CEO KMC ang’oka, mrithi wake aanza kusakwa

MABOSI wa KMC wako katika mchakato wa kutafuta ofisa mtendaji mkuu mpya (CEO), baada ya Daniel Mwakasungula, aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo kumaliza mkataba, huku kukiwa hakuna mazungumzo mapya ya kuongeza mwingine kikosini humo.

Licha ya uongozi wa KMC kutoweka wazi juu ya suala hilo, lakini Mwanaspoti linatambua Mwakasungula amemaliza mkataba wake na kikosi hicho, hivyo mchakato wa kutafuta mrithi wake atakayechukua nafasi hiyo unaendelea ndani kwa ndani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwakasungula amesema ni kweli amemaliza mkataba na kikosi hicho, ingawa suala la mazungumzo ya kuongeza mkataba mwingine mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa sasa sio muda sahihi wa kuzungumzia jambo hilo.


“Nipo safarini ndugu yangu ila ukweli ni kwamba nimemaliza mkataba wangu na KMC nikiwa mtendaji mkuu, ishu ya kuendelea nao kwa sasa hilo siwezi kuliweka wazi kwa sababu hakuna makubaliano mapya rasmi tuliyofikiana,” amesema Mwakasungula.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua, Mwakasungula aliyejiunga na kikosi hicho, Agosti 15, 2022, akichukua nafasi ya Walter Harrison aliyeajiriwa na Yanga kama meneja wa timu, hatoongeza mkataba mpya na kwa sasa anaangalia fursa nyingine.

Mkataba wa Mwakasungula na KMC ulifikia ukomo tangu Septemba 29, 2025, ambapo uongozi wa klabu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni unaendelea na mchakato wa kutafuta mrithi wake, wanayeamini ataendeleza mazuri yaliyofanywa na anayeondoka.

KMC inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nane sasa tangu 2018-2019, imeuanza msimu huu kwa matokeo yasiyoridhisha kwani imepoteza mechi mbili na kushinda moja kati ya tatu ikikusanya pointi tatu pekee na kukamata nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi hiyo.