Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza Desemba 30, 2025 kuwa siku ya kupiga kura katika jimbo la Fuoni, Wilaya ya Magharibi B, Zanzibar.
Hatua hiyo inatokana na kifo cha aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Abass Ali Mwinyi, kilichotokea Septemba 25, 2025. Kutokana na kifo cha mgombea huyo, uchaguzi katika jimbo hilo ulisitishwa.
Mbali na jimbo hilo, INEC pia imepanga Desemba 30 kuwa tarehe ya uchaguzi wa madiwani katika kata mbili za Chamwino, Jimbo la Morogoro Mjini na Mbagala Kuu, jimbo la Mbagala kutokana na vifo vya wagombea wa nafasi hizo.
INEC imesema hatua hiyo imezingatia masharti ya kifungu cha 68(1), (3) na (4) na 71(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Oktoba 3, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima, kutokana na mabadiliko hayo, tume imetoa ratiba mpya ya uchaguzi kwa maeneo husika.
“Siku ya kupiga kura kwa ubunge wa Jimbo la Fuoni na udiwani katika kata za Chamwino na Mbagala Kuu itakuwa Jumanne, Desemba 30, 2025,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema fomu za uteuzi kwa mgombea ubunge jimbo la Fuoni kupitia CCM na wagombea udiwani katika kata za Chamwino na Mbagala Kuu kupitia CUF zitatolewa kuanzia Oktoba 15 hadi Oktoba 21, 2025.
Waliofariki ni mgombea udiwani wa Chamwino, Hassani Salum Hassani aliyefariki dunia Septemba 27, 2025. Siku hiyohiyo, mgombea mwingine wa udiwani, Rajabu Mwanga aliyekuwa akiwania kata ya Mbagala Kuu, alifariki dunia.
Uteuzi wa mgombea ubunge na udiwani wa sehemu husika utafanyika Oktoba 21, 2025.
Kuhusu kampeni, INEC imesema katika jimbo la Fuoni zitaanza Oktoba 22 hadi Oktoba 27, 2025. Oktoba 28 hadi Novemba 4, 2025 kampeni zitasitishwa kupisha upigaji kura ya mapema upande wa Zanzibar na siku ya kupiga kura hadi kutangazwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utafanyika Oktoba 29, 2025.
Baada ya hapo Novemba 5 hadi Desemba 29, 2025 kampeni zitaendelea.
Tume imesema kampeni za uchaguzi wa udiwani Chamwino na Mbagala Kuu zitafanyika kuanzia Oktoba 22 hadi Oktoba 28, 2025 na Oktoba 29 hadi Novemba 4, 2025 kampeni zitasitishwa ili kupisha siku ya kupiga kura na matokeo ya uchaguzi mkuu. Novemba 5 hadi Desemba 29, 2025 kampeni zitaendelea.
INEC imesema kwa mujibu wa kifungu cha 71(2) cha Sheria ya Uchaguzi, uteuzi mpya hautahusisha mgombea mwingine yeyote aliyeteuliwa kihalali katika uteuzi wa awali, isipokuwa pale atakapotoa taarifa ya kujitoa.
Tume imesema imevikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, sheria, Kanuni za Maadili ya Uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yaliyowekwa ili kufanikisha ratiba mpya ya uchaguzi katika maeneo husika.