Watano wauawa Tunduru, Polisi wakamata 15

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linachunguza mauaji ya kikatili ya watu watano na wengine watatu kujeruhiwa, tukio linalosadikiwa kuhusisha wafugaji katika Kijiji cha Wenje, Kata ya Narasi Magharibi, wilayani Tunduru.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chillya amethibitisha tukio hilo akieleza lilitokea Oktoba mosi, 2025 saa saba usiku katika Kitongoji cha Likologo.

Amesema miili ya wananchi waliopoteza maisha ilikutwa wameuawa katika maeneo tofauti kwa kukatwa na kuchomwa na vitu vyenye ncha kali mwilini.

Amewataja waliofariki dunia kuwa ni Mfaume Ali (68), Imani Abdu (50), Abdalla Biashara (37), Mipango Mwituta (54) na Khamis Shaibu (13).

Majeruhi ni Jana Athmani (46), Khalifa Mbahu (49) na Mahara Mahara (56), ambao wamelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Mtakatifu Augustine wakipatiwa matibabu.

Amesema baada ya taarifa za tukio hilo kuripotiwa kituo kikuu cha Polisi, askari walianza msako uliowezesha kukamatwa watuhumiwa 15, ambao bado wanaoshikiliwa kwa mahojiano.

Amesema katika msako pia walikamata vifurushi vitano vya nyama ya ng’ombe na mikuki inayosadikiwa kutumika katika mauaji hayo.

Kwa mujibu wa kamanda, inadaiwa siku moja kabla ya tukio hilo, Septemba 30, 2025, saa 11:00 jioni, mkazi wa Kijiji cha Nakapunda, Hassani Moshi akiwa shambani alishambuliwa na mfugaji ambaye jina lake halijafahamika.

Baada ya tukio hilo, amesema wananchi wa Kijiji cha Nakapunda wapatao 100 waliwafuata wafugaji kwenye makazi yao kwenye Kitongoji cha Likologo, ambao nao baada ya kuona idadi kubwa ya wananchi ikiwafuata, walikimbia na kuacha mifugo yao.

Amesema wananchi walikwenda kufungua zizi la ng’ombe, wakawachinja na kuchukua nyama.

Kamanda amesema wakiwa njiani na vifurushi vya nyama wakirudi kijijini kwao, walivamiwa na kundi la wafugaji waliowashambulia kwa mapanga na mikuki na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi watatu.

Jeshi la Polisi linaendelea na msako ili kuwakamata watuhumiwa waliotoroka, huku likionya wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi.

“Tunaendelea na uchunguzi wa kina, baada ya kukamilika watuhumiwa wote watapelekwa mahakamani. Tunatoa rai kwa wananchi kutatua migogoro kwa njia za kisheria badala ya kutumia nguvu,” amesema.

Katika video zilizosambaa mtandaoni, mkazi wa Kijiji cha Nakapunda, Mwinyi Kuwale, amesema chanzo cha tukio hilo ni kupotea ngʼombe mmoja wa wafugaji.

Amesema wakati wakimtafuta walikutana na kijana akilima shambani kwake, ambaye walimuuliza kuhusu ng’ombe huyo na alipowajibu hajamuona wakampiga.

“Baada ya kuja kina mama, wafugaji walikimbia, vijana waliitwa kwa ajili ya kumpeleka hospitali, huku wakulima wakianza kuwatafuta wafugaji katika makambi yao lakini walikuwa wameshahama,” amesema.

Amesema baadaye wafugaji na wakulima walikutana ndipo ugomvi ulipoanza na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi watatu.

Kuwale ameiomba Serikali kuwaondoa wafugaji katika eneo hilo akidai wanapopotelewa na mfugo huhisi waliochukua ni wakulima.

Naye, Mohamed Kawale,  aliyejeruhiwa na wafugaji Agosti 26, 2025 amesema usalama wao kwa sasa ni mdogo kwani alishapata hasara ya mazao yake kutokana na uingizaji wa mifugo katika mashamba yake.

“Mwaka huu nimeona wameingiza ng’ombe wao zaidi ya 150 ndani ya kijiji katika eneo ambalo sisi tunapata huduma za mboga, tulipohoji walichukua fimbo na kunipiga kichwani, nilipozuia walinivunja mkono na nilitoa taarifa kituo cha polisi kijijini kwetu na kupewa ruhusa (fomu) ya kwenda Hospitali ya Ndanda,” amesema.

Mkazi mwingine, Karafa Jasa, amesema siku tatu nyuma ndugu yao Hassan Mponda, alipigwa na wafugaji akiwa nyumbani kwake.

“Wananchi walivyofika katika nyumba ya Hassan namna walivyomuona, walijawa na jazba kwa sababu wiki zilizopita viongozi wa wilaya walikuja na kuahidi vitu vingi, ikiwepo kuwafukuza wafugaji,” amedai.