kazi halisi, uzalishaji unashuka na jamii inashindwa kusonga mbele. Zaidi ya hapo, tabia ya kutegemea bahati inaweza kusababisha madeni na utumwa wa kifedha. Wengine, wakikosa pesa za kucheza kamari, huelekea kwenye njia nyingine haramu ili kupata fedha za “chapchap”, jambo linalozaa wizi, udanganyifu na uhalifu.

Ni nchi gani imepiga hatua kwa kutegemea kamari? Hakuna. Maendeleo ya kweli yanatokana na ubunifu, bidii na subira katika shughuli halali. Bahati nasibu haiwezi kuwa msingi wa maendeleo ya taifa au jamii.

Ni wakati sasa wa kuona thamani ya fursa halali zilizopo. Soko la kilimo lina nafasi tele kwa wanaoweza kuzalisha kwa njia bunifu na kuongeza thamani ya mazao. Sekta ya teknolojia na ubunifu inafunguka, ikiwaruhusu vijana kuanzisha biashara za kidijitali, ujasiriamali wa kijamii na kazi za kiuhandisi. Sanaa na utamaduni vinatoa fursa za kipato kupitia muziki, filamu, na mengine. Hivi vyote vinaweza kutupatia kipato bila kuvunja sheria au kukiuka maadili.

Ili haya yafanikiwe, serikali na jamii zinapaswa kuweka mazingira rafiki. Sera za kifedha zinazowezesha upatikanaji wa mikopo nafuu, mafunzo ya stadi na ushauri kwa wajasiriamali wapya, pamoja na kulinda haki za kazi.

Wakati huohuo, tunapaswa kutoa elimu ya maadili na uaminifu kutoka ngazi ya familia hadi shule, ili kutengeneza kizazi kitakachothamini uadilifu. Sheria ziimarishwe dhidi ya uhalifu kama usafirishaji haramu wa watu, wizi wa kimtandao, biashara ya dawa za kulevya na kamari isiyo na nidhamu.

Tukichagua kuwekeza nguvu zetu katika shughuli halali, tunajenga msingi imara wa uchumi endelevu. Hata kama mafanikio yanakuja polepole, yana mizizi imara na hayatikiswi na woga wa kufikiri “nitaumbuliwa.”