Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed, ameahidi kuwa endapo atachaguliwa, ndani ya siku 100 za kwanza atatekeleza mpango wa kusaidia wanawake wasioolewa kupata waume.
Pia, ameahidi ndani ya kipindi hicho za siku 100 atatekeleza mpango wa kuwatafutia wenza watu wenye ulemavu ambao hawajaoa wala kuolewa.
Amesema, kwa sasa watu wenye mahitaji maalumu wengi hawana waume, hivyo atahakikisha kila mmoja anapewa mume wa kumuowa.
Hayo ameyasema leo Jumamosi Oktoba 4, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Kigunda, Jimbo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
“Wananchi mkinichagua wanawake ambao hawana waume nitawaozesha wote na watu wenye mahitaji maalumu ili wawe na utulivu,” amesema Hamad.
Pia, amesema watu wenye mahitaji maalumu atawewekea bajeti yao kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi na kujiendeleza kimaisha kwani wanapitia changamoto mbalimbali kutokana na hali yao.
Amesema, katika Serikali yake itapambania kuwapa wanaume, wanawake wa kuoa kwa lengo la kuondosha uhalifu ndani ya jamii kwa sababu vijana wanajiingiza katika makundi hayo kutafutia chakula familia zao.
“Huwezi kuondoa umasikini bila ya kuwa na elimu bora ndio maana wanahitaji kuwatengeneza walimu mazingira mazuri ya kutoa elimu itakayokidhi haja kwa wananchi na wanafunzi wafanye kazi za staha baada ya kumaliza vyuo vikuu,” amesema.
Amesema hilo litawasaidia wananchi na vijana kuwa wabunifu na wenye uwezo wa kufanya tafiti juu ya kazi ambazo wanahitaji kuzifanya.
Hamad amefafanua kuwa, hakuna sababu ya wananchi wa Zanzibar kuwa na umasikini kutokana na rasilimali zilizopo nchini, lakini kukithiri kwa rushwa imechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa umasika.
Sambamba na hilo, amesema Serikali hiyo itazuia mfumuko wa bei kwa kuweka bei elekezi na sio wakati huu kila mmoja kuuza kwa mujibu anavyojipangia mwenyewe.
Naye, Mwenyekiti wa umoja wa wanawake ADC, Nadhera Haji amesema taifa lolote linahitaji vijana wenye uchungu wa taifa lao licha jimbo hilo kuwa na utalii lakini hawanufaiki nao ndio sababu ya kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo.
Naye, mgombea uwakilishi wa Jimbo hilo, Chumu Ali Makame amesema endapo atachagulia atahakikisha walimu wa madrasa wanalipwa mshahara kama ilivyo kwa walimu wa shuleni.
Pia, amesema atanunua gari maalumu ili lichukue wanafunzi kuwapeleka shuleni na kuwarudisha nyumbani.