Vigogo Bodi ya chai watua Rungwe sakata la wafanyakazi

Mbeya. Siku moja baada ya Mwananchi kuripoti taharuki katika eneo la Katumba, wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, kufuatia wafanyakazi 216 wa kiwanda cha wakulima wa zao la chai Rungwe kugomea kufukuzwa kazi, Serikali imeingilia kati na kuwataka wasubiri hatima yao leo.

Oktoba 2, 2025, taharuki ilitanda kiwandani hapo kutokana na wafanyakazi hao kuandamana kwa mabango kupinga kufukuzwa kazi wakidai stahiki zao, huku wakiiomba Serikali kuingilia kati.

Alhamisi, Oktoba 2, 2025, wafanyakazi hao 216 wa kiwanda hicho waliandamana kwa mabango kupinga kufukuzwa kazi na waajiri wa kiwanda hicho, Tatepa na Maris Afrika, wakishinikiza kulipwa stahiki zao zaidi ya Sh2.17 bilioni.

Wafanyakazi hao walisema msimamo wao ni kuendelea na kazi hadi waajiri wao Tatepa na Maris Afrika (wawekezaji kiwandani hapo) watakapowalipa stahiki zao.

Mbali na msimamo huo wa kutoondoka kazini, waliiomba Serikali kuingilia kati kwa kuwa tangu kufungwa kwa kiwanda hicho Mei 9, 2025, zaidi ya wakulima 15,000 wameathirika na baadhi wameanza kutelekeza mashamba yao, huku wengine wakihamia kilimo cha mazao mengine, hali iliyouathiri uchumi wa wilaya hiyo.

Jana Jumamosi, Oktoba 4, 2025, Bodi ya Chai nchini chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Beatrice Banzi, aliiongoza timu ya watendaji wa bodi hiyo kufika kiwandani hapo kusikiliza kero za wakulima na wafanyakazi hao.

Katika kikao kifupi kilichoshirikisha viongozi wengine wa Serikali, akiwamo Katibu Tawala wa Wilaya ya Rungwe, Ally Kiumwa, pamoja na mambo mengine wameazimia kusubiri majibu ya mwajiri aliyesema atayatoa kesho, Jumatatu, Oktoba 6, 2025.

Beatrice amesema Serikali ipo pamoja na wafanyakazi hao kuhakikisha haki zao inapatikana, huku akiwaomba wawe watulivu kwa kuwa Serikali haitawaacha.

“Nimeamua kufika mwenyewe na baadhi ya watendaji wa bodi, akiwamo mwanasheria Godfrey Exaud, baada ya kusikia taharuki hii. Kimsingi Serikali iko makini muda wote, na tuwaombe wafanyakazi watulie hadi Jumatatu,” amesema Beatrice.

“Tumesikiliza changamoto ilivyokuwa, hivyo tutakuwapo na mamlaka nyingine kusikiliza. Serikali ipo pamoja nao kuhakikisha haki yao inapatikana; watulie, wawe wavumilivu,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa zao hilo Rungwe na Busokelo (RBTC), David Mwamakasi, ameipongeza bodi hiyo kwa hatua za haraka, akieleza kuwa matarajio ni kuona hali iliyotokea ikiisha salama.

“Nimpongeze na kumshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Bodi kwa hatua za haraka alizochukua kufuatilia sakata hili, na tunaamini litaisha salama kwa kuwa Serikali imefika,” amesema Mwamakasi.