Dar es Salaam. Wanaharakati wa haki za wanawake wameongeza msukumo kwa Serikali kufanya marekebisho ya sheria zilizopitwa na wakati, hususan zile za kimila, wakisema ndizo chanzo kikuu cha aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia unaoendelea kukithiri, hususan kwa kutumia majukwaa ya kidijitali.
Wito huo umetolewa leo, Ijumaa Oktoba 3, 2025 na Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF), Anna Kulaya, wakati wa mdahalo wa kitaifa kuhusu ukatili unaofanywa kwa kutumia teknolojia na ukatili dhidi ya wanawake katika uchaguzi.
Mdahalo huo ni sehemu ya maandalizi ya kampeni ya kimataifa ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, inayolenga kuhamasisha jamii kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake, hususan katika mazingira ya kisiasa na kijamii.
Kulaya amesema licha ya juhudi za muda mrefu za kutaka mabadiliko ya sheria, bado zipo sheria kandamizi zinazowanyima wanawake haki za msingi kama vile kumiliki na kurithi mali.
“Kwa miaka mingi tumekuwa tukipaza sauti tukitaka marekebisho ya sheria za kimila zinazowanyima wanawake haki ya kurithi ardhi na mali nyingine. Kukosekana kwa haki hii kumesababisha ukatili wa kisaikolojia, na mara nyingine humkatisha mwanamke tamaa ya kushiriki kwenye siasa kutokana na unyanyasaji wa mtandaoni,” amesema.

Amesema teknolojia, licha ya kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo, imekuwa pia chanzo cha ukatili mpya, ambapo wanawake wanaojihusisha na shughuli za kisiasa au kijamii hukumbwa na ujumbe wa matusi na vitisho mitandaoni, hali inayowaathiri kisaikolojia na kuwadhoofisha kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi.
Akinukuu utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women), Kulaya amesema zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wamepitia aina mbalimbali za ukatili, ukiwemo unyanyasaji wa kisaikolojia na ule unaotokana na matumizi ya teknolojia.
“Kuna sheria kadhaa zinazohitaji kurekebishwa kwa haraka, kama Sheria ya Ndoa. Nchi nyingine zimeweza kupitisha sheria maalumu za kukabiliana na ukatili wa kijinsia. Dunia inavyoendelea na teknolojia kama akili unde (AI) kuwa sehemu ya maisha ya kila siku, nasi tunapaswa kuchukua hatua sasa,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Tanzania Women Cross Party (TWCP), Dk Ave-Maria Semakafu, amesema ukatili wa mtandaoni ni tishio kubwa kwa wanawake na unawakatisha tamaa kushiriki katika siasa na uongozi.
“Mwanamke anaweza kutumiwa ujumbe wa matusi moja kwa moja kwenye simu yake, lakini hata akijaribu kutafuta haki, haipatikani licha ya kuwa na ushahidi wa kutosha. Mahakama mara nyingi hukataa ushahidi wa ujumbe wa simu kwa madai kuwa sheria zilizopo hazitambui ushahidi wa namna hiyo, jambo linaloendeleza ubaguzi dhidi ya wanawake,” amesema.
Dk Semakafu ameongeza kuwa sasa hivi unyanyasaji huo unafanyika hata katika mahusiano ya karibu, ambapo mwanamke hupokea vitisho kutoka kwa mwenza au jamaa wa karibu, akimtaka ajiondoe katika shughuli za kisiasa au kijamii.
“Matokeo yake, wanawake wengi huogopa kudai haki zao za kidemokrasia. Kupitia jukwaa hili, tunalenga kuandaa azimio la pamoja litakalowahamasisha na kuwawezesha wadau kushirikiana katika kutokomeza ukatili huu,” amesema.