Mtanzania anakitaka kiatu Misri | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Oscar Evalisto anayekipiga Makadi FC amesema mipango yake msimu huu ni kuchukua kiatu cha mfungaji bora kwenye ligi hiyo.

Hadi sasa mshambuliaji huyo amecheza mechi tatu akifunga mabao matatu na asisti moja akiisaidia timu hiyo kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Evalisto amesema anatamani ananyakue tuzo hiyo na kuisaidia Makadi FC kupanda Ligi Daraja la kwanza msimu ujao ambayo ndio malengo makuu ya timu hiyo.

“Kila ninapopata nafasi napambana ili kuhakikisha natimiza malengo yangu, msimu uliopita sikuanza vizuri kutokana na kuchelewa kujiunga na timu naamini kama nitaendelea kupata nafasi ya kucheza nitatimiza kile nilichokipanga,” amesema Evalisto na kuongeza;

“Malengo ya timu kupanda kucheza Ligi Daraja la kwanza na msimu huu timu imejiandaa vyema kuanzia usajili kila kitu ili kuhakikisha msimu ujao tunakwenda kupambana na vigogo.”

Huu ni msimu wa pili kwa mshambuliaji huyo kuitumikia Makadi. Msimu uliopita alicheza miezi sita akitokea Mlandege na aliwahi kupita Paje Star ya Zanzibar na Lipuli U-20.

Msimu wake wa kwanza alicheza mechi nne akifunga mabao matatu na asisti moja akisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 27.