Mwinyi kujenga ghati la kudumu Tumbatu

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk Hussein Mwinyi, ameahidi kuwajengea ghati la kudumu wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu ili kumaliza changamoto ya kushindwa kutoka na kuingia wakati maji ya bahari yanapoondoka.

Vilevile, ameahidi ataipandisha hadhi Tumbatu kuwa wilaya kamili, kutoka wilaya ndogo ya sasa.

Akihutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni leo Oktoba 4, 2025 katika uwanja wa Shule ya Tumbatu, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk Mwinyi  amesema wameshamwagiza mkandarasi kujega ghati.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Mwinyi akizungumza katika mkutano wa kampeni kisiwani Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja



“Hii ni changamoto kubwa hapa Tumbatu, maji yanapoondoka watu wanashindwa kuingia au kutoka, hata kama mtu akiwa anakwenda hospitali anatatakiwa kusubiri,” amesema.

Ili kuondokana na changamoto Dk Mwinyi amesema: “Tukirejea madarakani tutaifanya kuwa wilaya kamili, hiki ni kilio pia cha muda mrefu.”

Dk Mwinyi amesema wanaendelea na ujenzi wa hospitali ya wilaya katika kisiwa hicho, ili kuwaondolea adha ya kuvushwa majini kwenda Hospitali za Unguja kwa ajili ya kupata huduma.

“Madaktari walikuwa wanakuja huku kwa wiki mara moja, wakati mwingine mwanamke anataka kujifungua, mpaka avushwe kwenda Unguja, wakati mwingine ndio maji yanakuwa yametoka, sasa hayo yote tunakwenda kuyakomesha,” amesema.

Amesema baada ya hospitali hiyo kukamilika kila huduma itafanyika kisiwani humo, kwani watapelekwa madaktari wa kutosha na vifaa vya kisasa.

Wananchi, wananchama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi wakiwa kwenye mkutano wa kampeni wakati mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho Dk Hussein Mwinyi akiomba kura kisiwa cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja



Kuhusu barabara, amesema wataalamu wameshauri kusafirisha lami itakuwa vigumu maana itafika ikiwa imeganda, hivyo watajenga barabaraza kwa kutumia zege na kazi imeanza, mkandarasi yupo anaendelea.

“Kisiwa kizima kitakuwa na barabara za zege, kila sehemu itakuwa ni kuteleza tu,” amesema.

Dk Mwinyi amesema wamejenga tangi la ujazo wa lita milioni moja lakini visima vilivyochimbwa vimeonekana havina uwezo wa kujaza tangi hilo.

“Kwa hiyo nimeshaagiza Zawa (Mamlaka ya Maji Zanzibar), kuvusha kiasi cha maji kinachobakia kutoka Unguja yaje mpaka hapa, kwa kipindi kifupi maji hayatakuwa tena changamoto katika kisiwa hiki,” amesema.

Kuhusu elimu, amesema wataendelea kujenga shule za kisasa, kujaza vifaa, maabara na maktaba ili watoto wapate ufaulu wa kimataifa.

Ameeleza wamejenga shule moja ya ghorofa na watajenga nyingine, mipango inatekelezwa ndani ya muda mfupi wakirejea madarakani.

Wananchi, wananchama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi wakiwa kwenye mkutano wa kampeni wakati mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho Dk Hussein Mwinyi akiomba kura kisiwa cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja



Dk Mwinyi amesema ajenda kubwa ya chama hicho ni kusimamia amani, mshikamano na umoja wa Wanzanzibari, kwani bila vitu hivyo hata hayo wanayosema hayawezi kufanyika.

“Chama cha Mapinduzi kimejizatiti kudumisha amani, umoja na mshikamano na sisi hii ndiyo ajenda yetu kubwa kuliko nyingine, kwa hiyo tuwe makini na watu wanaoona amani ni kitu cha ziada,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, amesema kumchagua Dk Mwinyi watakuwa wamechagua maendeleo.

Amesema mgombea huyo yupo tayari kuwatumikia Wazanzibari kwa sababu ni mwadilifu, anapenda kazi na kuwatumikia Wazanzibari wote, hivyo siku ya kupiga kura kila mmoja atoke kukipigia chama hicho.