Jumla ya watoto 15,000 wenye mdomo sungura wafanyiwa upasuaji

Dodoma. Jumla ya watoto 15,000 waliozaliwa na matatizo ya mdomo wazi (mdomo sungura) nchini wamepatiwa matibabu ya kurekebisha midomo yao kwa kipindi cha miaka 19 tangu huduma hiyo ianze kutolewa bure nchini.

‎Aidha, katika kipindi hicho, takribani watoto milioni mbili duniani kote wamefanyiwa upasuaji wa kurekebisha midomo yao na kurudisha tena tabasamu lao walilolikosa kwa muda mrefu.

‎Akizungumza kwenye maadhimisho ya kimataifa ya siku ya kutabasamu duniani yaliyofanyika leo Oktoba 3, 2025 kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, daktari bingwa wa upasuji wa hospitali hiyo, Dk Athanas Masele amesema kuanzia mwaka 2023 hadi sasa hospitali hiyo imewafanyia upasuaji wa kuwarekebisha midomo takribani watoto 149 kwa ufanisi mkubwa.

‎Dk Masele amesema matibabu ya mdomo wazi yalianza kutolewa hospitalini hapo tangu mwaka 2015 kwa njia ya msahama kwa wagonjwa au kuchangia gharama kidogo lakini ilipofika mwaka 2023 yalianza kutolewa bure baada ya Taasisi ya kimataifa ya Smile Training International kuanza kugharamia matibabu hayo.

‎Amesema kuanzia wakati huo matibabu hayo yamekuwa yakitolewa bure kwa watoto wote wanaozaliwa na mdomo wazi na idadi kubwa ya wazazi wamekuwa wakijitokeza kupata matibabu hayo kwa watoto wao na hata watu wazima waliochelewa kupata matibabu wakati wa utoto nao wamejitokeza na kufanyiwa marekebisho.

“Watu wengi walikuwa wanaamini kuzaliwa na mdomo wazi ni laana au inatokana na imani za kishirikina na uchawi lakini dhana hiyo kwa sasa imepotea na watu wanajitokeza kupata matibabu yanayowarejeshea upya tabasamu lao lililopotea kwa miaka mingi,” amesema Dk Masele.

‎Amesema changamoto ya watoto kuzaliwa midomo wazi ipo ya aina mbili aina ya kwanza ni ile ya mdomo wa juu kuwa wazi ambao unasababisha mtoto kushindwa kula na kuongea na aina ya pili ni ya mdomo wazi wa ndani ambao siyo rahisi kugundulika mapema lakini athari zinajitokeza kwa mtoto kushindwa kuongea vizuri.

‎Amesema matatizo yote mawili yanatibika kwa kufanyiwa upasuaji ambapo uwazi wa mdomo wa nje unafanyika mtoto akifikisha miezi mitatu na uwazi wa ndani unafanyika akifikisha miezi tisa tangu kuzaliwa.

“Uwazi wa nje ni rahisi kushoneka lakini uwazi wa ndani una changamoto kidogo kutokana na mdomo wa mtoto kuwa mdogo hivyo vifaa vya kufanyia upasuaji haviwezi kutumika na ndiyo maana inashauriwa wafanyiwe upasuaji wakifikisha miezi tisa,” amesema Dk Masele.

‎Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Shirika la Smile Training International, Veronica Kamwela amesema shirika hilo linaratibu matibabu ya mdomo wazi ambapo kwa kipindi cha miaka 19 ya shirika hilo jumla ya watoto milioni 2 duniani kote na watoto 15,000 nchini, wamefanyiwa upasuaji wa kuwarekebisha midomo yao.

‎Amesema watoto wanaozaliwa na tatizo hilo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo unyanyapaa hali inayowasababisha wazazi na walezi kuwaficha watoto hao kwa kudhani kuwa wamelaaniwa au wamelogwa.

‎Amesema pamoja na kugharamia upasuaji lakini shirika hilo linatoa huduma ya ushauri wa kisaikolojia kwa watoto na wazazi wenye midomo wazi na kuwapatia mafunzo ya kutamka maneno vizuri baada ya upasuaji kwani tatizo hilo husababisha watoto kushindwa kutamka maneno vizuri.

‎Mbali na hilo pia wamekuwa wakitoa vifaa wasaidizi kwa watoto wenye matatizo ya kusikia na huduma za matibabu ya koo, pua na masikio ambapo matibabu yote hayo hutolewa bure.

‎Kwa upande wake, mkurugenzi msaidizi wa huduma za kinywa na meno kutoka Wizara ya Afya, Dk Baraka Nzobo amesema tatizo la mdomo wazi linatibika na halisababishwi na imani za kishirikina.

‎Amesema watoto wanaozaliwa na tatizo hilo wanaweza kutibiwa na kurejea kwenye hali yao ya kawaida na kutimiza malengo yao kama walivyo watoto wengine.

‎Aidha, ameishukuru Serikali kwa kuruhusu shirika hilo kufanya kazi nchini kwani gharama za matibabu za upasuaji kwa watoto hao ni Sh1.2 milioni kwa kila mtoto lakini gharama hizo zinatolewa bure.

‎Akizungumza kwa niaba ya wazazi wa watoto waliofanyiwa upasuaji kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Kauye Said ameishukuru Serikali kwa kugharamia matibabu ya watoto wao kwani hata wangeambiwa wachangie nusu ya gharama ya matibabu wasingeweza.

‎Amesema lakini kwa sasa wazazi na watoto wao wana furaha baada ya upasuaji uliorudisha tabasamu lao baada ya kukata tamaa.