Mbeya. Mgombea ubunge Uyole Dk Tulia Ackson amesema atashughulikia kero ya ukosefu wa mikopo asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya wanawake ,vijana na watu wenye ulemavu.
Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 3,2025 wakati akiomba kura na kueleza utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2025, 2030 kwa wananchi wa Kata ya Mwakibete Mtaa wa Gerejini eneo la Soweto.
“Nimesikia kilio chenu kuna vikundi waliomba mikopo wakapata, lakini wapo wengine wamefuatilia hawajapata naahidi hilo limekwisha nitafuatilia cha msingi Oktoba 29, mwaka huu mkipigie kura Chama cha Mapinduzi (CCM),ili kuweza kutatua cha changamoto zenu,” amesema.
Katika hatua nyingine amesema atazungumza na uongozi wa Jiji la Mbeya kuona uwezekano wa kutoa mikopo kwa kundi la vijana watengeneza vyombo vya moto sambamba na kuwatengea eneo rasmi na kuendesha shughuli zao.
Dk Tulia amesema Serikali inaendelea kutatua changamoto za makundi ya vijana na kutenge fedha kwa ajili ya kutoa mikopo katika makundi hayo na kwamba hivi karibuni halmashauri imetoa zaidi ya Sh3.2 bilioni.
“Licha ya halmashauri kutenga fedha za mikopo kila mwaka, lakini ndani ya siku 100 za mgombea Urais Samia Suluhu Hassan atamwaga mabilioni ya fedha kuwezesha makundi hayo, jambo lenu ni moja tu Oktoba 29,mwaka huu ni kutiki, “amesema.
Wakati huo huo amehamasisha wananchi kutumia haki ya kikatiba kujitokeza kupiga kura za kishindo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Dk Tulia na Diwani Kata ya Mwakibete Lucas Mwampiki,” amesema.
Amesema namna pekee ya kutatuliwa changamoto zenu ni kukipigia kura Chama cha Mapinduzi (CCM ) ili kusogezewa maendeleo kwa wakati.
Diwani Kata ya Mwakibete, Lucas Mwampiki amemuomba Dk Tulia kuboreshewa miundombinu ya elimu, barabara ili kusaidia jamii kunufaika na miradi ya Serikali ya awamu ya sita.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Mkoa wa Mbeya, Edna Mwaigomole amemtaja Dk Tulia ni dawa ya wananchi wa Mbeya na Uyole hivyo ni jukumu la kila mmoja kupiga kura za kishindo Oktoba 29, 2025.
“Tunataka kura nyingi za heshima kwa Dk Tulia na Samia ili tuweze kuletewa maendeleo makubwa katika majimbo ya Mbeya mjini na Uyole,” amesema.
Mjasiriamali wa mbogamboga Soko la Soweto, Siwema Haule amesema changamoto kubwa ni ukosefu wa mitaji na soko la kisasa na kumuomba mgombea akipata ridhaa kuanza na changamoto hizo.