Wadau wa maendeleo kujenga shule ya Sh1 bilioni Lindi

Lindi. Changamoto ya kusoma katika madarasa chakavu itakwenda kumalizika baada ya wadau wa maendeleo kutoa fedha zaidi ya Sh1 bilioni ili kuweza kujengwa kwa shule ya kisasa katika eneo la Likong’o, Manispaa ya Lindi.

Akizungumza mara baada ya kutembelea majengo ya shule hiyo leo Ijumaa Oktoba 3, 2025, Mhandisi Burhan Omary amesema mradi huo wa Shule ya Msingi Likong’o utagharimu zaidi ya Sh1 bilioni ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 53 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 27, 2025.

Mhandisi Omary ameendelea kusema kuwa ujenzi wa shule hiyo utakuwa na madarasa tisa na madarasa mawili ya shule ya awali nyumba za walimu jengo la utawala pamoja na kuwekewa samani katika madarasa pamoja ofisi za walimu.

“Mradi huu ukimalizika utagharimu zaidi ya Sh1 bilioni na hadi sasa tumeajiri wafanyakazi wazawa 107 na ujenzi wa shule hii ukikamilika utakuwa umemaliza changamoto ya elimu katika eneo hili kwani walimu watakuwa wanaishi hapa hapa shuleni kuliko ilivyo sasa walimu wanatoka mbali kuja kufundisha hapa,” amesema Mhandisi Omary.

Ofisa maendeleo mwandamizi kutoka TPDC, Ally Mluge amesema lengo la ujenzi wa shule hiyo  ni kutoa ushirikiano  kwa serikali na kurudisha kwa jamii kama kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo shule.

“Tumekuwa na kawaida ya kurudisha kwa jamii katika kuboresha miundombinu mbalimbali kama shule na kutoa ushirikiano kwa serikali katika kuleta maendeleo,” amesema Mluge.

Kaimu Mwenyekiti Renatus Nyandaakiongozana na kamati ya CSR kutoka TPDC, amesema ujenzi wa mradi wa shule ni wa mfano kwani utachochea ukuaji wa elimu katika eneo la Likong’o na amewahakikishia wananchi kuwa ifikapo 2026 wanafunzi wa awali wataanza kusoma katika shule hiyo.

“Niwahakikishie wananchi wa Likong’o kuwa ifikapo 2026 watoto wenu wataanza kusoma katika shule hii mpya, na pia niwapongeze sana wasimamizi wa mradi, tumelidhishwa na maendeleo ya mradi huu,” amesema Nyanda.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Likong’o, Shafii Said ameishukuru TPDC kwa kuwajengea shule ya kisasa na amesema shule hiyo ikimalizika itaondoa changamoto ya madarasa na kuinua ubora wa elimu.

“Shule hii ya Likong’o ina wanafunzi 275, ujio wa shule hii mpya itasaidia kuongeza wanafunzi na walimu wataweza kujituma ipasavyo kwani hawatakuwa wanaishi hapahapa shuleni, niwahakikishie viongozi, hata ubora wa elimu utazidi kupanda,” amesema Said.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva amewashukuru TPDC kwa kuboresha mazingira ya elimu pamoja na kuinua hadhi ya shule.

“Tunawashukuru sana TPDC kwa kurudisha kwa jamii na kutuboresha mazingira ya shule yetu, imani yangu kwenu mradi utakamilika kwa wakati na ifikapo mwaka 2026 wanafunzi wa darasa la awali wataanza kuyatumia madarasa yao,” amesema Mwanziva.