Bado Watatu – 48 | Mwanaspoti

AKAONGEZA: “Yule wa kiume alifia hapa Tanga. Alikuwa amepata mali ambayo ilichukuliwa na rafiki yake kwa vile ndugu yake hakuwa akijulikana. Kwa bahati njema, ndugu yake huyo wa kike alikuja kupata habari kuwa kaka yake amefariki dunia akiwa Tanga na alikuwa na mali.
“Mwanamke huyo, pamoja na mtoto wake aliyemzaa ambaye wakati huo alikuwa amemaliza kidato cha sita, walikuja Tanga. Mwanamke huyo akafanikiwa kuipata nyumba aliyokuwa akiishi kaka yake, lakini alikuta hata yule mtu aliyeachiwa mali na kaka yake naye alikuwa amefariki dunia.
“Wakaelezwa mkasa wa kusikitisha kwamba kaka yake aliacha mtoto ambaye alilelewa na mtu aliyeachiwa mali na kaka yake. Lakini watoto wa huyo mtu wakaja kumuua mwenzao kwa sababu waliambiwa angerithi yeye ile mali kwa sababu ni ya baba yake. Ndiyo wakaona wamuue, lakini wote walikamatwa na kuhukumiwa kunyongwa.
“Yule mwanamke na mwanawe walirudi walikotoka, lakini baadaye mwanawe alikuja Tanga peke yake kuangalia uwezekano wa kuipata mali ya mjomba wake. Akiwa Tanga alikuja kugundua kwamba wale watu wanne walionyongwa walikuwa wameachiwa kinyemela na walikuwa wanaishi uraiani wakiwa wamebadili majina yao.
“Kijana huyo alipata uchungu sana akaamua kuwatafuta. Zile siku alizokuwa amekuja na mama yake, alifanikiwa kuipata laini ya simu aliyokuwa akiitumia yule kijana mwenzake aliyeuawa kwani alikuwa akilala chumbani mwake. Ile laini aliichukua akawa anaitumia yeye.
“Kijana huyo, kwa kutumia mbinu za kigaidi, alifanikiwa kuwanasa wale wote waliomuua ndugu yake na kisha kuachiwa kinyemela na mkuu wa gereza. Na yeye aliwanyonga mmoja baada ya mwingine.
“Ili kuwababaisha polisi, kijana huyo aliwahi kulifukua kaburi la kijana aliyekuwa ameuawa na kuchukua alama ya dole gumba lake, ambapo alikuwa akiweka katika karatasi zenye ujumbe alizokuwa akiweka shingoni mwa watu aliowanyonga.
“Polisi walihangaika sana kumtafuta muuaji bila mafanikio, huku wakiamini kwamba marehemu ndiye aliyekuwa akiwanyonga kutokana na kuwepo kwa alama ya dole gumba lake kwenye zile karatasi na kutokana na kutumia namba ya simu yenye jina la marehemu.
“Mwisho, kijana huyo alimtumia ujumbe kachero aliyekuwa akichunguza mauaji hayo na kumwambia kwamba ameshamaliza kazi na amerudi kaburini, jambo ambalo lilisumbua akili ya kachero huyo.
“Sasa leo utakuwa mwisho wako wa kuhangaika katika uchunguzi huu. Nilikwambia kwenye simu kwamba mimi ni mtu muhimu sana kwako, nikiwa na maana kwamba nilikuwa na umuhimu katika uchunguzi wako kwa sababu nilikuwa ninajua kile ambacho ulikuwa unakitafuta…”
“Ninakukatisha… niambie huyo kijana yuko wapi?”
“Yuko na wewe na unazungumza naye hivi sasa.”
“Una maana kuwa ni wewe?”
“Ndiyo, ni mimi,” akanijibu kijasiri.
Kwa sababu ya kutaharuki kumuona kijana huyo, niliinuka kwenye kiti nikamfuata mahali alipoketi na kumuuliza:
“Una uhakika kwamba kijana uliyenieleza ni wewe mwenyewe?”
“Ndiyo, ni mimi.”
Nikamuuliza tena:
“Wewe ndiye uliyewanyonga wale wafungwa?”
“Ndiyo, niliwanyonga wafungwa wanne waliokuwa wametoroshwa kuepushwa na adhabu ya kifo.”
Nilimtulizia macho kijana huyo kwa sekunde kadhaa nikiwa namtazama.

“Una mashaka kwamba si mimi?” Kijana huyo akaniuliza.

“Una chochote cha kunithibitishia kwamba wewe ni mzima na ni kweli ndiye uliyewanyonga watu wale?”

Kijana huyo alitoa simu yake, akanipigia kisha akaniambia:

“Tazama namba iliyotokeza kwenye simu yako.”

Nikaichukua simu yangu iliyokuwa juu ya meza ambayo ilikuwa inaita. Nikaitazama namba iliyokuwa inapiga na kuona ilikuwa ni ile namba ya Thomas Christopher.
“Sasa nimeamini kuwa ni wewe. Wewe ndiye uliyenitumia ujumbe kwenye simu yangu ukaniambia kuwa umemaliza kazi…?”
“Naam. Ndiye mimi.”
“Nakushukuru sana kwa kujitokeza wewe mwenyewe. Nikwambie ukweli kwamba wewe ni kijana mdogo sana lakini ulisumbua sana akili yangu.”
“Ninajua kuwa nilikusumbua, samahani sana lakini ilibidi niwaue wale watu kwani kitendo walichokifanya hakikuwa na adhabu nyingine zaidi ya kifo.”
Nikarudi kwenye kiti na kuketi.
“Sasa ni kitu gani kilichokufanya ujitokeze licha ya kujua kuwa umeua?”
“Nimejitokeza ili niwaeleze ukweli polisi. Nilikuwa ninajua kwamba polisi walikuwa hawajui kuwa watu waliokuwa wananyongwa walishahukumiwa kunyongwa na mahakama.”
“Baada ya wewe kugundua kuwa wale watu walitoroshwa, kwa nini hukuja polisi kutuarifu?”
“Unajua mawazo ya majaji na mahakimu yako tofauti. Nilishuku jaji mwingine anaweza kuwaachia kwa kuona hawana hatia wakati walikuwa wamemuua ndugu yangu kwa tamaa ya kutaka kupata utajiri usiowahusu. Kama nilivyokueleza, Christopher ni kaka wa mama yangu, kwa hiyo Christopher ni mjomba wangu. Kama ni mjomba wangu angalau ningekuwa na haki ya kumrithi mimi, siyo watu wale. Kitendo chao cha kumuua Thomas kilinitia uchungu, lakini kitendo cha mkuu wa gereza kuwaachia kilinitia uchungu zaidi.”
“Ndiyo sababu ukachukua uamuzi wa kuwaua mwenyewe?”
“Ndiyo.”
“Katika kufanya hivyo ulitegemea nini?”
“Niliategemea kwamba ningekamatwa lakini sikukamatwa, kwa hiyo nikajitokeza mwenyewe.”
Nikamtazama yule kijana huku nikijiuliza mahakama itampa hukumu gani kijana huyu aliyeua kwa uchungu. Nikajiambia kimoyomoyo, kitendo chake cha kuchukua sheria mkononi ni kinyume cha sheria. Kwa vyovyote vile anaweza kukutana na adhabu ya kitanzi kwani ameua kwa kukusudia kuua.
“Ninasikitika kukwambia kwamba nitakukamata ili na wewe tukufikishe mahakamani kwa sababu umetenda kosa lisilosameheka.”
“Hata wale wauaji walitenda kosa lisilosameheka.”
“Basi sheria itafuata mkondo wake.”
“Nilitegemea kwamba ingekuwa hivyo. Kama sheria inafuata mkondo wake kama unavyosema wewe, kina Unyeke nisingewanyonga mimi, wangenyongwa gerezani kama wengine wanavyonyongwa.”
Nilihisi maneno ya kijana huyo yalikuwa na ukweli. Nikamtazama na kumtolea tabasamu la huzuni, kisha nikatikisa kichwa kumsikitikia.
“Ninakusikitikia sana. Hivi mama yako yuko wapi?”
“Yuko Lindi.”
“Anajua kwamba umewaua watu waliomuua Thomas?”
“Hajui. Sikuwahi kumueleza.”
“Kwanini hukumueleza?”
“Kwa sababu nilijua kwamba angenikataza wakati mimi mwenyewe nilishadhamiria kuwaua.”
“Kwa sababu ulijua kuwa ungekamatwa na hata uliponusurika ukaona ujitokeze mwenyewe, mimi kama afisa wa polisi ambaye husimamia sheria, sina kingine zaidi ya kutimiza jukumu langu.”
Nikainua mkono wa simu ya mezani na kumpigia afisa upelelezi.
“Hello… inspekta Fadhil. Habari ya huko?” Sauti ya afisa upelelezi ikasikika mara tu baada ya kupokea simu yangu.
“Habari ni nzuri afande.”
“Ndiyo. Kuna nini zaidi?”
“Nimempata muuaji wa kina Unyeke.”
“Unasema kweli?”
“Ni kitu cha ajabu sana kwa sababu amejitokeza mwenyewe na nipo naye hapa ofisini kwangu.”
“Ni nani?”
“Ni kijana mmoja ambaye alifanikiwa kuifanya polisi imdhanie kuwa ni marehemu Thomas kutokana na mbinu zake alizotumia kuwaua wale watu.”
“Umesema amejitokeza mwenyewe, amekuja kukueleza nini?”
“Kunieleza kwamba yeye ndiye aliyewanyonga kina Unyeke.”
“Kwanini?”
“Amenieleza kisa kirefu. Ameniambia watu hao walimuua Thomas ambaye ni ndugu yake — shangazi kwa mjomba, kisha akaja kugundua kuwa wauaji hao walitoroshwa jela na walikuwa uraiani.”
“Sasa nisubiri, ninakuja hapo ofisini kwako.”
“Ninakusubiri.”
Nikauweka mkono wa simu mahali pake kisha nikamtazama yule kijana ambaye naye alikuwa akinitazama.
“Unaitwa nani?” nikamuuliza.
“Naitwa Faustin Ojuku.”
Nikaandika jina hilo kwenye karatasi iliyokuwa mezani kwangu.
“Una umri gani?”
“Ukifika mwezi wa saba mwaka huu nitatimiza umri wa miaka ishirini na tisa.”
“Una mke?”
“Sijaoa bado.”
“Elimu yako ikoje… ulifika kidato cha ngapi?”
“Kidato cha sita.”
“Tangu umekuja hapa Tanga una muda gani sasa?”
“Mara ya kwanza tulikuja na mama yangu mwaka juzi baada ya kupata taarifa kuwa mjomba wangu amefariki dunia, halafu tulirudi tena Lindi. Lakini baadaye nilikuja tena peke yangu kutafuta maisha huku Tanga. Nilifikia Pongwe na nikabahatika kupata kazi katika kiwanda cha Mchina mmoja mwekezaji kilichopo Pongwe ambako ndiko ninakofanya kazi.”
“Wewe mwenyewe unaishi wapi?”
“Nimepanga chumba hapo hapo Pongwe.”
“Ni lini uligundua kuwa kina Unyeke walitoroshwa jela?”
“Kama miezi sita hivi iliyopita.”
“Hebu nieleze, ulijuaje kama hao watu walitoroshwa jela?”
“Unajua nilikuwa nikieleza kile kisa cha mjomba wangu na jinsi ndugu yangu Thomas alivyouawa kwa watu mbalimbali. Katika hao watu wapo waliokuwa wakiwafahamu kina Unyeke. Sasa nikaanza kusikia tetesi kutoka kwa mtu mmoja kwamba kina Unyeke wapo uraiani, kuna mtu aliwaona.”
Kijana huyo akaendelea kunieleza:
“Kwanza sikuamini ile habari, lakini nilikuja kuisikia tena kwa mtu mwingine ndipo nilipoanza uchunguzi. Nilifanya uchunguzi kwa miezi mitatu mpaka nikathibitisha kuwa kweli hao watu walitoroshwa jela na mkuu wa gereza.”