Pantev aahidi soka safi, Simba yazungumzia ishu yake ya leseni

MENEJA Mkuu wa Simba raia wa Bulgaria, Dimitar Pantev, amewasili kwa ajili ya kukiongoza kikosi hicho huku akiahidi kutengeneza timu ya ushindani, itakayocheza soka safi na la kuvutia.

Pantev amewasili leo mchana Oktoba 4, 2025 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja tangu atambulishwe kufuatia kuondoka kwa Fadlu Davids.

“Ni mapema sana kuahidi chochote kwa sasa, ila ninachoweza kuwaambia mashabiki watarajie aina nzuri ya uchezaji kwa sababu ndio kitu muhimu kwetu na wenzangu,” amesema Pantev.

Aidha kocha huyo, alisema sababu kubwa iliyomshawishi kujiunga na Simba ni kutokana na ukubwa wa timu hiyo na mipango endelevu ya kikosi hicho.

AMEWA 01


“Nilikuwa na ofa nyingi lakini baada ya Simba kuonyesha uhitaji na kunielezea mipango yao, kiukweli nilishawishika na kuomba waajiri wangu Gaborone United kuniruhusu na nawashukuru sana kwa kuelewa mahitaji yangu,” amesema.

KUHUSU UTAMBULISHO WAKE
Baada ya sintofahamu nyingi kuhusiana na Pantev kutokidhi vigezo vya kusimama kama kocha mkuu wa benchi la ufundi huku Simba ikimtambulisha kama Meneja Mkuu na sio Kocha Mkuu, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kilichofanyika ni kubadili muundo wa timu hiyo.

“Kumuita Pantev meneja maana yake sisi tumebadilisha muundo wetu, kwa maana yeye ndiye atakayesimamia uendeshaji mzima wa kikosi hicho.

AMEWA 02


“Pantev atahusika na mapendekezo ya mchezaji gani asajiliwe, wa kuachwa, wa kutolewa kwa mkopo, kufuatilia kiwango cha mchezaji mmoja mmoja na tathimini ya ujumla ya kikosi chetu, ndio maana tukampa cheo hicho ili isiwe ndani ya uwanja tu, bali shughuli zote ahusike mwenyewe,” amesema Ally.

Sababu za kuzuka kwa mjadala huo ni kutokana na Kocha huyo kuwa na Leseni ya UEFA A, tofauti na inayotakiwa ya UEFA Pro kwa ajili ya kuiongoza timu kama kocha mkuu kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa yaliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Kutokuwa na Leseni ya UEFA Pro, kunamfanya Pantev kupoteza sifa hiyo.

AMEWA 03


Pantev mwenye umri wa miaka 49, alizaliwa Juni 26, 1976, jijini Varna huko Bulgaria, ambapo amewasili kuanza kufanya kazi akiwa na Kocha Msaidizi, Simeonov Boyko Kamenov ambaye naye ni raia wa Bulgaria.

Simba ni timu ya tano kufundishwa na Kocha Pantev barani Afrika, kabla ya hapo amezinoa Victoria United ya Cameroon, FC Johansen ya Sierra Leone, Orapa na Gaborone United za Botswana.

Pantev amecheza soka hadi katika ngazi ya Ligi Kuu ambapo alikuwa akicheza kwenye nafasi ya kiungo.

AMEWA 04


Akiwa mchezaji amezitumikia timu za Cherno More, FC Suvolovo, Chernomorets Byala, Kaliakra Kavarna, Chernomorets Balchik, Volov Shumen, Dobrudzha, Vladislav, Shabla na Spartak Varba.

Maisha yake ya ukocha yalianzia katika kikosi cha vijana cha Varna City kisha akawa Kocha Msaidizi wa Al Ahli Hebron kisha akawa Kocha Mkuu katika timu za Flamengo, Victoria United, Johansen, Orapa na baadaye Gaborone United.

Katika miaka hiyo mitano aliyofundisha Afrika, ametwaa mataji mawili ya ligi Kuu katika timu mbili kutoka mataifa mawili tofauti ambayo ni ya Ligi Kuu Cameroon na Ligi Kuu Botswana.

AMEWA 05


Muda mwingi ameutumia kufundisha mchezo wa Futsal na ametwaa mataji matano ya Ligi Kuu Bulgaria ya mchezo wa Futsal.

Ameondoka Gaborone United akiwa ameitumikia kwa muda wa miezi minane (siku 254) tangu alipojiunga nayo Januari 23 mwaka, huku akiipa ubingwa wa Ligi ya Botswana msimu wa 2024-2025.