Moshi. Mamia ya waombolezaji leo Ijumaa, Oktoba 3, 2025 wamejitokeza kushiriki mazishi ya mfanyabiashara wa sekta ya utalii, Azizi Yasin Msuya (39), aliyedaiwa kujiua kwa kujinyonga nyumbani kwake Sambarai, Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Msuya alikutwa amefariki dunia Alhamisi, Oktoba 2, 2025 majira ya saa mbili asubuhi nyumbani kwake katika Kata ya Kindi, Tarafa ya Kibosho.
Mwili wake uligundulika ukiwa umening’inia kwa kamba ya katani iliyokuwa imefungwa juu ya kenchi.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, marehemu alikuwa akijihusisha na biashara ya kusafirisha wageni (tours) katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Simon Maigwa, amesema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa marehemu alijinyonga kutokana na msongo wa mawazo uliosababishwa na madeni ya benki na watu binafsi aliyokuwa akikabiliana nayo kwa muda mrefu.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alijinyonga kutokana na msongo wa mawazo uliotokana na madeni ya benki na watu binafsi,” alisema Kamanda Maigwa na kuongeza kuwa mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa uchunguzi na taratibu za mazishi.
Katika mazishi hayo, Sheikh wa Kata ya Mfumini kutoka Mahakama ya Kadhi Kilimanjaro, Bashiru Bakari Maharo, ametoa wito kwa wote waliokuwa wanamdai na waliokuwa wanadaiwa na marehemu kuonana na familia ili kuweka mambo sawa.
“Tunaomba wale wanaomdai ndugu yetu wajitokeze. Familia ipo hapa, baba yake ndiye anayebeba dhima ya kulipa madeni. Kifo chake hakijaondoa madeni, mje muone familia ili muweke utaratibu wa kulipa,” amesema Sheikh Maharo.
Kwa upande wake, Imamu wa Msikiti wa Pasua, Swalehe Mbwana, amesema marehemu alikuwa akijitolea kusaidia jamii, ikiwemo kulipia huduma za maji na umeme katika madrasa pamoja na kuchangia vifaa vya ujenzi.
Juma Raibu, mgombea udiwani wa Kata ya Bomambuzi, amesema marehemu alikuwa kijana mstaarabu na mpenda kusaidia.
“Nitoe rai kwa vijana wenzangu, tusichukue sheria mkononi hata pale tunapokumbwa na changamoto. Ni bora tukashirikisha wazee, viongozi wa dini au hata polisi ili tupate msaada kuliko kuchukua hatua ya kujiua,” amesema.
Naye Onest Massawe, daktari bingwa wa mifupa katika Hospitali ya KCMC na jirani wa marehemu, amesema Msuya alikuwa mstari wa mbele kushirikiana na wenzake katika shughuli za kijamii, ikiwemo kuboresha miundombinu ya mtaa.
“Marehemu ni jirani yetu mtaa kwa kweli marehemu tumeshirikiana naye kwenye vitu vingi ikiwemo utengenezaji wa miundombinu ya mtaa wetu na vitu vingine ameshirikiana nasi kwenye kila hali ya furaha huzuni alikuwa mstari wa mbele sana,” amesema Massawe.
Wadau wa sekta ya utalii wamesema kifo cha Msuya ni pengo kubwa kwa biashara hiyo. Mmiliki wa kampuni ya Golden Climb, Said Mwinyi, amesema marehemu alikuwa mshirika wa karibu katika kuandaa safari za watalii na alijulikana kwa uadilifu wake.
“Hili ni pigo kwetu. Tulimjua kama kijana mwenye bidii na ubunifu. Tunawaomba vijana wenzake kutokata tamaa bali kuendelea kujituma licha ya changamoto za kimaisha,” amesema Mwinyi.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Sambarai, Didas Alphonce Mwacha, amesema familia ya marehemu imekuwa mfano wa mshikamano katika eneo hilo na jamii inapaswa kushirikiana kuiunga mkono.
“Tunawaomba wakazi wenzetu tusimame na familia hii. Tumepoteza kijana wetu ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya mtaa,” amesema Mwacha.