Dar es Salaam. Walalamikaji katika kesi ya mgawanyo wa rasilimali dhidiya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameibua jipya, wakitaka wadaiwa, wakiwemo Makamu Mwenyekiti (Bara) wa chama hicho, John Heche na katibu mkuu John Mnyika wafungwe kwa madai ya kudharau amri ya mahakama.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ilifunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Zanzibar na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Walalamikaji pia walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakiiomba mahakama itoe amri kuwazuia kufanya shughuli zozote za kisiasa na kutumia mali za chama, mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Juni 10, 2025 mahakama katika uamuzi ilikubali hoja za walalamikaji, hivyo ilitoa amri ya zuio kwa walalamikiwa kujishughulisha na shughuli zozote za kisiasa. Pia, ikawazuia wao, mawakala au mtu yeyote anayefanya kazi kwa maelekezo au kwa niaba yao, kutumia mali za chama hicho mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Wakati shauri likisubiri kusikilizwa, walalamikaji wamefungua lingine la maombi madogo, dhidi ya wadaiwa katika kesi ya msingi, viongozi wengine na wanachama, wakidai wameidharau mahakama kwa kukiuka amri ya Juni 10.
Mbali ya Heche na Mnyika, wengine ni wanaolengwa na maombi hayo ni Rose Mayemba, Brenda Rupia, Hilda Newton, Twaha Mwaipaya na Gervas Lyenda. Wamo pia wadhamini wa Chadema.
Shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura inayothibitishwa na mmoja wa mawakili wa waombaji, Mulamuzi Byabusha.
Byabusha anadai Heche, katibu mkuu wa Chadema na mawakala wao, wafanyakazi na/au watumishi wao, wamekuwa wakikaidi amri hiyo ya mahakama, hivyo anaiomba mahakama iamuru wakamatwe na kuwekwa kizuizini kama wafungwa wa madai, kwa kukaidi kwa makusudi amri halali ya mahakama.
Anadai kati ya Juni 10 na Septemba 2025, mjibu maombi wa kwanza hadi wa saba wamekuwa wakikaidi waziwazi na mara kwa mara amri halali ya mahakama kwa kuendesha na kushiriki shughuli za kisiasa, zikiwamo mikutano ya ndani ya Chadema, mikutano na wanahabari na hotuba kwa umma juu ya masuala ya kisiasa.
Pia, anadai kwa nyakati tofauti, wamewahamasisha viongozi wengine, mawakala na wanachama wa Chadema kuendelea kufanya shughuli za kisiasa za chama, kinyume cha amri hiyo halali.
Maombi hayo yanaungwa mkono na kiapo cha pamoja cha waombaji/walalamikaji, wakibainisha tarehe ambazo wajibu maombi mmojammoja au kwa pamoja wamekuwa wakifanya shughuli za kisiasa.
Wakati maombi hayo yakisubiri kupangiwa tarehe, kupitia mtandao wa X, Heche ameandika: “Said Issa (mlalamikaji), madai yenu mlisema mnataka mgawanyo wa mali… mara mnataka chama kifungiwe shughuli zake, ambalo halina uhusiano wowote na mgawanyo wa mali… sasa mnataka viongozi wafungwe, sio? Mwisho mtaomba Chadema ifutwe na msajili… Kufuta Chadema siyo kufuta kiu ya mabadiliko, mtashangaa sana.”
Katika kesi ya msingi iliyozua masuala hayo, walalamikaji wanaomba mahakama itamke kuwa wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A (1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.
Vilevile, wanaiomba itamke kwamba, ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Mbali ya hayo, wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya mahakama yatakapotekelezwa na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika pamoja na gharama za kesi.
Walalamikiwa wameweka pingamizi la awali wakihoji mamlaka ya mahakama kusikiliza shauri hilo lenye madai ya kikatiba, kwani inasikilizwa na jaji mmoja.
Pingamizi limepangwa kusikilizwa Oktoba 30, 2025.