Kathmandu. Watu zaidi ya 40 wamefariki dunia na wengine hawajulikani walipo baada ya kutokea kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini Nepal.
Mafuriko hayo yamesababishwa na mvua kubwa iliyoanza kunyesha tangu Ijumaa Oktoba 03, 2025 na kusababisha vifo, watu kutoweka na kusababisha uharibifu wa miundombinu ikiwemo barabara na madaraja.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Reuters, Msemaji wa mamlaka ya kudhibiti maafa nchini humo, Shanti Mahat amesema hadi kufikia asubuhi ya leo Jumapili Oktoba 05, 2025 tayari watu 47 wamethibitika kufariki dunia.
Pia watu tisa hawajulikani walipo huku wakisisitiza shughuli za uokoaji zinaendelea.
kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi wa Nepal, Kalidas Dhauboji mvua hizo kubwa zimesababisha maporomoko ya ardhi ambayo yamefanya baadhi ya barabara kuu kufungwa na hivyo kufanya mamia ya wasafiri kukwama.
Pia katika mji wa Kathmandu, mito kadhaa imefurika na kufunika baadhi ya barabara na makazi ya watu.
Dharmendra Kumar Mishra, gavana wa eneo la Sunsari, amesema milango yote 56 ya Bwawa la Koshi imefunguliwa ili kupunguza maji, ikilinganishwa na milango 10 hadi 12 pekee ambayo hufunguliwa katika hali ya kawaida, na mamlaka zimepiga marufuku magari kupita kwenye daraja hilo.
Msemaji wa uwanja wa ndege wa Kathmandu, Rinji Sherpa amesema safari za ndege kwenda mataifa mengine zinaendelea kama kawaida.
Wataalamu wa hali ya hewa wamesema mvua hizo zinatarajiwa kuendelea hadi kesho Jumatatu Oktoba 6,2025 hivyo kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.