Morogoro. Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) kwa kushirikiana na asasi ya kiraia ya Utawala Bora (Wajibu) kimetia saini makubaliano ya kufanya utafiti wa kina kutathimini vyanzo vya ucheleweshaji wa utekelezaji miradi ya ubia nchini.
Utiaji saini umefanyika leo Ijumaa Oktoba 3, 2025 mjini Morogoro, ukiwashirikisha Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila na Mkurugenzi wa Wajibu, Ludovick Utouh.
Kafulila amesema utafiti huo umelenga kubaini kinachosababisha ucheleweshaji wa miradi ya ubia ili kutoa suluhisho la vitendo kutekeleza miradi kwa ufanisi, uwazi na manufaa kwa umma.
Amesema mambo muhimu yatakayotazamwa kwenye utafiti huo ni uchambuzi wa sera, sheria, kanuni na miundombinu ya kitaasisi iliyopo kwa sasa, pamoja na kutoa mapendekezo ya kisera na kimkakati yenye kuzingatia uhalisia wa mazingira ya Kitanzania yatakayowezesha utekelezaji wa miradi ya ubia kwa wakati, tija na kuzingatia uwajibikaji wa matumizi ya rasilimali za umma.
“Kupitia utafiti huu, tunalenga kufichua mizizi ya changamoto hizi na kuweka bayana hatua mahususi za kurekebisha hali hiyo ya ucheleweshaji wa miradi ya ubia,” amesema na kuongeza:
“Tunaamini matokeo ya utafiti huu yatatoa mwanga mpya wa maboresho ya kisera na kitaasisi ili kuongeza tija, uwazi na uwajibikaji katika miradi ya ubia.”
Kwa upande wake Utouh amesema: “Malengo yetu ni kushirikiana na Serikali na kuishauri ili utendaji wake uwe bora, hasa linapokuja suala la makusanyo na matumizi ya fedha za umma.”
Miradi ya ubia ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha uboreshaji wa huduma kwa wananchi kupitia ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma, huku ripoti ya mwisho ya utafiti huo ikitarajia kukamilika ndani ya miezi mitatu.