Bado Watatu – 49 | Mwanaspoti

AKAMUULIZA; “Ndiyo ukapanga kuwanyonga wewe?”
“Ndiyo.”
“Unaweza kudhani ulifanya uamuzi wa maana, lakini ungekuwa na maana kama ungekuja kuiarifu polisi. Kwa kuchukua sheria mkononi mwako umetenda kosa ambalo linaweza kuyagharimu maisha yako.”
“Kwa mtu ambaye amejitokeza mwenyewe polisi ujue alishakubaliana na lolote. Kama nimeweza kulipa kisasi kwa wale watu, mtakachoniamulia nyinyi polisi, niamulieni!”
“Uko tayari kwenda kujibu mashtaka mahakamani?”
“Kama ambavyo nilikuwa tayari kujitokeza polisi mimi mwenyewe, niko tayari pia kujibu mashtaka hayo mahakamani.”
Wakati naendelea kuzungumza na kijana huyo, afisa upelelezi akausukuma mlango wa ofisi na kuingia.
“Ondoka umpishe afande,” nikamwambia yule kijana aondoke kwenye kiti.
Alipoondoka, nikamwambia afisa upelelezi:
“Karibu kiti afande.”
Kabla ya kukaa, afisa huyo alimtazama yule kijana na kuniuliza:
“Kijana mwenyewe ndiye huyu?”
“Ndiye huyo afande.”
“Mbona haelekei?”
“Ni kweli, lakini kaa, atakueleza mwenyewe.”
Afisa upelelezi akakaa kwenye kiti.
“Kijana mwenyewe ndiye huyo. Amenipigia simu dakika chache zilizopita akaniambia anataka kuniona nikamwambia aje. Alipokuja akanieleza yeye ndiye aliyewanyonga kina Unyeke.”
Afisa upelelezi akamtazama kijana huyo kwa mshangao.
“Hebu eleza wewe kijana, nini kilitokea?”
“Kilichotokea ni kwamba…”
“Acha kueleza ukiwa wima, kaa chini!”
“Sawa.”
Kijana akakaa chini.
“Sasa eleza nini kilitokea? Kwanza unaitwa nani?”
“Naitwa Faustin Ojuku.”
“Sasa eleza huo mkasa.”
“Kwa kifupi mimi ndiye niliyewaua wale watu wanne mliowakuta wamenyongwa.”
Afisa upelelezi alimtazama vizuri kijana huyo kisha akamuuliza.
“Hao watu unaowazungumzia wewe ni kina nani?”
“Sijazingatia majina yao lakini ni familia ya Unyeke.”
“Wewe ndio uliwanyonga?”
“Ndiyo.”
“Kwa nini?”
“Wale walikuwa wamehukumiwa kunyongwa na mahakama kwa kosa la mauaji lakini walitoroshwa jela ili kuepushwa na adhabu ya kifo.”
Afisa upelelezi aliendelea kumtazama yule kijana wakati anazungumza. Alipomaliza kueleza akamuuliza tena.
“Kama kweli wewe ndiye uliyewanyonga ilikupasaje kuchukua jukumu hilo?”
“Ni kwa sababu kile kitendo cha kutoroshwa kwao kilinikasirisha. Yule kijana waliyemuua alikuwa ni ndugu yangu.”
“Muelezee historia nzima kama ulivyonieleza mimi,” nikamwambia yule kijana.
Kijana huyo akamueleza kisa kizima kilivyotokea hadi akachukua uamuzi wa kuwanyongwa watu hao.
“Unahisi kwamba una akili timamu?” afisa upelelezi akamuuliza.
“Sina shaka yoyote. Ningekuwa na tatizo la akili nisingefika kidato cha sita.”
“Umesoma hadi kidato cha sita?”
“Ndiyo.”
“Mama yako yuko wapi?”
“Yuko Lindi.”
“Hapa Tanga uko na nani?”
“Niko peke yangu. Aliyekuwa ndugu yangu ndiye huyo aliyeuawa.”
“Una maana kwamba uliweza kuwanyonga wale watu wewe mwenyewe bila msaada wa mtu mwingine?”
“Sikusaidiwa na mtu yeyote.”
“Ulitumia mbinu gani?”
“Mpango wa kuwanyonga niliupanga kwa miezi mitatu. Nilizingatia kutogundulika na kukamatwa kabla sijamaliza kuwanyonga watu wote wanne na pia nilizingatia ni jinsi gani ningeweza kuwazungusha nyinyi polisi.”
“Na ni kweli ulituzungusha. Kwa mpango wako huo ninakupongeza lakini ujue kuwa japokuwa ulikuwa unalipa  kisasi cha ndugu yako lakini utakutana na mkono wa sheria.”
“Sioni kama mimi ni mhalifu.”
“Kuua ni uhalifu.”
“Kutekeleza amri ya mahakama kuwa watu wale wanyongwe ni uhalifu?”
“Amri ya mahakama haikuwa juu yako wewe.”
“Yule ambaye ilikuwa ni juu yake kuitekeleza lakini akashindwa kuitekeleza na badala yake nikaitekeleza mimi bado kutakuwa na kosa?”
“Kutakuwa na kosa. Wewe ulipaswa kuiarifu polisi kuwa wale watu waliohukumiwa kunyongwa wametoroshwa. Sisi polisi tungewakamata na kuwapeleka mahakamani.”
“Watu wameshahukumiwa kunyongwa unawapeleka mahakamani wakafanywe nini?”
Afisa upelelezi akanitazama na kutoa kicheko kidogo.
“Tutamuandalia mashitaka na kumfikisha mahakamani,” akaniambia kisha akamtazama kijana huyo.
“Tunakushukuru kwa kutupunguzia kazi ya kukutafuta.”
Kijana huyo hakusema kitu. Aliinamisha kichwa chake chini kama aliyekuwa akiwaza.
Baada ya sekunde chache aliuinua uso wake na kutuambia.
“Naomba niwape namba ya mzazi wangu ili mufahamishe kama niko hapa polisi.”
“Tupatie hiyo namba. Tunahitaji kuzungumza na huyo mzazi wako,” nikamwambia.
Kijana huyo alikuwa akitaja namba ya simu hiyo nikamwambia.
“Nipatie simu yako.”
Akasimama na kuitoa simu yake mfukoni akaiweka juu ya meza kisha akarudi kukaa.
Niliichukua ile simu na kumwambia anitajie tena namba ya mzazi wake.
Aliponitajia namba hiyo niliipiga kwenye simu ile ile aliyonipa likatokea jina la Mom.
“Huyu ni mama yako siyo…?” nikamuuliza.
“Ndiyo ni mama yangu”
“Ambaye umesema yuko Lindi?”
“Ndiyo.”
Simu iliita kwa sekunde kadhaa kabla ya  kupokelewa na sauti ya mwanamke ikasikika.
“Hello…Faustin, hujambo mwanangu?”
“Sijambo ingawa siye Faustin. Unazungumza na mtu mwingine.”
“Nani mwenzangu? Hii ni namba ya mwanangu Faustin.”
“Ndiyo ni simu ya mwanao. Hapa ni kituo cha polisi jijini Tanga. Ninapenda kukujulisha kwamba mwanao tuko naye hapa.”
“Amefanya nini?” Sauti ya mwanamke huyo sasa ilikuwa imetaharuki.
“Kwanza ninataka utuhakikishie kama huyu ni mwanao kweli?’
“Ndiyo ni mwanangu. Alikuja Tanga kwa ajili ya kutafuta kazi.”
“Hebu tueleze kama ni kweli ulikuwa na kaka yako aliyekuwa akitwa Christopher.”
“Ni kweli lakini alishafariki dunia huko huko Tanga.”
“Hebu nieleze historia yenu.”
“”Yeye alikuja huko Tanga tangu akiwa mdogo sana. Tulisikia kwamba alioa huko akazaa mtoto mmoja anayetwa Thomas lakini huyo kaka  alipata maradhi akafariki.”
Na nini kilitokea kwa huyo mtoto wake?”
“Tulisikia kwamba aliuawa.”
“Aliuawa  na nani na kwa sababu gani?”
“Mimi na mwanangu huyo tulikuja huko Tanga tukaelezwa hadithi ndefu. Tuliambiwa kwamba huyo kaka kabla ya kufa alimuachia rafiki yake anayeitwa Unyeke mali yake pamoja na mtoto wake ambaye wakati huo alikuwa mdogo…”
“Ndiyo.”
“Inasemekana kaka alimwambia rafiki yake huyo kwamba pindi atakapokufa atamiliki mali zake pamoja na kumlea mtoto wake hadi atakapofika umri wa miaka kumi na minane amrithishe zile mali.
“Kaka alipokufa Unyeke akamlea yule mtoto pamoja na kumiliki mali ya marehemu. Lakini yule mtoto alipofikia umri wa kurithi mali ya marehemu baba yake ambaye ni kaka yangu, Unyeke aliwaeleza watoto wake kwamba Thomas ndiye atarithi ile mali kwa sababu ni ya marehemu baba yake. Watoto hao ambao walikuwa wakubwa kuliko Thomas walipojua kwamba hawatapata kitu wakapanga njama za kumuua ili ile mali ibaki mikononi mwao.
“Baada ya kumuua walimzika bila baba yao kujua. Sasa Thomas akawa haonekani. Habari zikafika polisi. Katika uchunguzi wa kumtafuta, mfanyakazi wa ndani aliwambia polisi kwamba siku ya mwisho ambayo alitokweka, Thomas aliondoka akiwa na watoto wa Unyeke na kutoka siku hiyo hakuonekana tena.
“Polisi wakaanza kuwahoji watoto wa Unyeke ili kupata ukweli huku wengine wakianza kukimbia. Baada ya mtoto mmojawapo kubanwa na polisi akasema kwamba walimuua walipokwenda shamba na aliwapeleka polisi kuwaonesha mahali walipomzika.
“Wale vijana walishitakiwa mahakamani na walihukumiwa kunyongwa. Sisi tulipofika Tanga na kujitambulisha tulikataliwa tukaambiwa kwamba Thomas hakuwa na ndugu na ndiyo maana mali yake na mtoto wake vilichukuliwa na rafiki yake Unyeke ambaye muda huo naye alikuwa ameshakufa. Ikabidi turudi lakini baadaye mwanangu alikuja tena huko Tanga kutafuta kazi.”
Baada ya kufika hapo nikamuuliza swali la kumtega.
“Umeniambia kwamba wale vijana waliomuua Thomas walihukumiwa kunyongwa. Je walinyongwa au ilikuwaje?”
“Sasa hapo sijui kama walinyongwa au bado.”
“Kuna taarifa kwamba walitoroshwa jela. Wewe hukupata taarifa hizo?”
“Taarifa hizo sikuzipata.”
“Sasa ninakupa picha ya makosa ya kijana wako Faustin. Wale wafungwa waliomuua Thomas walitoroshwa jela na wakawa wanaishi kama watu wengine. Katika kipindi ambacho Faustin yuko hapa Tanga alikuja kugundua kuwa wafungwa hao wametoroshwa. Umenielewa?”
“Ninakuelewa.”
“Sasa kosa la Faustin ni kwamba badala ya yeye kwenda polisi kutoa ripoti kwamba wale watu waliomuua Thomas wametoroshwa jela, yeye aliamua kuwatafuta yeye mwenyewe na kuanza kuwanyonga mmoja mmoja. Baada ya kuwamaliza wote amejileta yeye mwenyewe polisi na kutuambia kuwa yeye ndiye aliyewanyonga watu hao, kwa hiyo sheria ifuate mkondo wake.”
“Eh! Mwanagu Faustin ameweza kufanya hivyo? Faustin ni mdogo sana!” Sauti ya mama wa Faustin ikasikika ghafla.
“Yeye mwenyewe ndio ametuthibitishia kuwa ndiye aliyewanyonga na alijileta polisi yeye mwenyewe na tuko naye hapa. Tunaweza kumpa simu uongee naye.”
“Hebu mpe nimsikilize.”
Niliweka spika ya kusikika kwenye simu kisha nikampa simu Faustin.
“Ongea na mama yako,” nikamwambia.