Zimwi la Max, Pacome linavyomwandama Manula

MNAHESABU lakini? Ilianza kama utani mara baada ya pambano la Dabi ya Kariakoo lililopigwa Novemba 5, 2023.

Katika pambano hilo la duru la kwanza la msimu wa 2023-2024, Simba ilipigwa mkono na Yanga kwa kufumuliwa mabao 5-1 na kusababisha tafrani Msimbazi.

Lakini, kama huna kumbukumbu nzuri ni kwamba mabao ya Yanga yalifungwa na Maxi Nzengeli aliyetupia mawili, Pacome Zouzoua, Kennedy Musonda na Stephanie Aziz KI waliofunga bao moja moja.

Mabosi wa Simba waliamua ‘kumla kichwa’ kocha Roberto Oliveira ‘Robartinho’ siku mbili baadaye. Hata hivyo, mambo hayakuishia hapo, kwani msala ulihamia kwa kipa namba moja wa timu hiyo kipindi hicho aliyekuwa langoni Simba ikidhalilishwa na vijana wa Miguel Gamondi.

Ndio. Kipa Aishi Manula alitupiwa lawama bila kujali kama alipewa mechi akitoka kuwa majeruhi na hakuwa na utimamu wa kulicheza pambano hilo kubwa dhidi ya watani waliokuwa wa moto.

Kelele hizo zilimfanya kocha aliyechukua nafasi ya Robertinho yaani Abdelhak Benchikha kumpiga benchi hadi Machi 6, 2024 alipompanga dhidi ya Tanzania Prisons mechi ikipigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na Simba kulala kwa mabao 2-1.

MANU 04


Kama umesahau ni kwamba mabao yote ya maafande hao wa Magereza yaliwekwa kimiani na straika Samson Mbangula dakika ya 44 na 62, huku lile la kufutia machozi la Simba likifungwa na Fabrice Ngoma dakika ya 89.

Sasa kama hujui ni kwamba hilo ndilo likawa pambano la mwisho la Ligi Kuu kwa kipa huyo aliyekuwa Tanzania One ambaye kwa sasa yupo Azam FC, klabu iliyomtambulisha katika Ligi Kuu 2012 na kudumu nayo hadi msimu wa 2017-2018 alipotua Msimbazi akikaa kwa misimu saba.

Dalili za hatari kwa Manula zilianza mapema hata kabla ya mechi hizo, mara aliposajiliwa kipa Ayoub Lakred aliyegeuzwa kuwa namba moja na Manula kupigwa benchi karibu mechi kibao ukiacha pale alipokuwa majeruhi.

Hata alipokuja kocha Fadlu Davids msimu uliopita alimpitisha mswaki kwa msimu mzima bila kumpa mechi yoyote ya mashindano kuanzia Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho Afrika na Kombe la Shirikisho (FA).

Ukihesabu tangu mara ya mwisho Manula adake pambano la Ligi Kuu pale Morogoro hadi leo Jumapili unaposoma taarifa hii ni kwamba mwamba huyo hajacheza mechi ya Ligi kwa siku 578, yaani mwaka mmoja na miezi saba amekuwa ‘mtazamaji’ katika ligi aliyobeba na kutawala tuzo za Kipa Bora akiweka rekodi ya ‘clean sheet’ 19 iliyofikiwa na Mousa Camara msimu uliopita.

MANU 01


MANU 01

Awali, wakati akichomeshwa mahindi katika benchi la Simba zilikuja taarifa kwamba Azam FC ilitaka kumrudisha.

Hesabu zikagoma katika dirisha dogo kwa kilichoelezwa mabosi wa Msimbazi ni kama walikuwa ‘wakimkomoa’ wakitaka amalize kwanza mkataba uliosalia.

Hata hivyo, msimu ukaisha na jamaa akawa mmoja ya mastaa wa awali wa Simba kupewa ‘thank you’ kabla ya kutambulishwa na Azam FC kwamba kijana amerudi nyumbani.

Mashabiki wa soka wakawa na tumaini kubwa la kutaka kumuona Manula akirudi katika milingoti mitatu akiidakia timu iliyompa jina kubwa kabla ya kunyakuliwa na Simba, na kutwaa nayo mataji manne ya Ligi Kuu Bara mfululizo na kuifikisha katika robo fainali karibu sita za michuano ya CAF.

Lakini, kitu alichokutana nacho Azam FC hata mwenyewe huenda haamini, kwani tayari timu hiyo imecheza mechi nne za mashindano zikiwamo mbili za Kombe la Shirikisho Afrika na nyingine kama hizo za Ligi Kuu Bara bila kupewa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.

Kama langoni hatasimama Zuberi Foba, basi atakuwa Issa Fofana aliyesajiliwa hivi karibuni kutoka Al Hilal ya Sudan.

Inadaiwa kuwa kocha mpya wa Azam, Florent Ibenge hana mpango na Manula aliyemkuta ameshasajili wakati anajiunga na timu hiyo, huku akiwa ameshapendekeza Fofana atue kuchukua nafasi ya Mohamed Mustafa aliyekuwa kipa namba moja kabla ya kuachwa msimu huu kwenda Al Hilal, wapinzani wakubwa wa klabu aliyotoka awali kabla ya kutua Azam yaani Al Merrikh.

MANU 02


MANU 02

Kukosa nafasi ya kucheza kwa muda mrefu katika Ligi Kuu Bara hususan alipokuwa Simba na hata sasa akiwa Azam ni kama kumemponza Manula kutemwa hadi timu ya taifa ‘Taifa Stars’ iliyotangazwa hivi karibuni ili kumalizia mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Zambia.

Kocha Hemed Suleimani ‘Morocco’ ameamua kuwaita makipa Zubeir Foba wa Azam, Hussein Masalanga (Singida Black Stars) na Yakoub Suleiman aliyetua Simba akitokea JKT Tanzania ambaye kwa sasa ndiye kipa namba moja wa Stars itakayocheza pia mechi ya kirafiki na Iran, Oktoba 14.

Mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa itapigwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

MANU 03


Akimzungumzia kipa huyo, kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah ‘King’ Kibadeni amesema anaamini Manula bado ni kipa mzuri anayeweza kupambania nafasi hivyo ni wakati wa kutambua Watanzania wengi wana imani naye kubwa kutokana na kiwango chake.

“Nafikiri umri wake bado unamruhusu kucheza, lakini kama unavyojua ni yeye mwenyewe kuamua kushawishi benchi la ufundi wakati wa mazoezi. Kwa sasa kinachoonekana ni mwendelezo wa yaliyokuwa yanamtokea pia akiwa Simba,” amesema.

Kibadeni amesema Manula hakuitwa ‘Tanzania One’ kwa bahati mbaya isipokuwa ni kutokana na kiwango bora alicho nacho, hivyo ikiwa sio mgonjwa kama alivyoripotiwa wakati akiwa Simba, basi anapaswa kupambana kwani nafasi ya kucheza bado ipo kwake.

Kwa upande wa nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua amesema mpira ni mchezo wa nafasi na sio muda wa kumshauri Manula ahame kwa sababu ndio kwanza mashindano mbalimbali yameanza, hivyo kilichobaki kwake ni kuendelea kupambana kikosini.

“Kwa levo za Manula kiukweli inasikitisha kuona hata Azam hapati nafasi ambayo wengi tulikuwa tunatarajia ingekuwa ni njia sahihi ya kurejesha ubora wake ambao Simba ulianza kupotea. Kwangu namshauri asikate tamaa na apambane haswa,” amesema.