Jaji Mkuu mstaafu Kenya ajiunga chama cha siasa kumng’oa Ruto madarakani

Dar es Salaam. Jaji Mkuu mstaafu wa Kenya, David Maraga, ambaye aliweka historia barani Afrika kwa kuimarisha heshima na uhuru wa mahakama kwa kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais mwaka 2017, sasa amejiunga rasmi na chama kipya cha United Green Movement (UGM) kwa lengo la kumkabili Rais William Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Maraga, ambaye alistaafu mwaka 2021 akiwa Jaji Mkuu wa 14 wa Kenya, hakustaafu kama jaji wa kawaida,  aliondoka akiwa sauti ya maadili na ujasiri wa kikatiba.

Badala ya kujitenga na shughuli za kijamii, alijiunga na uanaharakati wa kiraia, akionekana hadharani katika maandamano ya vijana wa kizazi kipya (G-Z), ambapo alilaani matumizi ya nguvu kupita kiasi na mashambulizi ya polisi kwa silaha za moto, dhidi ya waandamanaji.

Maraga ni mwanasiasa mpya kabisa, ambaye hajawahi kuwania nafasi yoyote ya kisiasa, na hakujiunga na wanasiasa wakongwe wa nchi, kama wengine.

Mfano, Naibu Rais aliyeondolewa madarakani, Rigathi Gachagua ametangaza kuungana na wanasiasa wakongwe kupambana na Rais Ruto.


Gachagua tayari ametangaza kuungana na Kalonzo Musyoka (Kiongozi wa Chama cha Wiper), Eugene Wamalwa  (Kiongozi wa DAP-K), Martha Karua (Kiongozi wa NARC Kenya), Peter Munya (Kiongozi wa PNU), Jeremiah Kioni (Katibu Mkuu wa Jubilee) na Waziri wa zamani wa Usalama wa Ndani, Dk Fred Matiang’i, ambao wameunda muungano mpya wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Mbali na jitihada za wapinzani kuanzisha umoja wa kumng’oa Ruto madarakani, kiongozi huyo naye ameungana na kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, ikiwamo kuteua mawaziri watano kutoka ODM.

Hatua ya Maranga kujiunga na chama kichanga cha United Green Movement (UGM), inaonyesha kiongozi huyo mwana taaluma wa sheria, anataka kuleta siasa mpya nchini Kenya.

Utetezi wa haki wa Maraga ulianza hata kabla ya kustaafu, ambapo kuna wakati aliwahi kumwandikia barua Rais wa wakati huo, Uhuru Kenyatta akimshauri avunje Bunge kwa sababu “limeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kupitisha sheria” kuhusu kuzingatia usawa wa jinsia katika ugavi wa nafasi za kazi.

Chama cha UGM alichojiunga Maraga, hakina wanasiasa wakongwe kama vilivyo vyama vingine, ni chama ambacho kwa mara ya kwanza kinatazamiwa kusimamisha mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Chama cha UGM, kinachojitambulisha kwa misingi ya haki ya kijamii, ujumuishaji na utunzaji wa mazingira, kimejipambanua kuwa mbadala wa kweli katika ulingo wa siasa za Kenya.

Kwa kumteua Maraga, mwanasheria mashuhuri anayeaminika kwa uadilifu na uthabiti wa kikatiba, chama cha UGM kinaashiria dhamira yake ya kuleta mwelekeo mpya wa uongozi unaozingatia sheria, maadili na masilahi ya wananchi wote.

Maraga ambaye tayari UGM imemteua kuwa mgombea urais 2027, amekanusha madai kwamba, yeye ni mradi wa mtu fulani, akisema hana mpango wa kusikiliza wanaompinga au wanaomtaka ajiondoe katika kinyang’anyiro cha urais.

“Siogopi. Wale wanaonitishia na kunitaka niungane na mirengo yao wajue kuwa ninawania nafasi ya juu kabisa, ili kulinda na kusimamia katiba ya nchi.”

Maraga ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa uongozi wa Ruto, alisema yeye ndiye tiba ya matatizo yanayokumba Wakenya chini ya utawala wa Kenya Kwanza.

Kwa mujibu a Malaga, chama cha UGM kina maadili na misingi inayolingana na falsafa yake ya uongozi unaozingatia katiba badala ya kulazimisha mambo kwa wananchi.

“Tangu nitangaze nia ya kuwania urais, Wakenya wengi wamekuwa wakiniuliza chama changu ni kipi, nami nimekuwa nikiwaambia kuwa bado natafuta. Si kazi rahisi kama wengi wanavyofikiria kupata chama kinacholingana na misingi unayoamini,” alisema Maraga.

Akizungumzia katiba ya chama hicho, amesema inaendana na ndoto yake kama Rais ajaye wa Kenya, ambayo ni kuzingatia utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa wananchi.

Na kwamba iwapo atachaguliwa kuwa Rais, ameahidi kuhakikisha kuwa ushirikishaji wa umma unapewa kipaumbele katika sekta zote ili kukuza uwazi na uwajibikaji.

“Jopo la waanzilishi, kama chuo cha uchaguzi cha chama, limenichagua mapema kusubiri kuteuliwa baadaye na Mkutano Mkuu wa Kitaifa kama mgombea urais wa chama cha United Green Movement katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.”

“Nitafanya kila niwezalo kukiimarisha chama hiki na kukifanya kuwa miongoni mwa vyama imara zaidi nchini. Chama ambacho kitaibuka mshindi si tu katika urais 2027, bali pia kitashinda viti vingi katika Bunge la Kitaifa na mabunge ya kaunti.”

Septemba mosi 2017, Mahakama ya Juu ya Kenya, ikiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga, ilitoa uamuzi wa kihistoria barani Afrika kwa kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 8, 2017.

Maraga katika uamuzi huo aliongoza jopo la majaji sita ambapo katika uamuzi wao majaji wanne walisema uchaguzi haukuwa halali huku wawili wakipinga.

Uamuzi huo wa kipekee ulitokana na dosari na ukiukaji wa taratibu za kikatiba na kisheria katika mchakato wa uchaguzi.

Hatua hii ilidhihirisha kwa mara ya kwanza kwamba mahakama za Kenya zinaweza kuwa huru, jasiri na zenye kuzingatia utawala wa sheria, hata mbele ya mamlaka ya juu kisiasa.

Uamuzi huo uliipa mahakama ya Kenya heshima ya kimataifa na kuwa mfano wa kuigwa katika bara zima la Afrika kuhusu nguvu na nafasi ya mahakama katika kulinda demokrasia.

Mahakama ilitoa uamuzi huo baada ya muungano wa upinzani (Nasa), ulioongozwa na Raila Odinga, kuwasilisha kesi kupinga matokeo yaliyompa ushindi rais wa wakati huo, Uhuru Kenyatta.

Katika uamuzi wake, Mahakama ilibaini kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haikufuata masharti ya katiba na sheria za uchaguzi, hasa katika kujumlisha na kuwasilisha matokeo ya urais.

Pia, ilibaini mfumo wa kielektroniki wa IEBC haukuonyesha uwazi wa kutosha, na kutokuwepo kwa uthibitisho wa fomu halali kutoka vituo vya kupigia kura (fomu 34A na 34B).

Mahakama pia ilibaini uchaguzi haukuwa huru na wa haki, jambo ambalo ni msingi muhimu wa uchaguzi wa kidemokrasia, kama ulivyobainishwa kwenye Katiba ya Kenya (2010).

Mahakama ‘yaambukiza’ Malawi

Hatua kama ya Kenya, pia ilifikiwa Februari 3, 2020 na Mahakama ya Katiba ya Malawi kwa kutoa uamuzi wa pili wa kihistoria kwa kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais wa Mei 2019, ambao ulimtangaza rais wa wakati huo, Peter Mutharika, kuwa mshindi dhidi ya mpinzani wake Lazarus Chakwera wa Chama cha Malawi Congress Party (MCP).

Mahakama hiyo ilibaini kuwa uchaguzi huo haukufanyika kwa njia ya haki, huru na ya kuaminika, kwa sababu zifuatazo kadhaa.

Ilisema fomu za kujumlisha matokeo zilihaririwa kwa kutumia Tipex (aina ya dawa ya kufuta maandishi), jambo lililozua wasiwasi kuhusu uhalali wa mchakato.

Matokeo mengi hayakuwa na sahihi za maofisa wa uchaguzi, kama inavyotakiwa kisheria.

Vilevile, Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) ilishindwa kueleza wazi jinsi ilivyoshughulikia malalamiko na changamoto zilizojitokeza wakati wa uchaguzi.

Pia mahakama ilisema kuwa mchakato mzima ulikiuka masharti ya katiba yanayohakikisha chaguzi huru, za haki, na zinazowakilisha matakwa ya wananchi.

Kwa kuzingatia hoja hizo, mahakama ilifuta ushindi wa Mutharika na kuamuru uchaguzi mpya wa urais ufanyike ndani ya siku 150.

Mahakama pia iliagiza kufanyike mageuzi ya kisheria na ya kiutendaji katika Tume ya Uchaguzi.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.