Moto mwingine wazuka Kariakoo, stoo ya pafyumu yaungua

Dar es Salaam. Stoo ya kuhifadhia manukato (pafyumu) iliyoko katika ghorofa ya barabara za Msimbazi na Mkunguni, Kariakoo, imeungua usiku wa kuamkia leo huku chanzo cha moto huo kikiwa bado hakijajulikana.

Moto huo umetokea ikiwa ni siku 13 tangu stoo nyingine ya kuhifadhia mizigo ikiwamo viatu kuungua moto katika Mtaa wa Narung’ombe ambapo chanzo chake hakikujulikana huku uchunguzi ukiendelea.

Jengo hilo limeongeza idadi ya majengo yaliyoungua kufikia manne katika kipindi cha miezi mitatu huku Agosti pekee yakiungua majengo mawili ndani ya wiki mbili.

Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 4, 2025, Kamishna Msaidizi wa Zimamoto Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi amesema moto huo ulitokea katika sehemu ya juu ya jengo la ghorofa tano ambalo linajumuisha maduka na makazi ya watu.

“Jengo hili lina ground floor na first floor ambazo ni maduka kama kawaida huku kuanzia ghorofa ya pili hadi ya tano ni makazi ya watu. Sehemu ya juu kabisa ya jengo, juu ya roshani (rooftop), kulikuwa na stoo ya kuhifadhia manukato,” amesema Mabusi.

Amesema moto umetokea kwenye stoo ya juu na wao walipokea taarifa saa 5 usiku na timu yao ilifika eneo la tukio haraka kwa sababu hakukuwa na msongamano katika barabara na kufanikiwa haraka kabla haujasambaa kwenye sehemu za chini.

Mabusi amesema moto huo ulizimwa kabla haujaleta madhara makubwa kwa wakazi wa jengo hilo, ingawa bidhaa nyingi za manukato zilizokuwa kwenye stoo zilizoungua.

“Tunafanya uchunguzi kubaini chanzo cha moto, lakini bidhaa kama hizi za manukato huwa na hatari ya kuwaka kwa urahisi kutokana na kemikali zake,” amesema Mabusi na kuongeza kuwa.

“Kimsingi tulimaliza kazi mapema, hakuna madhara makubwa zaidi ya hasara ya mali. Tuliondoka eneo la tukio saa 6 usiku baada ya kuhakikisha hakuna moto wowote unaoweza kujirudia,” amesema.

Dereva wa bodaboda aliyeshuhudia tukio hilo, Hassan Mfaume amesema alisikia vitu vikilipuka akijua ni fataki lakini ghafla aliona moshi wakati akielekea barabara ya Uhuru.

“Nilisikia kama baruti wakati natokea Fire, nafika katika mataa ya msimbazi nikaona moshi na watu wakipiga kelele za moto lakini ghafla niliona gari la zimamoto,” amesema Mfaume.

Mfanyabiashara wa nguo za ndani katika jengo hilo, Asha Mtulia amesema alipigiwa simu kuwa jengo alilopanga linawaka moto na bidhaa zao zinaungua.

“Ilikuwa kama saa 6 usiku, nilipigiwa simu, kilichoungua ni stoo za wenzangu wanapohifadhia mizigo yao ya pafyumu, hata hivyo kwa sasa Kariakoo inatuogopesha hujui kesho biashara ya nani itateketea,” amesema Asha.

Naye mfanyabiashara karibu na jengo hilo na mkazi wa Kimara Zainabu Ramadhani amesema alipigiwa simu na jirani yake kuwa jengo analofanyia biashara linaungua hivyo alichukua pikipiki kufika katika eneo hilo.

“Nilipigiwa simu saa sita usiku nikaambiwa kuna moto mkubwa unaunguza jengo letu, lakini kufika hapa nilikuta jengo la jirani yetu ndiyo linawaka moto cha muhimu watu wapo salama kilichoungua ni bidhaa,” amesema Zainabu.