RC Dodoma awapigia chapuo bodaboda kwenye uchaguzi

Dodoma. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amelitaja kundi la waendesha pikipiki (bodaboda) kwamba ni watu maarufu katika kuchangamkia fursa, hivyo watu wengine wanapaswa kuiga mfano huo.

Ni kwa mfano huo, ameomba wananchi watumie nafasi ya ujanja huo ili wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi kwani Dodoma ilifanya vibaya katika uchaguzi wa 2020.

Senyamule ametoa kauli hiyo Ijumaa Oktoba 3, 2025 alipokuwa akizungumza na wajasiriamali na makundi ya wenye vikoba kutoka Kata za Jiji la Dodoma.

Senyamule amesema madereva bodaboda hunusa fursa na kuzichangamkia haraka kuliko wafanyabiashara wengine hata wenye mitaji mikubwa.

Amesema madereva hao wakiona mahali kuna watu wamehamia eneo jipya, huwa hawachelewi kujisogeza na mara moja wanaanzisha kijiwe chao.

“Hakikisheni mnachangamkia fursa za uwepo wa Makao makuu, wingi wa watu katika Jiji la Dodoma ni mtaji kwenu lakini mnashindwa kutumia fursa hizo, naomba muige wenzetu wa bodaboda walivyowajanja,” amesema Senyamule.

Amezitaja baadhi ya fursa ndani ya jiji ni uwepo wa uwanja wa ndege Msalato ambao hata kama hawapandi ndege lakini eneo lake lake linafaa kwa kila kundi kwa ajili ya kujipatia kipato.

Akizungumza kuhusu uchaguzi, amesema mwaka 2020 wapigakura wa Mkoa wa Dodoma walijitokeza kwa asilimia 45 tu kwa watu wa vijijini na kwa upande wa jiji hali ilikuwa mbaya zaidi kwani walijitokeza kwa asilimia 20 pekee.

“Ndiyo maana nasema tutumie fursa hii kwa ujanja kama bodaboda, tukijitokeza kwa wingi ndiyo ujanja wenyewe na tutampa deni kubwa yeyote atakayeshinda kwa wingi wa kura katika maeneo yetu.

“Tukisema Dodoma ni fahari ya Watanzania basi tutambue ni fahari kweli, tuchangamkie fursa hii ya kujitokeza kwa wingi tukapige kura maana huo ndiyo ujanja pekee ili walioingia madarakani tukawadai Maendeleo yetu,” amesema Senyamule.

Akizungumza katika kusanyiko hilo, Ofisa Maendeleo Mkoa wa Dodoma, Honoratha Rwegasira amesema lengo la kusanyiko hilo ni kuwapa elimu ya fedha na elimu ya mpigakura ili makundi hayo yaweze kujitambua.

Katika kusanyiko hilo ambalo walishiriki zaidi ya watu 600, amezungumzia changamoto ya fedha kwamba imekuwa ni tatizo kubwa hasa mikopo ambayo haina malengo.

Ofisa mikopo kutoka Benki Kuu ya Taifa (BoT), Fanuel Kijoji amesema mkopo siyo fedha halali ya mkopaji bali bali ni Mali ya mkopeshaji.

Kijoji amesema mkopo ni kifungo ambapo aliyefungua lazima ufike wakati atoke, ndivyo ilivyo watu wakikopa lazima warejeshe.

Hata hivyo, ameshauri wakopaji lazima wale na malengo na waache kukopa kwa mihemko bila kuwepo na mipango lakini watu wajifunze kuweka akina.