Mwenge wakagua barabara ya Sh115 milioni Mbozi

Songwe. Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi amewataka wananchi wa Wilaya ya Mbozi kuunga mkono jitihada za Serikali katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Hasamba, wilayani Mbozi baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Veta kwa kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilomita 1.8, amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila ubaguzi.

“Maendeleo yanayoshuhudiwa hapa ni juhudi za Serikali ya Rais Samia kuhakikisha kila mwananchi, bila kujali nafasi yake, ananufaika na miradi ya maendeleo,” amesema Ussi na kuongeza kuwa amejiridhisha kwa asilimia 100 na ubora wa kazi ya mradi huo.

Barabara hiyo inajengwa kwa gharama ya Sh115.8 milioni kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mbozi, ambapo inatarajiwa kurahisisha usafiri wa wanafunzi na wakufunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) na Chuo cha Uuguzi Mbozi, pamoja na kuunganisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, amesema lengo kuu la mradi huo ni kumuunga mkono Rais Samia baada ya kutoa Sh6.5 bilioni za ujenzi wa chuo cha Veta.

“Barabara hii si tu itasaidia taasisi, bali pia ni nyenzo ya kuchochea maendeleo ya wananchi, hasa kwenye usafirishaji wa mazao kama mahindi, kahawa, mbogamboga na mazao mengine kutoka mashambani kwenda viwandani, maghalani na masokoni,” amesema Mbega.

Wananchi wakishuhudia uwekaji jiwe la msingi katika jengo la polisi kata ya Ihanda wilayani Mbozi. Picha na Denis Sinkonde



Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Mbozi, Mhandisi Lyoki Mwita, amesema mradi huo ni sehemu ya mkataba wa ujenzi wa jumla ya barabara tatu zenye urefu wa kilomita 3.85 kwa gharama ya Sh214.3 milioni.

Amezitaja barabara nyingine kuwa ni ya Mwenge (kilomita moja) yenye thamani ya Sh67.1 milioni na barabara ya Old Vwawa (kilomita moja) yenye thamani ya Sh38.1 milioni.

Mhandisi Mwita amesema mradi unatekelezwa na kampuni ya S.A Investment Limited, ambapo tayari kazi za kufukia mifereji, kuchimba mifereji ya maji ya wazi (kilomita 0.57) na kuweka tabaka la changarawe kwa kilomita 1.70 kati ya 1.85 zimekamilika.

“Hadi sasa mkandarasi amelipwa Sh51.3 milioni kwa kazi zilizotekelezwa,” amesema Mwita.