Hii ndiyo mwendokasi tuitakayo, kibarua kichachowasubiri watendaji wapya

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuteua watendaji na bodi mpya za taasisi zinazosimamia na kuendesha mradi wa mabasi yaendayo haraka, wadau wanaeleza kazi iliyo mbele yao, huku wakitaka mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji, ili kufikia matarajio ya wananchi.

Aidha, mabasi yaliyoongezwa kwa muda kuanzia jana katika njia ya Kivukoni-Mbezi, yametajwa kuleta ahueni kwa wasafiri waliokuwa wanakabiliwa na kero kubwa ya usafiri.

Mradi wa BRT ulianzishwa kwa lengo la kuondoa kero ya msongamano wa magari jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, tangu ulipoanza huduma katika awamu ya kwanza ya ujenzi (njia ya Mbezi – Kivukoni), haujawahi kufanya kazi kwa ufanisi wala kufikia malengo yaliyotarajiwa.

Watendaji wa taasisi zinazosimamia mradi huo, wamebadilishwa mara kadhaa na jana, Oktoba 2, 2025, Rais Samia alitengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Athumani Kihamia na yule wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), Waziri Kindamba.

Badala yao, amewateua Said Tunda kuchukua nafasi ya Kihamia na Pius Ng’ingo kwa nafasi ya Kindamba. Vilevile, ameteua wenyeviti wa bodi; David Kafulila (Dart) na Ramadhan Dau (Udart).


Kwa mujibu wa wadau waliozungumza na Mwananchi leo Oktoba 3, 2025, wamesema kuna haja ya kurejea kwenye malengo ya kuanzishwa kwa mradi huo na kutengeneza muundo utakaotoa matokeo yanayotarajiwa.

Profesa Abel Kinyondo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema mabadiliko yaliyofanyika ni uamuzi wenye mrengo chanya kwa sababu ni hatua ya mwanzo ya kufanyia kazi matatizo yaliyopo kwenye mradi huo.

Hata hivyo, amesema si mara ya kwanza mabadiliko kama hayo yanafanyika, akieleza kikubwa ni kwa namna gani mabadiliko hayo yataleta maendeleo endelevu.

Amesema watendaji wapya ni kama wanakwenda kuanza upya kwa kuangalia malengo ya kuanzisha Udart na Dart. “Lengo la kwanza lilikuwa ‘tukianzisha Dart, tutatoa huduma ya usafiri ambayo ni ngazi ya juu kiasi kwamba si tu watu watawahi kutoka sehemu moja kwenda nyingine, lakini hata mwenye gari binafsi atapaki gari lake kwa sababu anaona akilitumia, gharama ni kubwa’,” amesema.

Mbali na hilo, mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude, amesema tatizo kubwa ni muundo wa mradi kwani ulipoanzishwa ulitakiwa upate mwendeshaji mwenye uwezo wa kifedha na uzoefu wa kuuendesha katika mfumo wa ubia kati ya sekta binafsi na Serikali (PPP).

“Sasa, huyo mwendeshaji hakupatikana, badala yake Udart wakajiweka kama waendeshaji. Hapo siasa zikaanza kuchezwa, Udart wakapewa kuwa waendeshaji wa mpito wakati mazingira ya kupata mtaalamu yanaendelea, hapo ndipo mambo yakaanza kubadilika,” amesema.


Mkude amependekeza watendaji wapya wapewe kipimo cha utendaji wao (KPI) ndani ya muda fulani ili kuleta matokeo. Pia, muundo wa uendeshaji wa mradi ubadilishwe ili kuleta tija.

Kwa upande wake, Dk Onesmo Kyauke, yeye amesema mradi wa BRT ulianza vizuri na sasa magari mengi yamekufa kutokana na usimamizi mbovu, hivyo amependekeza mabadiliko katika mifumo ya udhibiti.

Amesema uongozi mpya una kazi ya kuhakikisha magari mapya ya kutosha yanapatikana kwenye mradi huo na kuhakikisha mifumo ya kidijitali inatumika hasa kwenye ukataji wa tiketi kwa abiria.

“Ifike mahala, mtu anapoteuliwa awe anawajibika… kwa nini wasiweke ushindani, kwamba nafasi hii ya mkurugenzi itangazwe, watu waje na uzoefu wao na akikabidhiwa pale apewe target (malengo), akiweza apewe bonasi, asipoweza anafutwa kazi mara moja,” amesema.

Wakati wachumi wakipendekeza hayo, baadhi ya wananchi wamepongeza uamuzi wa Serikali na Kampuni ya Mofat Limited kuanza kutoa huduma katika Barabara ya Morogoro.


Oktoba 2, 2025 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema mapya 60 yanayopaswa kutumika katika mradi wa Mbagala yameongezwa ili kutatua changamoto iliyokuwapo barabara ya Morogoro iliyokuwa imesalia na mabasi 30 pekee.

Mwananchi imeshuhudia abiria wachache vituoni wanaosubiri mabasi, tofauti na ilivyokuwa awali waliposubiri kwa zaidi ya saa moja.

Mfanyabiashara wa samaki, mkazi wa Kimara, Tatu Rajab anasema: “Nilikuwa nikija kuchukua samaki nakaa muda mrefu kituoni, kwa sasa ni muda mfupi tu unakaa kituoni gari linakuja unaondoka, kwetu hii ni neema.”

Joseph Mkopa, mtumiaji wa usafiri huo amesema: “Hakuna purukushani kwa siku ya leo ikilinganishwa na siku zingine ambazo foleni ilikuwa kubwa, abiria tunaingia kwenye usafiri kwa utaratibu jambo ambalo walikuwa wanakosea ni kutuacha tuwe wengi eneo moja.”

Christina Mrosso, mkazi wa Ubungo, amesema kwa hali aliyoiona ya usafiri, anafikiria kuanza kuacha kutumia gari binafsi.

“Naishi Ubungo, shughuli zangu nafanya Kariakoo, ahueni ya usafiri ikiendelea nitaacha gari nyumbani kwani haitakuwa na haja, pia nitapunguza gharama,” amesema.

Anuari Kasmini, amesema kuna haja ya wafanyabiashara kuangalia namna ya kuanzisha maegesho ya magari mwishoni mwa vituo vya mabasi.

Japhet John, mkazi wa Mbezi amezishauri mamlaka zitumie fursa hii kusimamia utaratibu wa kuingia kwenye magari kwa foleni na kuondokana na utamaduni wa ovyo uliozoeleka wa kugombea mabasi.

“Mbona pale Mbezi tumeshazoea kupanga foleni, hata kule Muhimbili watu wanapamba foleni, kwa nini isiwe Kimara, Kariakoo, Ubungo au Feri?” amehoji.