Wanandoa msibague watoto wenu kwa jinsi

Canada. Kuna makabila yenye mazoea na mila za ovyo. Mila za makabila haya zimejengwa kwenye ubaguzi wa kijinsi ambao unaweza kuakisi namna jinsi inavyochukuliwa, kuthaminiwa hata kutothaminiwa katika jamii na mila za Kiafrika.

Kwa makabila haya mama asipozaa watoto wa kiume, kunakuwa na tatizo. Inapotokea hivyo, ndugu wa mume humuolea ndugu yao mke ili aweze kupata watoto wa kiume. Katika kufanya hivi, haijalishi nani ni baba wa watoto hawa isipokuwa uwepo wao.

Moja ya visingizio vya makabila haya ni kuwa mtoto amezaliwa kwenye mahari ya fulani, wakimaanisha mahari yaliyotolewa kwa wazazi wa mke.

Hivyo, hata ikibidi mama kutoka nje ya ndoa na kupata watoto wa kiume wasio wa mumewe, hakuna shida. Tukijiuliza, mosi, hii ni nini kama siyo ubaguzi wa kijinsia? Pili, je, watoto wapatikanao kupitia mila hii kweli ni wa baba anayewakubali ilimradi wanachangia kwenye ukoo wake? Je, hakuna njia nyingine ya kukabili ‘tatizo’ hili japo si tatizo?

Kwa kuangalia kisa hicho hapo juu, kuna ubaguzi wa kijinsia wa wazi katika jamii husika. Isitoshe, ubaguzi huu umefichwa kwenye kisingizio cha mila za kizamani zisizo na nafasi katika jamii ya sasa.

Swali hili halina jibu rahisi wala moja. Kwanza, inakuwaje binadamu, pamoja na ubinafsi wake, kukubali watoto wasio wake kwa kisingizio cha mila? Ni wangapi wameathiriwa na mila hii?

Wakati wahusika wakishabikia na kuridhika na mila hii, wajiulize kusingekuwako na watoto wa kike, dunia yetu ingekuwaje? Je, kuna mtu anayeandika barua ya maombi kwa Mungu azaliwe kama alivyo?

Katika kudurusu na kujadili kadhia hii, kwanza, tunagundua kuwa sababu ya ubaguzi huu wa kijinsia ni uelewa mdogo wa masuala ya uzazi.

Kisayansi, anayesababisha jinsi ya mtoto si mama, bali  baba ingawa anayeadhibiwa na kuathiwa nayo ni mama na watoto wa kike. Kama ni adhabu, aliyepaswa kuadhibiwa si mama bali baba.

Pili, tunadhani kuwa, licha ya ujinga, kuna kila dalili za wahusika kupenda mitala kwa kisingizio cha jinsi. Je, wakijua kuwa anayesababisha jinsi zote mbili ni baba, wataendelea na imani hii potofu na kuwaumiza kina mama na watoto? Kwetu sisi, mtoto ni mtoto bila kujali jinsi yake.

Tutatoa kisa kimoja ambapo baba alimtelekeza mkewe na watoto wake wa kiume na kwenda kutafuta mke mwingine aliyemzalia watoto wa kiume naye akaridhika asijue Mungu ana mipango mingine.

 Huyu bwana, pamoja na kuridhika, watoto walipokua, alijilaumu asijue la kufanya kwa sababu maji yalikuwa yameshamwagika.

Katika makuzi yao, watoto wa kike walibahatika kuwa na uwezo mkubwa darasani. Zaidi, waliolewa na waume wanaojiweza kinyume na kaka zao ambao wengi waliishia kuwa watu tegemezi kutokana na kutojiweza kiakili.

Miaka ilienda. Baadhi ya watoto wa kiume walijiingiza kwenye jinai na wengine wao kuishia gerezani. Kwa upande wa watoto wa kike, mambo yaliwanyookea. Akiwa amestaafu na nguvu zimemuishia, baba alijikuta akijipeleka kwa watoto aliowatelekeza akiomba wamtunze. Yaliyofuata ni historia.

 Kisa hiki kinatufundisha nini? Funzo la kwanza ni kwamba watoto wote ni sawa. Pili, tusiwabague watoto kijinsi.

Tatu, umdhaniaye ndiye siye. Nne, majuto ni mjukuu. Wewe ni nani hadi umhukumu kiumbe wa Mwenye Mungu kwa jinsi yake wakati ya kesho hayajulikani? Je, ungekuwa wewe ungetaka utendewe vipi?

Suluhisho la tatizo hili ni kwa jamii na wana jamii kwa ujumla kujielimisha juu ya sayansi ya uzazi. Pili, ni kuacha mila chakavu, kongwe, potofu, na za ovyo. Tatu, wakati wakiwabugua watoto kijinsi, wawakumbuke ambao hawakujaaliwa kupata mtoto hata mmoja.

Nne, waathirika  wa tatizo hili walione na kulitumia kama nyenzo ya kujikomboa kijamii na kijinsia. Tano, wahusika wajue kuwa watoto waliozaliwa na baba wengine wakawalea wakijua ukweli, wanaweza kuwaadhibu wazazi bila hata ya wao kujua.

Hivi, unajisikiaje kuwa baba yako ni yule baba jirani tajiri wakati baba yako feki ni maskini wa kutupwa? Sita, kinamama na baba wakatae mila hii kwa vile inawafanya walee au wasipate fursa ya kuwalea watoto wao.

Tumalizie. Kujua wazazi wa mtu ni haki  ya msingi na amkoseshaye au kumnyima haki hii mhusika, anamuumiza kisaikolojia, kijamii na hata kiuchumi.