Huyu ndiye Dimitar Pantev, kocha mpya Simba

Ndani ya muda mfupi kuanzia sasa, Simba itamtambulisha Dimitar Pantev kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo akirithi mikoba iliyoachwa wazi na Fadlu Davids aliyetimkia Raja Casablanca ya Morocco.

Pantev ana umri wa miaka 49, alizaliwa Juni 26, 1976, jijini Varna huko Bulgaria na ni raia wa nchi hiyo.

Kocha huyo ana leseni ya juu ya ukocha inayotolewa na Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA).


Simba ni timu ya tano kufundishwa na Kocha Pantev barani Afrika ambapo kabla ya hapo amezinoa Victoria United ya Cameroon, FC Johansen ya Sierra Leone na Orapa na Gaborone United za Botswana.

Amecheza soka hadi katika ngazi ya Ligi Kuu ambapo alikuwa akicheza kwenye nafasi ya kiungo.

Akiwa mchezaji amezitumikia timu za Cherno More, FC Suvolovo, Chernomorets Byala,   Kaliakra Kavarna, Chernomorets Balchik, Volov Shumen, Dobrudzha, Vladislav, Shabla na Spartak Varba.

Maisha yake ya ukocha yalianzia katika kikosi cha vijana cha Varna City kisha akawa Kocha Msaidizi wa Al Ahli Hebron kisha akawa Kocha Mkuu katika timu za Flamengo, Victoria United, Johansen, Orapa na baadaye Gaborone United.


Katika miaka hiyo mitano aliyofundisha Afrika, ametwaa mataji mawili ya ligi Kuu katika timu mbili kutoka mataifa mawili tofauti ambayo ni ya Ligi Kuu Cameroon na Ligi Kuu Botswana.

Muda mwingi ameutumia kufundisha mchezo wa Futsal na ametwaa mataji matano ya Ligi Kuu Bulgaria ya mchezo wa Futsal.

Ameondoka Gaborone United akiwa ameitumikia kwa muda wa miezi nane (siku 254) tangu alipojiunga nayo Januari 23 mwaka huu.