Gamondi aiteka paredi Singida, Mwigulu akipiga msumari wa taji Ligi Kuu

MAMIA ya mashabiki wa Singida Black Stars wamejitokeza leo Oktoba 4, 2025 katika mapokezi ya kikosi hicho ambacho kimerejea mkoani humo baada ya kutwaa ubingwa wa michuano ya Kagame.

Paredi ya kikosi hicho, imeanzia maeneo ya Puma saa 8:00 mchana, nje kidogo ya mkoa huo huku kukiwa na msafara wa magari na pikipiki kuelekea mjini kwenye Uwanja wa Bombadia.

Ilikuwa paredi ya umbali wa zaidi ya kilometa 20 huku msafara huo ukitembea taratibu, mara baada ya kuwasili Singida kutoka jijini Dar es Salaam.

Baada ya kufika kwenye Uwanja wa Bombadia, nahodha wa kikosi hicho, Kennedy Juma alishuka na Kombe la Kagame na moja kwa moja kwenda kulikabidhi kwa mgeni rasmi.

Mgeni rasmi ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ambaye alikuwa meza kuu pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe pamoja na viongozi wengine.

Akizungumzia mafanikio waliyoyapata, Mwenyekiti wa Singida Black Stars, Ibrahim Mirambo kipekee alitoa shukrani kwa wachezaji wa timu hiyo, makocha na walezi wao.

Baada ya salamu za hapa na pale pamoja na utambulisho wa wachezaji wote wa Singida Black Stars, kocha wa kikosi hicho, Miguel Gamondi alitoa neno la shukrani kwa mapokezi makubwa kwa watu wa Singida.

“Niwapongeze wachezaji, wenzangu wa benchi la ufundi na viongozi kwa kazi nzuri ambayo tumefanya pamoja, bado tuna kazi ya kufanya,” amesema.

Baada ya kutia neno, Gamondi aliwatoa kimasomaso mashabiki wa Singida kwa kuimba wimbo wake pendwa wa Jaiva uitwao Kautaka.

SAPRAIZI YA MWIGULU
Mishale ya saa 10 kasoro, Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alitinga uwanjani hapo ikiwa ni muda mchache tangu atoke kwenye majukumu yake mengine.

Mlezi huyo wa Singida Black Stars, aliibua shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo huku akipata nafasi ya kuzungumza na Wanasingida.

“Nina furaha kubwa kwa kombe hili kuwa katika ardhi ya mama yangu hapa Singida, tulikuwa na kikao cha chama sasa nilivyosikia habari za timu kufika na mimi nikasema sitachelewa kuona huu utukufu, nimpongeze kocha na wachezaji kwa ushindi huu mkubwa lakini pia ninawapongeza wachezaji wa 12 ambao ni mashabiki kwa kutoa nguvu kwa wachezaji.

“Sisi kama ilivyo kwa mkulima wa ng’ombe, tunafuata kile kinachofanywa, naamini makubwa zaidi yanakuja na mimi nitakuwa bega kwa bega kufanikisha hilo ambalo limesemwa la ubingwa wa ligi kuja hapa,” amesema.

Mara baada ya Mwigulu kuzungumza, alirudishwa tena Gamondi na kuanza kuimba na kucheza naye wimbo wake pendwa wa Kautaka akiwa sambamba na viongozi wengine.

Singida Black Stars imeweka historia kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Cecafa Kagame kwa mara ya kwanza baada ya kuifunga Al Hilal ya Sudan mabao 2-1 katika mechi ya fainali iliyopigwa Septemba 15, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.