Dodoma. Wakazi wa mtaa wa Nzuguni B jijini Dodoma wamevamia nyumba moja ambayo wanaishi vijana 23 wakimtuhumu mojawapo kuwa amekuwa akiwaingilia wanawake bila ridhaa yao nyakati za usiku.
Hata hivyo, askari Polisi wenye silaha mapema leo Jumapili Oktoba 5,2025 wakiwa kwenye magari matatu walifika haraka na kuondoka na vijana 23 ambao walidai kuwa wameletwa na shirika mojawapo kwa ajili ya kujifunza namna ya kuuza bidhaa mtandaoni.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nzuguni B Isaya Mahiga amesema mapema alfajiri ya leo alipokea simu kutoka kwa mmoja wa wananchi akieleza namna alivyovamiwa na mtu akitaka kumbaka.
Amesema mara moja aliwasiliana na ofisa wa Polisi Kata na walipofuatilia nyumba hiyo walibaini chumba kimoja kinaishi watu zaidi ya 23 ambapo miongoni mwao alikuwepo mtu waliyekuwa wakimtuhumu.
Mahiga amesema vijana walijikusanya na kuanza vurugu za kutaka wamtoe mtu aliyetuhumiwa huku wanawake wakiangua vilio kwamba wamenyimwa haki ya kumuona waliyemuita mbaya wao.
“Tunashukuru Polisi walifika kwa haraka maana vurugu zilianza kujitokeza watu wakaanza kurusha mawe wakitaka waachiwe washughulike na vijana hao huku wakiwa wamebeba silaha za jadi,” amesema Mahiga.
Amesema vijana hao na wengine wametajwa kutoka mikoa ya Mara, Kagera na Kigoma na wapo kwenye moja ya kampuni inayowafundisha kufanya biashara mtandao, lakini maisha yao ni magumu.
Akizungumza namna ilivyokuwa, Tina Masele amesema saa 9 usiku akiwa amelala ghafla kitandani alimuona huyo kijana akipanda kitandani na alipomuhoji alimwambia akae kimya vinginevyo angemuua kwa kisu.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nzuguni B Isaya Mahiga akiwa juu ya gari la Polisi akizungumza na wananchi waliokuwa na hasira wakitaka mtuhumiwa wa ubakaji atolewe wamuone.
Tina amesema alipata ujasiri mkubwa wa kupiga yowe kwa nguvu ndipo kijana huyo akakimbia lakini majirani walimkimbiza hadi akaingia ndani ya jengo hilo, ambapo walilizunguka kisha wakaita viongozi na walipofika wakabaini nyumba hiyo yenye vyumba viwili kulikuwa na vijana zaidi ya 23 wakiishi.
Naye Catherine Samwel amesema kuwa imeshatokea zaidi ya mara mbili kwake wanaingia usiku vijana na kuwatishia ili wanyamaze na kuwaachia watimize malengo yao.
Catherine amesema mtaani kwao siyo mara moja au mbili bali imekuwa ni matukio ya mara kwa mara lakini hawajawahi kuwakamata wahusika, ingawa taarifa wameshapeleka kwa viongozi na Serikali.