Kocha wa JKT Tanzania aja na mkakati mzito

KOCHA Mkuu wa Maafande wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema mojawapo wa mikakati mikubwa anayoifanyia kazi kipindi hiki cha kupisha kalenda ya Fifa ni kuhakikisha Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo unakuwa mwiba mkali kwa timu pinzani Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ahmad amesema anachohitaji kwa sasa ni kutengeneza na kuendeleza rekodi bora wakiwa uwanja wa nyumbani, licha ya kutambua sio rahisi kutokana na ushindani mkali uliopo kutoka kwa kila mpinzani wanayekutana naye.

“Tunahitaji kutengeneza ufalme katika uwanja wetu wa nyumbani kwa kuhakikisha unakuwa mgumu kwa kila mpinzani wetu msimu huu, hii itafanikiwa ikiwa tutaendelea kuonyesha kwa vitendo na mwendelezo mzuri utakaojenga hofu kwao,” amesema Ahmad

AHM 02


Sare ya timu hiyo ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Azam FC, Oktoba 1, 2025, imekifanya kikosi hicho kucheza jumla ya mechi 16 za Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Isamuhyo, kuanzia msimu wa 2024-2025 hadi sasa.

Katika mechi hizo 16 za Ligi Kuu Bara ilizocheza JKT Tanzania katika uwanja huo wa nyumbani, imeshinda mitano, sare tisa na kupoteza miwili, ambapo kikosi hicho kimefunga jumla ya mabao 18 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12.

AHM 01


Mechi hizo mbili ilizopoteza kuanzia msimu wa 2024-2025 hadi sasa, ni kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars, Februari 13, 2025 lililofungwa dakika ya 51 na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho Mghana Jonathan Sowah aliyehamia Simba.

Kichapo kingine ilichokipata JKT kwenye uwanja huo, kilikuwa pia cha kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Simba, katika mechi kali na ya kusisimua iliyopigwa, Mei 5, 2025, lililofungwa na aliyekuwa kiungo wa kikosi hicho, Fabrice Ngoma dakika ya 45+6.