Kamati ya Utendaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Oktoba 2, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi na kufanya uamuzi kwa mujibu wa kanuni.
Katika kikao hicho, adhabu mbalimbali na onyo zimetolewa kutokana na matukio yaliyofanyika kinyume na kanuni za uendeshaji wa ligi hiyo.
Katika taarifa hiyo, kamati imetoa maamuzi kama ifuatavyo
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Oktoba 2, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;
MECHI NAMBA 001: KMC FC 1-0 DODOMA JIJI
Klabu ya KMC imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la ubao wa kuonesha matokeo kwenye uwanja wake wa nyumbani, KMC Complex kutofanya kazi kama ilivyoelekezwa kwenye Kanuni ya Leseni za Klabu.
Hii ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 9:3 ya Ligi Kuu kuhusu Uwanja na 47:33 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40:5 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti Kimashindano.
Klabu ya Dodoma Jiji imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kuanza msimu wa Ligi Kuu na kucheza mchezo wa Ligi bila kuwa na kocha mwenye ujuzi kwa mujibu wa Kanuni ya 77:3(1, 2, 3).
Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:19 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
MECHI NAMBA 009: TRA UNITED SC 2-2 DODOMA JIJI FC
Klabu ya Dodoma Jiji imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kuanza msimu wa Ligi Kuu na kucheza mchezo wa Ligi bila kuwa na kocha mwenye ujuzi kwa mujibu wa Kanuni ya 77:3(1, 2, 3).
Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:19 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
MECHI NAMBA 011: NAMUNGO FC 1-0 TANZANIA PRISONS FC
Klabu ya Tanzania Prisons imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la mashabiki wake kufanya vurugu na kuingia kwenye uwanja wa Kasim Majaliwa bila kufuata utaratibu wakati wa mchezo tajwa hapo juu.
Siku ya tukio hilo, mashabiki wanaokadiriwa kufika 250 waliokuwa wamevalia jezi za klabu ya Tanzania Prisons walifika uwanjani hapo na kujitambulisha kuwa wao ni askari wa jeshi la Magereza hivyo hawawezi kulipa kiingilio ili kuingia uwanjani kushuhudia mchezo huo.
Kwasababu jambo hilo ni kinyume na taratibu za mchezo wa soka na kanuni za Ligi, maofisa wa mchezo huo wakiwemo kutoka N-CARD (mtoa huduma za uuzaji na uthibitishaji tiketi), waliwazuia mashabiki hao na kuwaelekeza kuwa wanapaswa kununua tiketi.
Hata hivyo, mashabiki hao hawakukubaliana na maelekezo hayo ndipo walipoamua kusukuma geti na kuingia uwanjani kwa nguvu.
Tukio hilo lisilo la kiuanamichezo lilisababisha athari hasi kadhaa ikiwemo mashabiki wengi waliokuwa eneo hilo kutumia mwaya huo kuingia uwanjani bila kulipa kiingilio, upotevu wa pesa taslimu Sh. 500,000 (laki tano) zilizokuwa zimehifadhiwa na afisa wa N-CARD, uharibifu wa mashine ya N-CARD ya kuuzia na kukagulia tiketi pamoja na majeraha kwa afisa wa N-Card, msimamizi wa kituo cha Lindi na kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu ya Namungo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Aidha, klabu ya Tanzania Prisons itatakiwa kulipa fedha zilizopotea, gharama za mali zilizoharibika pamoja na gharama za matibabu ya waathirika wa vurugu hizo kama ilivyoelekezwa kwenye Kanuni ya 47:3 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
MECHI NAMBA 013: KMC FC 0-1 SINGIDA BS FC
Klabu ya KMC imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la ubao wa kuonesha matokeo kwenye uwanja wake wa nyumbani, KMC Complex kutofanya kazi kama ilivyoelekezwa kwenye Kanuni ya Leseni za Klabu.
Hii ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 9:3 ya Ligi Kuu kuhusu Uwanja na 47:33 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40:5 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti Kimashindano.
MECHI NAMBA 014: YOUNG AFRICANS SC 3-0 PAMBA JIJI FC
Klabu ya Pamba Jiji imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kuchapisha picha jongeo (video) kwenye ukurasa rasmi wa klabu hiyo katika mtandao wa Instagram, ikiwaonesha wachezaji wa klabu hiyo wakifanya mazoezi gizani ndani ya uwanja wa Benjamin Mkapa Septemba 23, 2025, jambo ambalo lilizua taharuki na kuchafua taswira ya Ligi huku ikikosekana sababu ya msingi ya wao kufanya hivyo.
Timu ya Pamba ambayo ilikuwa na mchezo tajwa hapo juu dhidi ya Young Africans, ikiwa haijatoa taarifa yoyote kwa klabu mwenyeji, mamlaka za uwanja wala maofisa wa mchezo, ilifika uwanjani hapo saa 12:35 jioni kwa ajili kutumia haki ya kikanuni ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi katika muda wa mchezo (ambao ulipangwa kuanza saa 1:00 usiku).
Baada ya kufika uwanjani (ambapo taa zilikuwa hazijawashwa), viongozi wa ufundi wa timu hiyo waliendelea na programu yao kwa kuanza kuwafanyisha mazoezi wachezaji
gizani huku wakisikika wakitoa kauli chafu na za kejeli kwa mamlaka za soka kuwa zinawahujumu, wakisahau kuwa hata muda wa kuanza mazoezi ulioainishwa kikanuni (muda wa kuanza mchezo) ulikuwa haujafika na kwamba wahudumu wa uwanja huo walikuwa wanaendelea na taratibu za kuwasha jenereta na taa za uwanjani.
Wachezaji hao waliendelea na mazoezi yao lakini mara baada ya taa kuwaka kikamilifu na uwanja kuwa na mwanga wa kutosha majira ya saa 1:08 usiku, makocha waliwaamuru wachezaji wao kuondoka uwanjani na walipoulizwa na maofisa wa mchezo kwanini wanaondoka baada ya taa kuwashwa, walisema tayari wamekamilisha programu yao.
Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inazikumbusha klabu zote kuhakikisha zinafuata muongozo wake kwa kutoa taarifa mapema kuhusu ratiba zao za mazoezi ili maandalizi ya mazingira na miundombinu yafanyike kwa wakati kwa lengo la kukidhi mahitaji ya kikanuni.
Mkurugenzi wa Mashindano, Ibrahim Mohamed na walinzi wa uwanjani (stewards) wa klabu ya Young Africans, Soudy Hussein na Shamte Mkumba wamefungiwa kwa kipindi cha miezi mitatu (3) kila mmoja kwa kosa la kufanya kitendo ambacho ni kinyume na maadili ya uongozi wa mpira wa miguu, kwa kuwazuia maofisa wa mchezo tajwa hapo juu kutekeleza majukumu yao ya kiusalama wakati wa mchezo huo.
Maofisa hao wa Young Africans walipinga na kuwazuia maofisa wa mchezo huo kutumia walinzi wa uwanjani (stewards) walio chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kwenye eneo la kuchezea (pitch), wakitaka watumike walinzi wengine jambo ambalo ni kinyume na masharti yaliyoainishwa kwenye Sura ya pili (2) Kanuni za Ulinzi na Usalama za Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).
Pamoja na zuio hilo, Soudy Hussein na Shamte Mkumba walitoa kauli za vitisho kwamba watampiga mlinzi yeyote mwingine atakayesogea eneo la kuzunguka kiwanja (pitch) tofauti na wale walioletwa na klabu ya Yanga.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni 46:5 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.
MECHI NAMBA 018: DODOMA JIJI FC 2-0 COASTAL UNION FC
Klabu ya Dodoma Jiji imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kuanza msimu wa Ligi Kuu na kucheza mchezo wa Ligi bila kuwa na kocha mwenye ujuzi kwa mujibu wa Kanuni ya 77:3(1, 2, 3).
Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:19 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mwamuzi wa kati, Jackson Samwel kutoka Arusha na mwamuzi msaidizi namba 2 wa mchezo tajwa hapo juu wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira.
MECHI NAMBA 021: SINGIDA BS FC 1-0 MASHUJAA FC
Klabu ya Singida BS imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye uwanja wa KMC Complex kuelekea mchezo tajwa hapo juu Septemba 30, 2025.
Singida waliwasili uwanjani hapo saa 6:38 mchana badala ya saa 6:30 mchana kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Klabu ya Singida BS imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la ubao wa kuonesha matokeo kwenye uwanja wake wa nyumbani, KMC Complex kutofanya kazi kama ilivyoelekezwa kwenye Kanuni ya Leseni za Klabu.
Hii ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 9:3 ya Ligi Kuu kuhusu Uwanja na 47:33 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40:5 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti Kimashindano.
MECHI NAMBA 022: MBEYA CITY FC 0-0 YOUNG AFRICANS SC
Mchezaji wa klabu ya Young Africans, Ibrahim Abdullah amefungiwa michezo mitano (5) kwa kosa la kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa klabu ya Mbeya City, Ibrahim Ame, rafu ambayo ilionekana kuwa mbaya zaidi na ingeweza kuhatarisha usalama wa mchezaji huyo.
Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Omary Mdoe kutoka Tanga ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira.
Pamoja na matukio mengine, Omary Mdoe alishindwa kutafsiri sheria katika dakika ya 46 ambapo mchezaji wa Mbeya City, Matheo Anthony alishika mpira ndani ya eneo la penati lakini hakuchukua hatua yoyote. Mwamuzi huyo pia alishindwa kuchukua hatua baada ya mchezaji Ibrahim Abdullah kucheza rafu mbaya katika dakika ya tatu ya mchezo.
MECHI NAMBA 023: JKT TANZANIA FC 1-1 AZAM FC
Mchezaji wa klabu ya JKT Tanzania, Mohamed Bakari amefungiwa michezo mitano (5) kwa kosa la kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa klabu ya Azam FC, Lusajo Mwaikenda, rafu ambayo ilionekana kuwa mbaya na ingeweza kuhatarisha usalama wa mchezaji huyo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mwamuzi wa kati, Jackson Samwel kutoka Arusha na mwamuzi msaidizi namba 2 wa mchezo tajwa hapo juu wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira.