Samia ahitimisha kampeni Kanda ya Kaskazini akiahidi kukuza uchumi Manyara

Babati. Samia Suluhu Hassan, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, amehitimisha kampeni kanda ya Kaskazini akieleza mkakati wa kuufungua Mkoa wa Manyara kwa kuendeleza nguzo kuu za uchumi mkaoni humo.

Nguzo hizo ni kilimo, ufugaji, utalii, biashara na shughuli za uchimbaji madini, ambazo amesema zinatengeneza ajira kwa watu wengi.

Akizungumza leo Oktoba 4, 2025 kwenye mkutano uliofanyika Babati, amesema akipata ridhaa ya wananchi, Serikali itahakikisha shughuli hizi zinaendelezwa ili kukuza uchumi na kuongeza fursa zaidi za ajira.


Vilevile amesema wataendelea kutoa pembejeo, mbolea za ruzuku na mbegu za kisasa kuwawezesha wakulima kufanya kilimo chenye tija.

Pia, Serikali itatafuta masoko na kuhakikisha wakulima wanauza kwa bei nzuri.

“Kama nilivyosema Hanang na leo narudi kuwasisitiza tunataka wakulima wa Manyara waongeze kasi ya kulima ngano ili kufikia mwaka 2030 tufikie tani milioni moja. Hilo lifanyike pia kwa mazao mengine yanayolimwa mkoa huu,” amesema.

Amesema jitahada za kuhamasisha kilimo zitaenda sambamba na mkakati wa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.


Kuhusu uvuvi ameahidi kutoa boti nne kwa ajili ya wavuvi, moja ikiwa ya kuangalia usalama Ziwa Manyara. Pia, mtambo wa kusafisha Ziwa Babati ili kuondoa magugu kuwezesha uvuvi na utalii.

Katika sekta ya madini ameahidi kuwa na kongani za viwanda vya kuyaongeza thamani na kupima ardhi kubaini maeno mengine yenye madini.

“Tutaendelea kupima maeneo ya nchi kubaini mahali yalipo madini, kipaumbele chetu kitakuwa wachimbaji wadogo ili kutengeneza ajira za vijana,” amesema.


Vilevile ameahidi kujenga minara ili kusogeza huduma za mawasiliano katika vijiji vyote vya mkoa huo, akieleza simu ndiyo kila kitu.

Amehimiza wananchi kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, akisema: “Niwasisitize mabalozi usitoke peke yako pitia wananchi wako katika nyumba zako zote uende nao kituo cha kupiga kura. Msisitizo wangu kwa wana CCM twendeni tukakipe heshima chama chetu, wale wenye midomo midomo tukawaonyeshe kwa wingi wa kura tukaendelee kulinda heshima yetu barani Afrika.”

Aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, Cecilia Pareso amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura akisema:

“Uchaguzi upo na utafanyika, tuepeuka propaganda na tuogope matapeli wa siasa, itakapofika Oktoba 29 tujitokeze kwa wingi kupiga kura.”

Amemnadi Samia akisema ni mchapakazi, muadilifu, msikivu na mbunifu, hivyo ndiye kiongozi anayehitajika kwa miaka mitano ijayo.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima amemuhakikishia mgombea huyo ushindi wa kishindo akisema: “Ilani iliyopita imetekelezwa kwa asilimia 100, ilisema uchumi wa wananchi uimarishwe hilo limefanyika. Sisi kama chama tumeridhishwa na kila kilichofanyika ndiyo sababu tunasema utapata ushindi wa kishindo.”

Mratibu wa kampeni za chama hicho Kanda ya Kaskazini, Frederick Sumaye amesema Samia ni kiongozi mwenye upeo wa mbali na uvumilivu wa hali ya juu licha ya kushambuliwa.

“Hakutaka kuangalia miaka mitano ya uongozi wake, akatengeneza Dira ya Taifa ili kutengeneza barabara ya miaka 25 ijayo. Kingine huyu mama ni mvumilivu, wanamsema kwa mengi lakini anavumilia,” amesema na kuongeza:

“Ukweli ni kwamba anayepigwa vita siyo Samia, bali CCM. Wapo watu kutoka ndani na nje ya nchi wanaotaka chama hiki kianguke. Bahati mbaya wanakuta CCM haitikisiki hivyo wanaamua kuhamia kwa mwenyekiti.”

Katika mkutano huo, aliyekuwa mgombea ubunge Simanjiro kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Olekai Laizer alitangaza kujiunga na CCM akieleza aligundua upande huo amepotea.

Hilo limetokea zikiwa zimesalia siku 25 kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema chama hicho kinatambua kuna jitihada zinazofanyika kuwarubuni wagombea wake.

“Hata hivyo sisi hatuwezi kumlazimisha mtu, tunachoweza kuwaambia wanachofanya ni usaliti maana waliaminiwa na kupewa nafasi hiyo, pili hiki kinachoendelea ni hasara maana karatasi za kupigia kura zimeshatengenezwa,” amesema.

Wengine waliojiunga na CCM ni ni Katibu wa Chadema jimbo la Babati Mjini, Abubakar Nyaisanga na Katibu wa vijana wa ACT-Wazalendo, Daniel Oledodo.