Maana ya kiuchumi kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Tanzania

Dar es Salaam. Wakati Shilingi ya Tanzania ikiendelea kupanda thamani dhidi ya fedha za kigeni kila siku, wadau wameeleza faida na hasara wanazoweza kukutana nazo watu wanaouza bidhaa nje ya nchi.

Miongoni mwa faida walizozitaja ni kupungua kwa gharama za uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi ikiwemo mafuta, jambo ambalo litashusha gharama za uzalishaji bidhaa na hivyo kuleta ahueni kwa wananchi.

Maoni hayo yanatolewa ikiwa ni siku moja tangu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, kuwaambia waandishi wa habari kuwa thamani ya Shilingi ya Tanzania imeongezeka kwa asilimia 8.4 katika robo ya tatu ya mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 0.7 katika robo mwaka iliyotangulia.

Tutuba alitoa kauli hiyo alipokuwa akitangaza kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kitakachotumika katika robo ya nne ya mwaka 2025, baada ya Kamati ya Sera za Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania kufanya mapitio na kujiridhisha na uthabiti wa uchumi.

Taarifa ya BoT inaonesha kuwa Oktoba 4, 2025, Euro moja itanunuliwa kwa Sh2,844.31 na kuuzwa kwa Sh2,872.76, huku Dola moja ya Marekani ikinunuliwa kwa Sh2,436.03 na kuuzwa kwa Sh2,460.4.

Ikilinganishwa na Oktoba 4, 2024, Dola iliuzwa kwa Sh2,721.68 na ikaimarika hadi Sh2,716.48 kufikia Oktoba 23. Hali hiyo iliendelea hadi kufikia Sh2,620.57 mwishoni mwa Novemba.

Tutuba alisema hali hiyo imechangiwa na sekta ya nje kuendelea kuimarika, ikichangiwa na ongezeko la mauzo ya mazao ya biashara nje ya nchi, utalii na dhahabu, pamoja na kupungua kwa bei za mafuta ghafi katika soko la dunia.

Hali hiyo ilifanya nakisi ya urari wa malipo ya kawaida kwa Tanzania Bara kupungua hadi asilimia 2.4 ya Pato la Taifa kwa mwaka unaoishia Septemba 2025, kutoka asilimia 3.8 ya Pato la Taifa kwa mwaka uliotangulia.

Kwa upande wa Zanzibar, ziada ya urari wa malipo ya kawaida iliongezeka hadi Dola milioni 685.6 za Marekani kwa mwaka ulioishia Septemba 2025, kutoka Dola milioni 499.0 mwaka uliotangulia, kutokana na ongezeko la mapato ya huduma hususan shughuli za utalii.

“Kuimarika huku kwa sekta ya nje kulichangia ongezeko la ukwasi wa fedha za kigeni katika uchumi na kuimarika kwa thamani ya Shilingi. Hiyo ni baada ya Shilingi ya Tanzania kuendelea kuwa imara, huku thamani yake ikiongezeka kwa asilimia 8.4 katika robo ya tatu ya mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 0.7 katika robo mwaka iliyotangulia,” alisema Tutuba.

Hali hiyo ilifanya akiba ya fedha za kigeni kuendelea kuwa ya kutosha, ambapo mwishoni mwa Agosti 2025 ilifikia Dola milioni 6.4, kiwango kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa zaidi ya miezi mitano, sanjari na lengo la nchi na vigezo vya kikanda kwa EAC vya miezi 4.0 na 4.5, mtawalia.

Ukwasi wa fedha za kigeni unatarajiwa kuendelea kuongezeka kutokana na mauzo ya korosho na dhahabu, pamoja na shughuli za utalii.

Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi, amesema kuimarika kwa Shilingi ni jambo jema kwani uchumi wa Tanzania unategemea vitu vingi kutoka nje, hali inayofanya gharama za uagizaji ikiwemo mafuta kupungua.

“Gharama za uagizaji bidhaa zikipungua, zinapunguza pia gharama za uzalishaji na usafiri, hivyo husaidia katika kuwawezesha wananchi kiuchumi,” amesema.

Hata hivyo, amesema jambo hilo lina pande mbili kwani linaweza kuwa na maumivu kwa watu wanaouza bidhaa nje ya nchi, kwa sababu sasa watapata fedha kidogo.

“Ni kama inaumiza wauzaji wa bidhaa nje. Inatakiwa kuwa sawa, isisuke sana na isipande sana. Ikiwa inapanda na kushuka kila wakati, inaweka ugumu kwa mtu kufanya makadirio kama anataka kuwekeza au kuuza nje,” amesema Dk Olomi.

Amesema Shilingi ikiimarika zaidi inaweza kuvunja moyo watu kuuza nje, lakini kama watu wanapata nafuu katika kuingiza bidhaa inaweza kuweka msawazo.

“Shilingi ikiimarika inachukua muda hadi faida imfikie mzalishaji, kwa sababu mzalishaji akiuza anapata hasara,” amesema.

Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Lawi Yohana, amesema kuimarika huku kunamaanisha kuwa uchumi umekuwa kwa kiwango kilichokusudiwa, hali inayotokana na mauzo ya nje kuongezeka.

“Mauzo yameongezeka hasa kwenye utalii na mazao mbalimbali ya kilimo na madini. Hivi kwa pamoja vimefanya thamani ya Shilingi kuzidi kuimarika, na hii imethibitisha kuwa tumepunguza utegemezi kutoka nje ya nchi,” amesema Dk Lawi.

Ametolea mfano wa kuongezeka kwa matumizi ya gesi asilia kunavyochangia kupunguza utegemezi wa nishati ya mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi, hali inayofanya Shilingi ya Tanzania kuendelea kuimarika.

“Hii inafanya hata kiwango cha fedha za kigeni kuendelea kuongezeka, kwa sababu kuna shughuli mbalimbali zinaendelea ikiwemo utalii. Hili ni jambo zuri hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi ambacho tulitegemea kuwa uchumi ungeyumba, lakini inaonekana kuna usimamizi mzuri wa sera zetu za fedha,” amesema.

Ili kufanya thamani ya Shilingi kuendelea kuwa thabiti, alitaka bidhaa za ndani zitumike zaidi kuliko zile zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika uagizaji.