Skauti wa Simba ajiweka pembeni, afichua ishu nzito

Skauti Mkuu wa Simba, Mels Daalder amejiuzulu rasmi nafasi yake leo, Oktoba 4, 2025.

Daalder amesema kuwa ameamua kujiondoa katika nafasi hiyo kwa vile hajioni kama ana nafasi siku za usoni.

“Nimeamua kujiuzulu nafasi yangu kama Mkuu wa Skauti ndani ya Simba SC kwa vile sijitambui tena katika muelekeo wa klabu.

“Katika safari hii nzima nimekumbana na changamoto nyingi lakini nyakati hizo zote zimenijenga na kufanya mafanikio kuwa ya maana.  Jambo muhimu zaidi lilikuwa kufikia Fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF msimu wa 2024/2025, kumbukumbu ambayo nitatunza daima.

“Napenda kumshukuru kwa dhati Rais wa Klabu, Mohamed Dewji, Aliyekuwa Kocha Mkuu Fadlu Davids na wafanyakazi wake kwa uaminifu wao na ushirikiano mkubwa. Zaidi ya yote, shukrani zangu ziwaendee mashabiki, damu ya klabu hii kwa mapenzi yao na usaidizi usioyumbayumba.

“Ninaacha jukumu langu, lakini sio kwa upendo wangu. Nitaunganishwa na Simba kama shabiki, na ninatazamia siku zijazo katika soka,” amesema Daalder.

Kuondoka kwa Daalder kumetokea wiki chache tangu aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Fadlu Davids kuikacha Simba na kujiunga na Raja Casablanca ya Morocco.

Kuondoka kwa Fadlu kumeifanya Simba iamue kumchukua Dimitar Pantev ambaye imempa nafasi ya Umeneja.