Junguni yaeleza sababu za kufika uwanjani bila jezi

SIKU chache baada ya Bodi ya Ligi Zanzibar kuitoza faini timu ya Junguni kwa kufika uwanjani bila ya kuvaa jezi, uongozi wa timu hiyo umetaja sababu ya jambo hilo kutokea.

Tukio hilo, lilitokea katika mechi iliyopangwa kuchezwa Septemba 26, 2025 kati ya Junguni na Zimamoto kwenye Uwanja wa Gombani uliopo kisiwani Pemba saa 10:00 jioni.

Kufuatia Junguni kufika uwanjani hapo bila ya jezi, mechi hiyo ilivunjika na Zimamoto kupewa pointi tatu na mabao mawili, huku Junguni ikitozwa faini ya Sh200,000 na kuhesabika imepoteza mechi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Junguni, Shariff Omar Ramadhan amesema walifika uwanjani hapo mapema wakisubiria jezi zao zifike ili wacheze mechi.

Amesema, baada ya jezi hizo kuchelewa kufika kutokea Uwanja wa Ndege wa Pemba, uongozi ulimpa taarifa kamisaa wa mechi uwepo wa changamoto hiyo, ndipo kamisaa alipokutana na waamuzi wa kwa ajili ya kufanya uamuzi.

“Kabla ya kamisaa na waamuzi kuvunja mechi, jezi zilikwishafika na wachezaji walikuwa tayari wamevaa kwa ajili ya kucheza,” amesema.

Meneja huyo amesema uamuzi huo umeleta athari katika timu hiyo kwa sababu ilikuwa na uhakika wa kuvuna alama tatu katika mechi hiyo ya kwanza ya msimu.

Mbali na hilo, timu hiyo imeridhika na uamuzi huo na itajiandaa kwa michezo ijayo kwa kuhakikisha hairudii makosa.

Aidha, meneja huyo amesema mambo yote hayo yanayojitokeza ni kwa sababu hawana mdhamini wa timu, hivyo ametoa wito wajitokeze ili wafanye vizuri zaidi katika Ligi Kuu Zanzibar.

Katika uamuzi wa Bodi ya Ligi Kuu Zanzibar uliotolewa Oktoba 2, 2025, umebainisha kwamba, kwa mujibu wa ripoti ya kamisaa wa mechi hiyo, Junguni ilifika uwanjani ikiwa haina jezi, ambapo waamuzi waliwasubiri kutoka saa 10:00 jioni hadi saa 10:35 jioni hakukuwa na mabadiliko yoyote, wakalazimika kuvunja mechi.