KUNA mambo ya haraka anayopaswa kuanza nayo Dimitar Pantev ndani ya Simba baada ya kutambulishwa kuwa meneja mkuu. Ujio wa raia wa Bulgaria ni baada ya kuondoka kwa Fadlu Davids aliyekuwa kocha mkuu.
Pantev aliyetua nchini leo Jumamosi akiwa na msaidizi wake wakitokea Botswana alikokuwa akiifundisha Gaborone United, kuna mtihani mkubwa anakabiliana nao Simba, huku suala la nidhamu ndani na nje ya uwanja likidaiwa kuwa la kwanza la kufanyia kazi.
Nidhamu hiyo inahusu mbinu za uchezaji ambapo timu ya ushindi lazima imuheshimu mpinzani, lakini pia matendo ya wachezaji. Mbali na nidhamu, Simba inakabiliwa na mechi mbili za hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs ambapo mshindi anafuzu hatua ya makundi.
Mechi ya kwanza Simba inaanzia ugenini Oktoba 18 kisha marudiano Oktoba 25 jijini Dar es Salaam.
Katika kuiandaa timu, Simba inaingia kambini kesho Jumatatu huku ikiwa haina baadhi ya wachezaji kutokana na kwenda kuzitumikia timu zao za taifa.

Wakati inaingia kambini haitakuwa na wachezaji takriban saba ambao asilimia kubwa wanaunda kikosi cha kwanza. Wachezaji hao ni Yakoub Suleiman, Wilson Nangu, Yusuph Kagoma, Seleman Mwalimu na Morice Abraham walioitwa kuitumikia Taifa Stars, Steven Mukwala (Uganda) na Moussa Camara (Guinea).
Kalenda ya Fifa inatamatika Oktoba 14 ikiwa ni siku nne kabla ya Simba kucheza Nsingizini Hotspurs huko Eswatini.
Kutokana na hilo, benchi la ufundi la Simba akiwemo Pantev na wasaidizi wake kama Seleman Matola lina kazi ya kufanya kwenye maandalizi kuwakabili Nsingizini.
Baada ya Pantev kutua mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar siku moja tangu atambulishwe ameahidi kutengeneza timu ya ushindani itakayocheza soka safi na la kuvutia. “Ni mapema sana kuahidi chochote, ila ninachoweza kuwaambia mashabiki watarajie aina nzuri ya uchezaji kwa sababu ndio kitu muhimu kwetu na wenzangu,” amesema Pantev.
Kocha huyo amesema sababu kubwa iliyomshawishi kujiunga na Simba ni kutokana na ukubwa wa timu na mipango endelevu ya kikosi. “Nilikuwa na ofa nyingi, lakini baada ya Simba kuonyesha uhitaji na kunielezea mipango yao kiukweli nilishawishika na kuomba waajiri wangu Gaborone United kuniruhusu na nawashukuru kwa kuelewa mahitaji yangu,” amesema.

Baada ya sintofahamu kuhusiana na Pantev kutokidhi vigezo vya kusimama kama kocha mkuu wa benchi la ufundi, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kilichofanyika ni kubadili muundo wa timu hiyo.
“Kumuita Pantev meneja maana yake sisi tumebadilisha muundo wetu. Kwa maana yeye ndiye atakayesimamia uendeshaji mzima wa kikosi hicho.
“Pantev atahusika na mapendekezo ya mchezaji gani asajiliwe, wa kuachwa, wa kutolewa kwa mkopo, kufuatilia kiwango cha mchezaji mmoja mmoja na tathmini ya ujumla ya kikosi ndio maana tukampa cheo hicho ili isiwe ndani ya uwanja tu, bali shughuli zote ahusike mwenyewe,” amesema Ally.
Sababu za kuzuka kwa mjadala huo ni kutokana na kocha huyo kuwa na Leseni ya UEFA A tofauti na inayotakiwa ya UEFA Pro kwa ajili ya kuiongoza timu kama kocha mkuu kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa yaliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Kutokuwa na Leseni ya UEFA Pro kunamfanya Pantev kupoteza sifa hiyo.

Simba ni timu ya tano kufundishwa na Pantev barani Afrika kabla ya hapo amezinoa Victoria United ya Cameroon, Johansen ya Sierra Leone, Orapa na Gaborone United za Botswana akiwa ameitumikia kwa siku 254 tangu alipojiunga nayo Januari 23, mwaka huu huku akiipa ubingwa wa Ligi ya Botswana msimu uliopita.
Wakati mashabiki wa Simba wakimsubiri Pantev atue, walipata habari za skauti wa klabu hiyo, Mels Daalder, raia wa Uholanzi kujiuzulu.
Daalder ambaye alitambulishwa Simba Mei 25, 2023 kwamba ni skauti wa klabu alijiuzulu huku akitoa sababu kupitia akaunti yake ya Instagram akiandika: “Nimeamua kujiuzulu nafasi yangu kama mkuu wa skauti ndani ya Simba SC kwa vile sitambui tena mwelekeo wa klabu.
“Katika safari hii nzima nimekumbana na changamoto nyingi lakini nyakati hizo zote zimenijenga na kufanya mafanikio kuwa ya maana. Jambo muhimu zaidi lilikuwa kufikia fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF msimu wa 2024/2025 kumbukumbu ambayo nitatunza daima.

“Napenda kumshukuru kwa dhati rais wa klabu, Mohamed Dewji, aliyekuwa kocha mkuu Fadlu Davids na wafanyakazi wake kwa uaminifu na ushirikiano mkubwa. Zaidi ya yote, shukrani zangu ziwaendee mashabiki, damu ya klabu hii kwa mapenzi yao na usaidizi usioyumbayumba.
“Ninaacha jukumu langu, lakini sio kwa upendo wangu. Nitaunganishwa na Simba kama shabiki, na ninatazamia siku zijazo katika soka.”
Alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia kwa kina ishu hiyo, Daalder amesema mabadiliko ya uwajibikaji ndani ya klabu hiyo kwenye majukumu ndio yaliyosababisha kuchukua uamuzi huo.
Daadler amesema hakufurahishwa na uamuzi wa uongozi wa Simba kumchukua Pantev ambaye haamini kuwa ni kocha sahihi kuifundisha timu hiyo. “Kuna mambo yamebadilika ndani ya klabu yetu ambayo nimepima na kuona ni vyema nikajiweka pembeni ili kuacha taratibu zingine ziendelee.

“Unajua skauti nimefanya kazi vizuri na uongozi uliopita kuanzia Mohammed Dewji baadaye Salim (Mhene) na baadaye Mohammed anarudi tena wote hawa tulifanya kazi kwa kushirikishina mambo mengi.
“Nimeshirikiana vizuri sana na kocha Fadlu Davids. Nilishtuka alipotaka kuondoka lakini baadaye nilielewa ni kocha ambaye ana leseni kubwa UEFA Pro. Wakati huu nikashangaa sana tunakwenda kuchukua kocha ambaye sioni kama anastahili kuwa kwenye klabu yetu kubwa kama Simba kulingana na wasifu wake lakini pia hatujashirikishana,” amesema Daalder alipozungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu akiwa kwao Uholanzi.
Daadler amesema haoni kama kigezo cha Pantev kuisumbua Simba kwenye mchezo wa pili wa mtoano ni sababu ya kumchukua. “Inawezekana Gaborone walicheza vizuri, lakini nadhani watu wanashindwa kuelewa Simba ndio ilicheza vibaya. Kama Simba ingecheza vizuri hata kwa asilimia 75 tungewafunga nyingi Gaborone.
“Kulikuwa na nafasi ya kuchukua makocha wengine wenye vigezo na ubora wa kuifundisha Simba, lakini huyu tuliyemchukua namheshimu lakini sidhani kama ni chaguo sahihi kwa klabu kama hii.”