Zitto aahidi ajira kwa wananchi Tanga wakimchagua…

Tanga. Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto  Kabwe amewaomba wakazi wa Jiji la Tanga kumchagua mgombea ubunge wao Seif Abal Hassan ili wakarudishe heshima ya Tanga ya viwanda, ambavyo vitasaidia ongezeko la ajira.

Akizungumza  katika mkitano wa hadhara uliofanyika barabara ya 20 kata ya Ngamiani Kusini leo Ijumaa Oktoba 3, 2025 Zitto amesema mgombea wao ni mtaalam wa masuala ya biashara na anajua jinsi ya kunyanyua uchumi wa wananchi, na amempa mafunzo na kuelewa jinsi ya kupambania maendeleo.

Amesema Mkoa wa Tanga ndio eneo pekee ambalo kulikuwa na viwanda vingi ila kwa sasa vingi havifanyi kazi, hivyo wananchi wakimpa ridhaa mgombea wao atakwenda kusimamia masuala ya viwanda na shughuli nyingine ili wananchi hasa vijana waweze kupata ajira.

Jambo lingine ambalo wanakwenda kusimamia ni bomba la mafuta kwamba mradi huo uwe na faida kwa wananchi kwamba ACT-Wazalendo wakipewa kuongoza Serikali kwa kuchagua mbunhe na diwani wa Tanga, watakwenda kufuta kodi ambazo zinanyonya masrahi ya wananchi na waweze kupata maendeleo.

Ameongeza kuwa watatunga kanuni ambazo zitaweza kusaidia kampuni za mafuta zilizowekeza Tanga, wanakaa pamoja na kuangalia wanawezeshaje wananchi kupata maendeleo ikiwemo kufuta fedha ambazo wanashikwa wananchi kutoa marehemu wao hospitali.

“Tutabuni sera za kiuchumi ambazo zitazalisha ajira nyingi ili kuondokana na changamoto kubwa ya ajira kwa vijana wa Tanga, tutahakikisha tunaweka mazingira mazuri ili viwanda viweze kuwa vya kutosha  na watu wa Tanga waweze kupata ajira kama ilivyokuwa miaka ya 60 ambayo Tanga ilikuwa juu kiuchumi,” amesema Zitto.

Ameongeza kuwa kupitia mgombea ubunge wao watahakikisha wanaifanya Tanga kuwa kitovu cha biashara, kwa kuongeza utumiwaji wa bandari ya Tanga ambapo watahamasisha kuwepo mikakati ya nchi zote za Afrika Mashariki kutumia bandari hiyo.

Aidha, mgombea ubunge wa Tanga, Seif AbalHassan ameahidi kwenda kurudisha heshima ya Tanga kwa kusimamia vijana kupata ajira kupitia bandari na bomba la mafuta kwamba miradi hiyo iwe na faida kwa wananchi na sio watu wa kuja.

Kwamba atahakikisha wanawake wa Tanga wanapata mikopo ambayo itakuwa na faida  kwao na kuondokana na ile ya kausha damu ambayo imewafanya wakimbie hadi nyumba zao kwa kuogopa madeni jambo ambalo sio sahihi.

Amesema licha ya kutumia vitega uchumi hivyo pia atainua uchumi wa wananchi kupitia michezo, kwa kuanzisha mashindano ambayo vijana wataweza kupata ajira kupitia michezo kama ilivyo maeneo mengine kwani tayari zipo timu kubwa.

Katika kushiriki uchaguzi Mkuu chama cha ACT-Wazalendo kimesimamisha mgombea ubunge jijini Tanga pamoja na madiwani katika zote 27 wakiwemo wanawake.