SIMBA itarejea kambini Oktoba 5, 2025 ili kujiandaa na mechi zilizopo mbele yao Ligi Kuu Bara na ile ya kimataifa ikiwa imetinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kuna jambo limefanywa na mabosi wa klabu hiyo baada ya kutakiwa kutafuta uwanja nje ya Benjamin Mkapa.
Katibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alinukuliwa juzi akizitaka Simba na Yanga kutafuta uwanja kwa mechi zao za Ligi Kuu, kwani Kwa Mkapa utatumika kwa mechi za kimataifa tu na zile kubwa za dabi tu.
Jambo hilo limewafanya mabosi wa Simba fasta kufanya maamuzi ya kukimbilia Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo unaomilikiwa na jeshi kama uwanja wao wa nyumbani badala ya Kwa Mkapa.
Msimu uliopita Simba iliutumia Uwanja wa KMC Complex kwa mechi za nyumbani ikiwa sambamba na watani wao, Yanga lakini safari wameamua kukimbilia jeshini.

Muonekano wa uwanja wa Mej. Jen. Isamuhyo wakati wa usiku
Chanzo kutoka Simba kilisema klabu hiyo itacheza mechi nyingi za Ligi Kuu usiku na wameupigia hesabu Uwanja huo wa Isamuhyo ambao umefanyiwa marekebisho makubwa ikiwamo kufungwa taa, ili kuruhusu kutumika usiku kama ilivyoshuhudiwa katika mechi ya JKT Tanzania dhidi ya Azam FC ulioisha kwa sare ya bao 1-1 wiki iliyopita.
“Tumeuchagua uwanja huo kwa sababu una taa na mechi nyingi tutatakiwa kuzicheza usiku, hiyo ndiyo sababu ya kuuhama wa KMC tuliokuwa tunautumia msimu uliyopita kama uwanja wa nyumbani,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Simba itaweka wazi kuhusu mabadiliko hayo, kwani kwa sasa akili na nguvu zinaelekezwa katika mechi zilizopo mbele yetu hasa ya kimataifa tunayohitaji ushindi ugenini.”
Ratiba ya Ligi Kuu Bara iliyosimama kwa wiki mbili inaonyesha Simba itacheza dhidi ya Azam FC nyumbani inayohesabika kama dabi, hivyo itatumia uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya hapo itacheza mechi tano mfululizo ugenini hadi mwakani ndipo itakapokutana na Mtibwa Sugar mwakani ikiwa nyumbani inapoweza kutumia uwanja wa Wanajeshi hao.
Wakati Simba inauhama uwanja wa KMC, inadaiwa watani wao wa Yanga wenyewe wataendelea kusalia hapo katika mechi za nyumbani.