Kama kuna kitu huwa kinanisumbua kukielewa ni hizi zinazoitwa mila potofu. Hivi ukisema mila potofu unakuwa na maana gani?
Natambua kuwa kuna baadhi ya mambo yalifanywa na wazee waliotutangulia na huenda yakawa na changamoto ukiyatazama kwa jicho la ‘sisi tulioelimika’.
Hata hivyo, najaribu kujenga hoja kuwa mengi tunayoyatupa ni vile hatujataka tu kuyaelewa. Tumetumia miwani ya tamaduni nyingine na kukimbilia kuziita mila na desturi zetu kuwa ni ‘potofu’ au ‘mila zilizopitwa na wakati’ na kwa vile hatujajisumbua kuzielewa. Nitatoa mifano michache ya mila katika muktadha wa familia kutufikirisha pamoja.
Tuanze na mila ya namna ya kuanzisha uhusiano wa kimapenzi. Kama kuna jambo halikuchukuliwa kijuu juu katika jamii zetu ni ndoa. Ndoa halikuwa jambo binafsi la watu wawili.
Ndoa ulikuwa ni mchakato mrefu wa kuunganisha koo mbili kwa utaratibu unaohusisha wazee na watu wengine wenye hakima katika jamiii.
Tendo la kuchumbia, kwa mfano, liliwekewa miiko yake kudumisha adabu na nidhamu kabla vijana wawili hawajaanza kuishi pamoja. Mshenga haikuwa fasheni tu ya kurasimisha vitu vilivyokamilishwa siku nyingi kisirisiri. Mshenga alikuwa msimamizi wa nidhamu ya vijana wanaotafuta ridhaa ya familia zao kuingia kwenye ndoa.
Mchakato wa uchumba ulitanguliwa na ‘ushushushu’ wa kuchunguza kwa kina familia na ukoo wa pande mbili. Lengo lilikuwa kujua tabia, sifa na hulka nyingine zinazoweza kuathiri uhusiano wa familia hizo mbili.
Ikiwa kulipatikana taarifa zenye utata wa kuwepo tabia fulani fulani mbaya zenye madhara, mpango wote uliishia hapo na wahusika hawakulazimisha.
Hili la kusikiliza wazee ukiwaambia vijana wa siku hizi watakuambia, “Unaishi dunia ya wapi wewe?” Hapo ndipo unapoona nafasi ya jando na unyago.
Usipopitia mtalaa wa jamii yako, ukafuzu, hakuna mtu alikukabidhi majukumu ya heshima. Somo la wazee wameona mengi, sikiliza wazee, wazee wanajua usiyoyajua, liliwaepusha vijana na mengi.
Tuje kwenye mahari. Kijana alilazimika kulipa mahari kama alama ya shukrani inayotambua kazi iliyofanywa na familia iliyomlea mke wake. Ndio maana, katika jamii nyingi, kwa mfano, mahari ilikuwa vitu vinavyogawanywa kwa wazee, mashangazi na wengine.
Kulipwa kwa mahari kulimaanisha binti anahama na kuungana rasmi na ukoo wa kijana wa kiume atakayeongoza familia yake. Unahama kwenda kubeba wajibu wa kuanzisha familia yako ikiwa ndani ya ukoo wa mwanamume.
Sijui wanaofikiri lengo lilikuwa ni kutweza utu wa mwanamke na kumtumia kama chanzo cha kipato wanatumia kigezo gani?
Ukiingia kwenye ndoa ilifahamika nani ni nani. Hapakuwepo, kwa mfano, utata wa majukumu. Mlinzi wa familia, mwenye wajibu wa kuhakikisha wanafamilia wanalala usingizi wa pono alifahamika.
Nani anaenda kuchunga mifugo, nani anabaki nyumbani kulea watoto, wala halikuwa suala la mjadala. Mgawanyo huu wa majukumu ulikuwa na maana yake na uliondoa uwezekano wa migogoro inayotokana na mashindano ya nani ni nani.
Siku hizi watu wanaongelea sana haki za mtu mmoja moja. Kwamba ‘kama mimi nimetaka kutembea uchi barabarani nani wa kunipangia maisha?” Tumeanza kufikiri mtu mmoja anaweza kuwa haki ya kufanya apendavyo bila kuingiliwa na jamii. Sehemu ya matatizo mengi tuliyonayo yanaanzia hapa.
Ukichungua katika jamii zetu, haki za wengi zinaweka msingi wa haki za mtu mmoja moja. Ukitembea uchi barabarani, wenzio wa jinsi yako watakuchukulia hatua. Huwezi kutembea uchi na watu wakajifanya hawaoni aibu unayowasababishia kama jamii.
Hata kwenye ndoa, mambo mengi yalimalizwa kwa kutumia kanuni hiyo. Uhuru wa mtu binafsi haukutangulia maslahi ya familia, ukoo na jamii tofauti na ilivyo siku hizi. Bibi zetu sio kwamba hawakukutana na mambo magumu.
Ukiwa umeathiriwa na tamaduni za wengine, rahisi kuwahurumia na kuwaona kama wanyonge walionyanyasika. Ukizungumza na hawa kina bibi unaona kabisa uvumilivu wao ulijengwa kwenye misingi ya kutanguliza ustawi wa familia.
Utatuzi wa migogoro na makosa uliratibiwa na mifumo ya utoaji haki iliyolenga kumkumbusha mkosaji haja ya kurejea katika jamii yake. Tofauti na mifumo ya sheria za kimagharibi, jamii zetu zililenga kuponya zaidi uhusiano kuliko kuumiza.
Dhana hii ya kutoa adhabu zinazokarabati tabia na kujenga familia ndizo zinazochangia tabia tunayoisikia ya watu kusuluhisha makosa nje ya mahakama.
Namna gani tunaweza kuifanya sheria iakisi imani kuwa hakuna kosa lisilo na ufumbuzi unaojenga hilo ni swali kwa wanasheria.
Pamoja na utandawazi kuondoa mipaka ya utamaduni na kutukutanisha na kila aina ya tamaduni na mila mbalimbali duniani, bado ipo haja ya kukumbushana kutunza tamaduni na mila zetu.
Nyakati zinabadilika, ni kweli, na haja ya kuzipitia upya mila zetu ipo lakini kuuita utambulisho wetu kuwa ni “mila potofu” ni matusi tunayojitukana kwa kukumbatia elimu zisizoendana na maisha yetu.