DCEA yateketeza tani nne za dawa za kulevya zilizohifadhiwa kama vielelezo

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeteketeza zaidi ya tani nne za dawa za kulevya ambazo zilihifadhiwa kama vielelezo vya mashauri mbalimbali yaliyopo mahakamani.

Shughuli hiyo ilifanyika jana Oktoba 3, 2025 kwenye eneo la kiwanda cha saruji cha Twiga kilichopo Wazo jijini hapa, likiongozwa na Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo aliyetangaza msamaha kwa wauzaji wa dawa hizo watakaojisalimisha.


“Wapo wengi, mapapa wa dawa za kulevya, wengine wamekimbilia nchi mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika, tunaendelea kuwafuatilia katika nchi walizokimbilia ili sheria ifuate mkondo wake,” amesema Lyimo, akitoa wito kwa wanaojihusisha na biashara hiyo kuacha mara moja.

Amesema wale watakaoacha na kujisalimisha, Mamlaka haitowachukulia hatua zozote, itashirikiana nao ili kutokomeza kabisa mtandao wa dawa za kulevya nchini.

Akizungumzia uteketezaji wa dawa za kulevya uliofanyika leo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema jumla ya kilogramu 4,402.02 (zaidi ya tani nne) zimeteketezwa.


 Amezitaja dawa zilizoteketezwa kuwa ni  kilogramu 2,168.18 za methamphetamine, kilogramu 1,064.29 za heroin na gramu 326.95 za cocaine.

Nyingine ni kilogramu 515.48 za bangi na kilogramu 653.74 za mirungi.

Amesema dawa hizo zilihifadhiwa kama vielelezo vya mashauri mbalimbali yaliyopo mahakamani ambayo baadhi ya mashauri bado yanaendelea kusikilizwa huku mengine yakiwa tayari yametolewa hukumu.


“Kwa mashauri ambayo bado hayajakamilika, Mahakama iliagiza dawa hizo kuteketezwa kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo.

“Kama sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya ya mwaka 2015 inavyotaka vielelezo vya dawa za kulevya kuharibiwa wakati shauri likiendelea au baada ya hukumu kutolewa,” amesema Lyimo.

Amesema miongoni mwa mashauri yanayohusiana na dawa zilizoteketezwa ni kesi ya Najim Abdallah Mohamed iliyohusisha heroin kilogramu 882.71 na methamphetamine kilogramu 2,167.29.


 Katika mashauri yaliyotolewa hukumu, Kamishna Jenerali Lyimo  amesema ni pamoja na la Hassan Azizi, Salum Shaaban Mpangula na Hemed Juma Mrisho (Hororo) ambao kwa nyakati tofauti walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha.

Mashauri mengine ni la Ramadhan Shaban Gumbo aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, Irene Dickson Mseluka aliyehukumiwa miaka mitano jela na Gema Victor Mmasy aliyehukumiwa miaka mitatu jela.

“Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kisheria na kiutendaji kuhakikisha Tanzania inalindwa dhidi ya madhara ya dawa za kulevya.

“Sambamba na hatua hizo, Mamlaka itaendelea kuutaarifu umma kuhusu taarifa zinazohusu dawa za kulevya na kuimarisha ushirikiano na wananchi katika mapambano haya,” amesema.