Moto Kariakoo waibua hoja ya vifaa, mfumo wa umeme

Dar es Salaam. Stoo ya kuhifadhia manukato (pafyumu) iliyoko katika ghorofa la mitaa ya Msimbazi na Mkunguni, Kariakoo, iliteketea kwa moto usiku wa kuamkia Oktoba 4, 2025, chanzo kikiwa bado hakijajulikana.

Hilo limetokea ikiwa ni siku 13 tangu stoo nyingine ya kuhifadhia mizigo vikiwamo viatu kuungua katika Mtaa wa Narung’ombe, Kariakoo ambayo chanzo chake hakikujulikana, huku uchunguzi ukiendelea.

Tukio hilo limeongeza idadi ya majengo yaliyoungua kufikia manne kwa miezi mitatu, huku Agosti pekee yakiungua mawili ndani ya wiki mbili.

Mbali ya matukio hayo, inaelezwa yapo mengine ambayo hudhibitiwa mapema na wafanyabiashara kabla hayajaleta madhara.

Mwenendo huu wa matukio ya moto Kariakoo unaibua mjadala kuhusu ujenzi hasa unaohusisha mfumo wa umeme.

Katika mjadala huo, kunaibuliwa hoja ya baadhi ya watu kubana matumizi katika ujenzi wa mfumo wa umeme, ikiwamo utandazaji wa nyaya na ununuzi wa vifaa.

Hali hiyo inaelezwa haijitokezi katika ujenzi wa majengo mapya pekee, bali hata yanapobadilishwa matumizi yale ya zamani, kwa mfano kutoka makazi kwenda ofisi au biashara licha ya matumizi kuongezeka, miundombinu ya umeme hubaki ileile ya awali, hivyo kuelemewa.

Hoja nyingine ni matumizi ya mafundi wasio na viwango ili kukwepa gharama.

Haya ya kutozingatiwa viwango vya kitaalamu wakati wa kutandaza nyaya, ununuzi wa vifaa visivyo na kiwango na kutumia mafundi wasioidhinishwa na mamlaka husika kufanya kazi, yanatajwa huenda yakawa chanzo cha majanga hayo ya moto.

Mfanyabiashara wa nguo katika Mtaa wa Aggrey na Congo, Ashura Mohamed anasema yapo matukio ambayo taarifa zake hazitolewi kwa kuwa hudhibitiwa mapema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Said Omary, anasema moto unaotokea katika majengo ya Kariakoo wakati mwingine huchangiwa na usimamizi mbovu wakati wa ufungaji umeme.

“Unakuta ujenzi wa mifumo ya umeme anaachiwa fundi kufanya kila kitu kwa kufuata vifaa dukani na wakati huo mmiliki amembana kwenye malipo. Hivyo, hununua vifaa hata kama vipo chini ya kiwango ambavyo haviwezi kuhimili jengo husika,” anasema.

Anasema wakati mwingine mafundi wanabanwa na kupewa maelekezo ya kwenda kwenye maduka ambayo mmiliki au msimamizi ana urafiki na mwenye duka, hata kama fundi anafahamu kuwa vifaa hivyo havina ubora sawa na kazi inayofanyika.

Omary anasema haiwezekani jengo lenye vyumba zaidi ya 400 likatumia mifumo kama ya nyumba ya vyumba vitatu, jambo analosema linatengeneza hatari na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara wasiokuwa na hatia.

Anaeleza hayo ni kutokana na kutokuwapo uwajibikaji kwa viongozi wanaosimamia ujenzi ili kuhakiki kila hatua inakuwa salama.

“Nakutana na kesi nyingi za malalamiko ya wafanyabiashara kuanzia masuala ya moto hadi mazingira, ninapochukua na kupeleka sehemu husika ni kama zinapuuzwa tunahitaji mamlaka iwajibike,” anasema.

Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Dar es Salaam, Peter Mabusi anasema  matukio ya moto katika ghorofa za Kariakoo yanasababishwa na mambo mbalimbali, ikiwamo matumizi mabaya ya umeme, kuunganishwa kwa umeme kiholela na mifumo ya umeme isiyo salama katika majengo ya zamani.

“Mengi ya matukio ya moto tuliyoyaona hivi karibuni yamechangiwa na kuunganishwa kwa umeme kiholela kutoka kwenye majengo makubwa hadi kwenye vibanda vidogo. Hii inasababisha mzigo mkubwa wa umeme na hatari ya moto kuwa kubwa zaidi,” anasema.

Mabusi anasema baadhi ya majengo ya Kariakoo ambayo awali yalikuwa makazi, sasa yamebadilishwa kuwa ya biashara, lakini mifumo ya umeme iliyopo bado ni ileile ya zamani.

“Wakati majengo haya yanapofanyiwa mabadiliko, mifumo ya umeme haibadilishwi, jambo linaloongeza hatari ya moto. Wateja wanaojiunganisha umeme kiholela, pamoja na matumizi mabaya ya vifaa vya kielektroniki, yanaongeza uwezekano wa ajali,” anasema.

Pia, anasema uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha baadhi ya matukio ya moto.

“Tunachunguza ghorofa zote zilizoathirika tukishirikiana na vyombo vya usalama na mamlaka nyingine, lengo letu ni kuhakikisha hatari kama hizi zinapunguzwa na usalama wa kila mtu unadumishwa,” anasema.

Anasema wamiliki wa majengo na wateja wa umeme, hasa wale wanaojiunganisha kiholela, wanapaswa kuchukua tahadhari na kuhakikisha kila kifaa kinachotumia nishati hiyo kipo salama ili kuzuia ajali za moto.

Mkandarasi, Salum Shaweji akizungumza na Mwananchi, Septemba 29, 2025 anasema changamoto wanayokumbana nayo ni maelekezo kutoka kwa wamiliki wa majengo ambao hulazimisha kupunguza gharama kwa kila hatua ya ujenzi.

Anasema wamiliki wanaposhikilia mtazamo huo, usalama wa majengo na watu wanaotumia huduma unakuwa hatarini.

Anaeleza, kuna wakati mmiliki anakuambia: “Weka hivi kwa sababu sina pesa kwa muda huu na natakiwa kufanya vitu vingine.”

“Tukipinga, wanatafuta mkandarasi mwingine anayekubali. Mwisho wa siku jengo linawekwa waya wa kiwango cha nyumba ya kawaida kwenye ghorofa la biashara lenye watu mamia kila siku.”

Anasema vifaa vya umeme vinavyohitajika kwa majengo ya ghorofa vinatakiwa kuzingatia uwezo wa kubeba mzigo wa umeme mkubwa wa matumizi ya mashine, majokofu, taa nyingi na vifaa vya kielektroniki vinavyotumika kwa biashara.

Hata hivyo, anasema baadhi ya wamiliki hukwepa gharama na kuamua kutumia vifaa vilivyokusudiwa kwa nyumba za kawaida za familia.

Shaweji anasema licha ya utandazaji wa nyaya za umeme, pia wapo wenye nyumba wanaofunga swichi, soketi na maboksi ya usambazaji wa umeme visivyohimili mtiririko wa umeme mkubwa, hivyo kuzidiwa nguvu, kulipuka au kusababisha moto.

Anasema changamoto nyingine ni usimamizi hafifu, hivyo baadhi ya wahandisi wa majengo hawafanyi ukaguzi wa kina, matokeo yake huidhinisha kazi pasipo kuhakikisha vifaa vilivyowekwa iwapo vinakidhi ubora unaohitajika.

Kwa upande wake, mhandisi wa umeme, Robert Njarita anasema wamiliki wa nyumba hufanya makosa ya kununua nyaya za umeme bila kuzingatia ubora au ushauri wa wataalamu, jambo linalosababisha matatizo yanayohusiana na moto na kuharibika kwa vifaa.

Anawashauri wamiliki wa nyumba, wateja na mafundi kuzingatia ubora na aina ya nyaya wanazonunua kabla ya kuzitumia kwenye miradi ya umeme ili kuepusha majanga kama moto na kuharibika kwa vifaa vitumiavyo nishati hiyo.

Njarita anasema: “Nyaya zina tofauti, kuna za shaba na kuna za aluminiamu au mchanganyiko. Kila moja ina uwezo wake wa kupitisha umeme. Ukichagua nyaya zisizo na ubora, zinaweza kushindwa kustahimili, joto likizidi au likipungua zaidi ya kiwango cha kiufundi.”

Anasema nyaya za umeme huwa na maelezo ya kiufundi (data sheet) yanayoonesha kiwango cha umeme kinachoweza kupita, matumizi yanayofaa (mfano taa, soketi au mashine kubwa) na aina ya nyenzo iliyotumika.

“Mara nyingi watu hununua nyaya bila kuangalia ‘data sheet’ hiyo, matokeo yake ni nyaya kuchomeka, vifaa kuharibika au hata moto. Lazima fundi na mteja wakague maelezo ya nyaya kabla ya kuzinunua,” anasema.

Njarita anasema nyaya pia hubadilika kulingana na matumizi ya taa, soketi na nyaya ndogo za ndani, hivyo mafundi hawapaswi kuchanganya bila kuzingatia kanuni za kiufundi.

Njarita anasema mafundi wasio na ujuzi wanaoweka nyaya bila kufuata viwango wanasababisha hatari kubwa.

“Unapojenga nyumba ya biashara au ghorofa, hakikisha unaajiri fundi mwenye usajili au anayesimamiwa na mhandisi mwenye taaluma. Si mtu yeyote anayejiita fundi. Ujuzi usio sahihi unaleta majanga makubwa,” anasema na kuongeza kuwa, ulinzi wa mifumo ya umeme ni jambo muhimu.

Hata hivyo, anasema vifaa vya bei rahisi, visivyo na ubora husababisha tatizo la kushindwa kulinda mifumo pale dharura inapotokea.

“Wengi wanakimbilia gharama ndogo bila kuangalia ubora mwisho wa siku vifaa vyao vinaharibika, moto unatokea au watu wanaumia. Ni bora kulipa zaidi lakini uwe salama,” anasema.

Anawashauri wamiliki wa majengo kushirikiana na wahandisi wenye utaalamu ili kila mfumo wa umeme uwe na michoro na maelezo sahihi kabla ya kutekelezwa.

Msimamizi wa majengo matatu yaliyopo Kariakoo, ambaye ameomba kutotajwa jina, anasema baadhi ya wakazi katika majengo mawili yaliyokamilika ujenzi hulalamika vifaa vyao vya umeme kuungua mara kwa mara.

“Wamiliki hawataki kutumia fedha kwenye masuala ya umeme, wapo tayari kubadilisha fundi au mtaalamu akiamini anaibiwa,” anasema.

Anasema gharama ndogo haipaswi kuwa sababu ya kupuuza usalama, kwani akiwa msimamizi wa ujenzi kazi yake ni kushauri lakini hawezi kubadilisha uamuzi wa mmiliki bila idhini yake.