Katesh /Liwale. Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuimarisha kilimo cha ngano wilayani Hanang ili kufikia lengo la uzalishaji wa tani milioni moja ifikapo mwaka 2030.
Amesema hilo litafanyika kwa kuyarudisha serikalini mashamba yaliyotolewa kwa wawekezaji lakini wakashindwa kuyaendeleza.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni leo Oktoba 3, 2025 katika uwanja wa Mount Hanang, Katesh amesema haipendezi kuona Tanzania inategemea kiasi kikubwa cha ngano kutoka nje ya nchi.
“Tunafahamu kuna mashamba yalitolewa kwa wawekezaji lakini wameshindwa kuyaendeleza, sasa mkitupa ridhaa tunaenda kupitia mikataba ili mashamba yake tuyarudishe serikalini yatumike kufanya uzalishaji,” amesema na kuongeza:
“Haipendezi kuona tunategemea ngano kutoka nje wakati tuna ardhi na hali ya hewa inayoruhusu kulima zao hilo hapa Hanang, tutayachukua tuangalie jinsi ya kuyagawa yaweze kuzalisha, tujitosheleze kwa ngano na kufikia lengo letu la tani milioni moja.”
Samia aahidi kuongeza maeneo ya malisho Karatu
Mashamba hayo ni yaliyopo Kidgamot, Murjanda na Setchet. Uamuzi huo amesema utakwenda sambamba na kulichukua shamba la Bassotu, wakati Serikali ikisubiri uwekezaji mwingine ili kuruhusu wananchi kulitumia kwa utaratibu utakaowekwa wazi.
“Hapa nataka halmashauri iweke wazi utaratibu wa kupata nafasi katika shamba hili, maana tuna taarifa kuna vijimambo vinafanyika, sasa tunataka kila kitu kiwe wazi,” amesema.
Ameahidi kuendeleza sekta ya kilimo kwa kutoa mbolea na pembejeo za ruzuku kwa wakulima na kujenga bwala la umwagiliaji katika Kijiji cha Isakamwale, kilichopo wilayani Hanang.
Vilevile, amewatoa hofu wakulima wa mbaazi kutokana na changamoto ya kushuka kwa bei ya zao hilo. Amesema Serikali inaendelea kuzungumza na wanunuzi ili isiwe chini ya asilimia 70 ya bei ya mwaka jana.

“Nafahamu kwa sasa mnalia na bei ya mbaazi nikipita kusikiliza wanaopita kununua wana sababu nyingi za kushusha bei. Tunajadiliana na watu wa India ambao tunawazalishia hata kama bei inashuka lakini isiwe chini ya asilimia 70 ya bei ya mwaka uliopita,” amesema.
Kuhusu mifugo ameahidi kuendela kutoa ruzuku ya chanjo na utambuzi wa mifugo ili kukidhi viwango vinavyohitajika kwenye soko la kimataifa la wanyama na mazao ya nyama.
Hatua hiyo amesema inalenga kulifikia soko hilo ambalo Tanzania imelipata lakini kwa muda mrefu ilishindwa kukidhi vigezo kwa sababu ya wanyama kutotambulika na kukosa chanjo.
“Pia tunaendelea kuifanyia ukarabati minada na kuiweka katika viwango ambavyo hata mtu kutoka nje anaweza kuja kununua nyama bila kuwa na wasiwasi,” amesema.
Pia ameahidi ujenzi wa barabara ya Nangwa- Kondoa yenye urefu wa kilomita 79 kwa kiwango cha lami.
Mratibu wa Kanda ya Kaskazini, Frederick Sumaye amemuhakikishia mgombea huyo ushindi wa kishindo katika wilaya hiyo.
“Hanang ni nyumbani kwangu, ninakuhakikishia kura zako hapa hazitakuwa chini ya asilimia 90 kutokana na maendeleo makubwa ambayo yamefanyika,” amesema.
Kwa upande wake, mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi, ameeleza nasaha alizopewa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na hayati Waziri Mkuu mstaafu, Rashidi Kawawa, mwaka 1998 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).

Dk Nchimbi katika mkutano wa kampeni, uliofanyika Uwanja wa Ujenzi, Wilaya ya Liwale, Mkoa wa Lindi amesema: “Mmoja wa waasisi wa chama chetu, Rashid Mfaume Kawawa alitoka hapa. Katika viongozi waliopata kutokea, waliolitumikia Taifa ni Mfaume Kawawa.”
“Nilipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama chetu, kikao cha kwanza kabisa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alisema kama unataka kujifunza uzalendo kwa nchi yako kaa karibu na Mzee Kawawa,” amesema.
Amesema katika kipindi chote alipokuwa mwenyekiti wa UVCCM haukupita mwezi bila kwenda kuongea na Mzee Kawawa, kujifunza uzalendo na utumishi kwa nchi.
Dk Nchimbi amewaomba wananchi wa Liwale kujitokeza kwa wingi Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kumchagua mgombea urais wa chama hicho, Samia, wabunge na madiwani ili waendelee kuwatumikia.