Abiria wa mwendokasi wasilimulia uzoefu mabasi mapya siku ya pili

Dar es Salaam. Siku chache tangu kampuni ya Mofat Limited kuanza kutoa huduma ya mabasi mapya katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), baadhi ya abiria wameanza kuonyesha upendeleo wa aina fulani ya magari huku wafanyabiashara wa samaki wakieleza huduma mpya imekuwa neema kwa shughuli zao za kila siku.

Wafanyabiashara wa samaki kutoka Soko la Feri Kivukoni hadi Kimara wanasema kabla ya ujio wa mabasi mapya, walikuwa wakitumia saa mbili hadi tatu kusubiri usafiri, kitendo ambacho huwafanya samaki wao kuharibika.

Abiria wengine wamesema licha ya kwamba hakuna idadi kubwa ya abiria vituoni na kila wakati basi linapita, abiria wanasubiri mabasi mapya ya Mofat vituoni na kuyaacha mabasi ya zamani yapite.

Abiria hao hukaa vituoni kusubiri mabasi mapya ya Mofat yenye viyoyozi wakiyaacha ya zamani ambayo hupita vituoni abiria wakiyaangalia.


Oktoba 2, 2025, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa baada ya kutembelea mradi huo wa mabasi yaendayo haraka, kituo cha Kimara na Kivukoni alisema mabasi mapya 60 yameongezwa kutatua changamoto iliyokuwepo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, barabara ya Morogoro ilikuwa na mabasi 140 lakini hadi jana Oktoba 2, 2025 ni mabasi 30 pekee ndiyo yalibaki, hivyo mabasi 60 yatakwenda kuongeza nguvu kufikia mabasi 90.

Leo Ijumaa Oktoba 3, 2025, Mwananchi imetembelea vituo mbalimbali vya usafiri huo kujionea hali ilivyo baada ya kuongeza mabasi hayo na kubaini uchache wa abiria vituoni tofauti na siku zingine magari yakionekana vituoni kila baada ya muda mfupi.

Hii ni tofauti na awali ambapo abiria husubiri gari hata zaidi ya saa zima na wakati mwingine wengine huamua kuondoka ndani ya vutuo wakapande usafiri wa daladala au bajaji.

Mfanyabiashara wa samaki na mkazi wa Kimara, Tatu Rajab amesema awali kabla ya ujio wa mabasi hayo, alikuwa akikaa kituoni kwa saa mbili hadi tatu akiwa na samaki.

“Nilikuwa nikija kuchukua samaki nakaa muda mrefu kituoni, kwa sasa ni muda mfupi tu unakaa kituoni gari linakuja unaondoka kwetu hii ni neema,” amesema.


Kauli kama hiyo inatolewa pia na Sakina Rajab ambaye amesema jambo wanaloshukuru Serikali ni wafanyabiashara kutozuiwa kuingia kwenye magari mapya wakiwa na mizigo.

“Hatuna zuio la kuingia na samaki, tunatoka nyumbani kwa wakati na tunarudi kwa wakati kwa siku hizi mbili, Serikali iendelee kuongeza magari hata kwetu wafanyabiashara hii kwetu ni fursa bidhaa zetu hasa samaki hawakai muda mrefu,” amesema.

Kwa upande wake, Joseph Mkopa, mtumiaji wa usafiri huo amesema hakuna kero tena kwenye usafiri huo ikilinganishwa na siku za nyuma.

“Hakuna purukushani kwa siku ya leo ukilinganisha na siku zingine ambazo foleni ni kubwa, abiria tunaingia kwenye usafiri kwa utaratibu, jambo ambalo walikuwa wanakosea ni kutuacha tuwe wengi eneo moja,” amesema.

Joseph Timbuka, mtumiaji wa usafiri huo, amesema pamoja na ujio wa mabasi hayo bado mradi wa mabasi yaendayo haraka una matatizo katika usimamizi.

“Nimetoa maoni yangu kuhusu namna ya kuboresha huu mradi hatupaswi kuiendesha tena sisi wenyewe kwa sababu watu wamepewa na wameshindwa tuwape wawekezaji wa nje, bila kufanya hivyo tutauua mradi huu,” amesema.

Baadhi ya abiria wakizungumzia hilo, Nuru Afidhi, mkazi wa Kimara Korogwe, amesema walau leo hajaamka asubuhi sana kwa kuwa alikuwa na uhakika akifika kituoni atapata usafiri.

“Jamani, walau sasa nalala kwa kuongeza saa moja mbele, lakini huko nyuma ilibidi kuamka mapema zaidi ilimradi tu niwahi kuparangana na mwendokasi,” amesema Nuru.


Christina Mrosso, mkazi wa Ubungo, amesema kwa hali aliyoiona ya usafiri, sasa anafikiria kuanza kuacha kutumia gari lake binafsi na kupanda gari hizo kwani zimeonekana kuwa nyingi kwa sasa.

“Mimi naishi Ubungo na ninafanya shughuli zangu Kariakoo, hali ya ahueni ya usafiri ikiendelea kuwa hivi, nitaacha gari nyumbani sasa kwani haitakuwa na haja na pia nitapunguza gharama.

“Katika kulitekeleza hili nimejipa wiki mbili kwanza kuangalia hali itaendelea kuwa hivi au kabla sijachukua uamuzi,” amesema Christina.

Anuari Kasmini amesema sasa kuna haja ya wafanyabiashara kuangalia namna ya kuanzisha maegesho ya magari mwishoni mwa vituo vya mabasi hayo huku akishauri vile vya mwendokasi navyo visimamiwe kutoa huduma kwa wateja wao badala ya ilivyo sasa wamegeuza kwa kila mtu kuegesha gari lake.

Katika hatua nyingine, abiria waliokuwa vituoni wameonekana wakichagua mabasi ya kupanda huku wengi wakipendelea ya Mofat.

“Hata kama ni wewe jamani yaani unaona kuna gari ina kiyoyozi, mpya, utakimbilia kweli haya yenye joto na yaliyochoka?

“Tumeteseka sana watu wa Kimara ni muda wetu wa kuchagua nini tupande,” amesikika mmoja wa abiria wakati wa kupanda gari.

Arafat Mussa, mkazi wa Magomeni amesema hawezi kupanda gari chakavu kwani anajali usalama wake hivyo yupo tayari kusubiri basi jipya kuliko kupanda la zamani.

“Mvua ikinyesha wananyeshewa, milango haifungi na ameanza kutumia usafiri huo baada ya kusikia yapo mapya,hakuna uhakika wa usafiri unaenda Kariakoo kama unaenda Entebe nchini

Wakati malengo ya Mofat katika mabasi hayo ni kutoa huduma kwa kuwasha viyoyosi mwanzo hadi mwisho wa safari, baadhi ya abiria wameanza kuvunja ustaarabu huo kwa kufungua vioo.

Mwananchi ilishuhudia baadhi ya magari vioo vyake vikiwa vimefunguliwa huku baadhi ya madereva wakitangaza vifungwe.

Ukiacha hilo, pia, baadhi ya mabasi hayo mapya hayaonyeshi gari linapokwenda na hivyo kwa wale wazoefu wa kutumia usafiri huo hutumia njia ya kusimama kwenye eneo ambalo linaelekeza gari linapokwenda.

Kwa wasiojua utaratibu huo baadhi wamejikuta wakishuka kabla ya safari kuanza hasa wanaowahi kuuliza gari linaenda wapi na wengine hushuka katika kituo kingine cha kuunganisha gari la sehemu anapokwenda.